KOCHA Msaidizi wa JKT Ruvu, Azish Kondo, amesema hakuna timu
itakayowang’oa kileleni msimu huu, baada ya kufanikiwa kuwaondoa Yanga
waliokuwa wakishikilia nafasi hiyo.
Akifafanua kauli yake hiyo, Kondo alisema imekuwa kawaida kwa
kikosi hicho kuongoza ligi, lakini baada ya muda inashushwa na Simba, Yanga,
Azam na Mtibwa Sugar, jambo ambalo msimu huu wamelikataa kuona likitokea.
Alisema sababu zilizokuwa zinawafanya washushwe kileleni msimu
uliomalizika ni baadhi ya wachezaji wao kwenda katika mafunzo ya kijeshi na
kuwafanya kuchoka, lakini msimu huu
nyota wao wote tegemeo wamerejea na wapo vizuri.
“Kwa sasa wachezaji wetu wapo, hivyo tunajihakikishia kufanya
mambo makubwa msimu huu, tutang’ang’ania nafasi hiyo hadi mwisho wa ligi kwa
sababu nia yetu ni kutaka kupata ubingwa,” alisema.
Kikosi hicho kinaongoza ligi hiyo kikiwa na pointi 6, baada ya
kushuka dimbani mechi mbili na kufanikiwa kushinda zote, hali iliyowafanya
kuwashusha waliokuwa wanaongoza ligi hiyo, Yanga, ambayo sasa inashikilia
nafasi ya pili.
No comments:
Post a Comment