TIMU ya Simba inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki na KMKM ya
Zanzibar Septemba 6, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo itakuwa ni ya pili kwa mabingwa hao wa zamani wa
Ligi Kuu Bara, ambapo Jumapili iliyopita walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya
Mafunzo ya Zanzibar na kuibuka na ushindi wa mabao 4-3.
Simba watatumia mechi hiyo kama moja ya maandalizi yao
kuelekea mchezao wao wa tatu kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa
Sugar, utakaopigwa Septemba 14, kwenye Uwanja wa Taifa.
Akizungumza jana, mratibu wa mchezo huyo, Rifati Said,
alisema KMKM ambao pia ni mabingwa wa soka Zanzibar, wanatarajiwa kuja kutafuta
na kulinda heshima yao mbele ya Simba.
Alisema kuwa maandalizi yote yapo tayari kwa ajili ya mechi
hiyo, ambapo kila timu imejipanga kuhakikisha inaibuka na ushindi.
Simba, ambao wananolewa na Kocha mzawa Abdallah Kibadeni ‘King
Kibadeni’, wanashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo, ikiwa nyuma
ya Mtibwa Sugar inayoshikilia nafasi ya tano na Coastal Union inayoshikilia
nafasi ya nne.
No comments:
Post a Comment