KIKOSI cha timu ya taifa ya maboresho leo kimefungwa mabao
2-1 na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23 ya Burundi katika mchezo wa
kirafiki wa kimataifa uliofanyika kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam.
Katika mchezo huo
timu zote mbili zilianza mpambano huo kwa kasi huku kila upande ukisoma mbinu
za wapinzani wao ili kuweza kupata bao la mapema.
Vijana wa Tanzania ndio waliokuwa wa kwanza kulifikia lango
la wageni wao Burundi na kupoteza nafasi ya wazi kupitia kwa mshambuliaji wake
Kelvin Friday ambaye katika mchezo huo alionekana kutokuwa makini kwa kupoteza
nafasi nyingi alizozipata.
Kufuatia kosakosa hizo za vijana wa maboresho Burundi wanao
nolewa na kocha Mjerumani Wilfried
Rainer, walitulia na kupanga vyema mashambulizi yao lakini walijikuta
wakifungwa bao la mapema na mshambuliaji Rashidi Yusufu aliyefunga kwa kichwa
akiunganisha krosi ya Gidaeli Michael.
Kuingia kwa mabao hilo kulionekana kuizindua Burundi na
kuanza kuonyesha makucha yao kwa kufanya mashambulizi mengi katika lango la
Tanzania na dakika ya 18 nusura Fabrise Nininahazwe aisawazishie timu yake
baada ya kupiga shuti kali lakini likapanguliwa kiufundi na kipa Aishi Manuna
na kuwa kona.
Jitihada za wachezaji wa Burundi zilizaa matunda baada ya
kufanikiwa kusawazisha bao hilo katika dakika ya 25 lililofungwa na
Ninihazwe,aliyemtoka beki wa kushoto wa Tanzania Miraji Adam na kufunga
kirahisi.
Bao hilo lilionekana kuivuruga kabisa Tanzania iliyokuwa
chini ya kocha Mart Nooij, na kuwaacha Burundi wakiutawala mchezo huo na
Ninihazwe, aliyekuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Tanzania nusura aifungia bao
la pili timu yake baada ya mpira wakichwa alioupiga dakika ya 32 kudakwa na
Manula na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 1-1.
Kipindi cha pili Vijana wa kocha Rainer, walionekana kupania
kuibuka na ushindi wa ugenini baada ya kuanza kwa kasi huku wakiutawala mchezo
na kuliandama lango la Tanzania na kupoteza nafasi nyingi za mabao walizozipata
.
Katika dakika ya 57 mshambuliaji wa Burundi Laudit Mavugo,
alikosa bao la wazi akiwa amebaki yeye na kipa wa Tanzania lakini mpira wa
kichwa alioupiga ulipanguliwa na kipa huyo na kuwa kona isiyokuwa na mazara.
Katika kipindi hicho cha pili kikosi cha Tanzania
kilionekana kuzidiwa kabisa hasa eneo la kiungo na kuwaacha wapinzani wao
Burundi wakicheza wanavyo taka kitu ambacho kilisababisha wapate bao la pili
dakika ya 78 mfungaji akiwa Nassoro Niyunkuru alimalizia kwa shuti kali krosi
ya Fiston Abdulrazak.
Pamoja na Tanzania kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji
kwa kumtoa Friday na kumuingiza Shiza Ramadhani, Omar Njenje lakini timu hiyo
haikuweza kupata bao la kusawazisha.
Zikiwa zimesalia dakika 10 mpambano huo kumalizika Tanzania
ilionekana kuzinduka na kufanya mashambuliaizi mengi kwenye lango la Burundi
lakini wapinzani wao walijipanga vyema na kuondosha hatari zote langoni mwao.
Tanzania: Aishi Manula Adam Miraji,Gidael Michael,Jorome
Mgeveke/Emmanuel SemwandaEndrew Vicent,Salim Mbonde,Rashind Yusufu/Omari
Njenje,Hassan Banda,Atupele green, Klevin Friday/Abubakar Mohamed,Hussein
Moshi.
No comments:
Post a Comment