Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
imepitisha usajili wa Ligi Daraja la Pili (SDL) huku ikikata majina mawili ya
wachezaji katika klabu za Abajalo ya Dar es Salaam na Magereza ya Iringa.
Klabu hizo mbili zilisajili wachezaji 31
badala ya 30 ambapo ni kinyume na Kanuni ya 61(2) ya Ligi Daraja la Pili
inayoruhusu klabu kusajili wachezaji wasiozidi 30 na wasiopungua 18.
Wachezaji ambao Kamati ya Sheria iliyokutana
jana (Novemba 11 mwaka huu) imewaondoa ni wale waliokuwa wameorodheshwa namba
31 katika usajili wa klabu hizo. Wachezaji hao ni Andrew Mathew Kazembe
(Abajalo) na Joshua Omari (Magereza).
Michuano ya Ligi Daraja la Pili
inayoshirikisha timu 24 katika makundi manne ya timu sita kwa mtindo wa
nyumbani na ugenini itaanza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu.
Wachezaji waliopitishwa katika kila
klabu na idadi yao kwenye mabano ni Abajalo (30), Arusha FC (18), Bulyanhulu
(28), Kariakoo (30), Kiluvya United (23), Magereza (30), Mbao (27), Milambo
(29), Mji Mkuu (29) na Mkamba Rangers (30).
Wengine ni Mpanda United (29),
Mshikamano (28), Mvuvumwa (18), Njombe Mji (25), Pamba (24), Rwamkoma JKT (25),
Singida United (26), Town Small Boys (22), Transit Camp (28), Ujenzi Rukwa
(30), Volcano (25) na Wenda (20).
No comments:
Post a Comment