Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Monday, September 30, 2013

SABABU ZA MAN UNITED KUFUNGWA NA MAN CITY 4-1



 
MANCHESTER, England
NAHODHA wa Manchester City, Vincent Kompany, ametoboa siri iliyoifanya timu yao ikaibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya mahasimu wao, Manchester United, akidai ni kujituma kwao.
Anasema, timu nzima ilijituma siku hiyo kwa vile kila mmoja aliuona ushindi kwa City ulikuwa muhimu na wenye maana zaidi kuliko ilivyokuwa kwa United.
Ni kweli, kujituma huko kulionekana kulipa na kama wasingefanya hivyo, wasingeweza kushinda mechi yao. Lakini kwa wale walioitazama mechi hiyo vizuri, watakiri kwamba City, inayonolewa na kocha Manuel Pellegrini pia iliizidi Man United kwa kila idara uwanjani.
United ilionekana kupwaya kwa sababu ilikuwa na pengo kwenye safu yake ya ushambuliaji, kutokana na kutokuwepo kwa Robin Van Persie. Hata hivyo hiyo inaweza isiwe sababu kwani Man City ya Jumapili, ilikuwa sawa sawa.
Kabla ya mechi hiyo, City ya Pellegrini, haikuwa imewahi kuonyesha uzuri wowote na hakuna mtu ambaye angetegemea matokeo kama hayo, lakini kwa uchezaji ule, ilionekana kuwa ni timu iliyojipanga vizuri zaidi kushinda vigogo wote msimu huu.
Nahodha wake, Vincent Kompany na kiungo Yaya Toure walionekana kuwa wao ndio nyota wa mchezo kwa siku hiyo, baada ya kutawala safu ya ulinzi na dimba la kati kiasi cha kuwadhibiti kabisa United.
Kompany alimficha kabisa, Wayne Rooney kwa zaidi ya dakika 60, wakati Toure alikuwa kinara katika kupandisha mashambulizi yote ya City katikati ya dimba na kuifanya Man United kupoteana mara kwa mara.
Kiukweli, vita katika idara ya katikati ilikuwa kubwa lakini, Toure alionekana kuimudu vilivyo.
Toure amekuwa akitumiwa na Pellegrini kama kiungo mkabaji na kwa waliomuona siku hiyo watakubali uwezo wake. Alikuwa akizuia mashambulizi yote yasifike kwao na akatawala kwa kuudhibiti mpira usiende kwa maadui huku akipanda kuongeza nguvu.
Alifanya hivyo kwa dakika zote tisini, na matunda yake ya kupanda mbele yalionekana baada ya kwenda kufunga bao moja kati ya manne.
Uhuru wake wa kupanda na kushuka huku akisaidiana na Fernandinho, uliwafanya waonekane wameitimiza kazi yao ipasavyo, huku wakiwazidi Marouane Fellaini na Michael Carrick.
Pellegrini anaitaka timu yake icheze kwa kumiliki mpira muda mrefu na kwa kumtumia Toure, wamepata mchezaji sahihi wa kuwasaidia.
Alipiga pasi nyingi kuliko mchezaji yeyote wa timu yake, ambapo idadi inaonyesha kuwa aliwazidi kwa pasi 52 sahihi katika mchezo mzima na hadi hivi sasa anaongoza kwa wachezaji wote wa Ligi Kuu ya England.
Kabla ya mechi, ilidhaniwa kuwa winga wa City, Jesus Navas, angeweza kuwa 'sumu' dhidi ya beki wa kushoto wa United, Patrice Evra, ambaye alifikiriwa kuwa ndiye angekuwa mwiba wa kuanzisha mashambulizi.
Vile vile wengi walitarajia kuwa winga wa United, Antonio Valencia angeweza kuwa hatari kwa wapinzani wao hao kutokana na kucheza upande wa beki, Aleksandar Kolarov, ambaye hakabi sana.
Ukweli ukawa kwamba, katika upande huo, Valencia alifunikwa na badala yake Kolarov ndiye aliyeonekana kung'ara zaidi. Uchezaji wa pasi za haraka wa City ulikuwa hatari kwa Man United pande za pembeni, ambapo mabeki walikuwa wakipanda na kushuka muda wote, Kolarov akiongoza.
Bao la kwanza la City, lilikuwa ni mfano mzuri wa aina hiyo ya uchezaji.
Navas aliiba mpira na kuurudisha kwa kipa wake, Joe Hart. Baada ya kipa huyo kuondoa hatari, ulikwenda moja kwa moja kupigwa kichwa na Rio Ferdinand na kunaswa na Samir Nasri.
Nasri aliuchukua haraka na kumpasia Kolarov ambaye alikuwa akipanda kwa kasi, huku Valencia akishindwa kumkaba. Valencia alionekana mvivu kupita kiasi, pengine kutokana na kuzidiwa na akamuachia kazi Chris Smalling ya kuwadhibiti watu wawili, jambo ambalo hakuliweza na kusababisha kufungwa bao.
Sehemu nyingine ya sababu ni kwamba, Toure hakuwa na kazi kubwa ya kupasua katikati na hakuwa na hofu yoyote ya kuzuiwa na watu kama Fellaini au Carrick, hata kama wote wawili wangemfukuza nyuma yake.
Fellaini na Carrick walikuwa wakichunga zaidi pindi Toure alipokuwa akiwafuata na wakasahau kwamba walikuwa wanaachia mwanya kwa wachezaji wengine kuidhuru timu yao.
Haikutarajiwa kama Carrick angeweza kupanda mbele na hata Fellaini alipojaribu kufanya hivyo hakuweza kuleta madhara yoyote zaidi ya kile alichokifanya dakika ya 53 tu.
Toure na Fernandinho walimudu kucheza kama viungo huru, kwa sababu timu yao ilijipanga sawasawa katika idara hiyo na walikuwa na watu wa kazi upande wa ushambuliaji, kotekote kuanzia upande wa pembeni au katikati.
United haikufanya shambulizi lolote kutokea pembeni hadi City ilipokuwa mbele kwa mabao 4-0, ndipo waliposhtuka.
Katika dakika zote 45 za kipindi cha kwanza, Fellaini alionekana kujaribu kukaba tu, Danny Welbeck akawa kama mtoto yatima mbele peke yake na United haikuweza kuwa na madhara yoyote.
Ni kama vile Man United haikujua ni kwanini imeamua kumnunua mtu kama Fellaini na kumchezesha nafasi ya ukabaji wakati anapaswa kuwa kwenye nafasi ya ushambuliaji.
Katika mechi hiyo, United walipaswa kumtumia mbele badala ya ukabaji ili asaidie kupeleka mashambulizi kwa timu pinzani na hilo alilidhihirisha kipindi cha pili (dakika ya 68), alipoweza kupanda mbele na kumpa kipa wa City, Hart usumbufu wa kuokoa hatari yake ya kwanza kubwa.
Baada ya mechi kumalizika, takwimu zinaonyesha kuwa alikuwa miongoni mwa wachezaji waliomudu kugusa mpira mara nyingi zaidi hata alipohamia mbele kwenye eneo la wapinzani.
Lakini kwa upande wa ukabaji, alionekana kupotea na kushindwa kugusa baadhi ya mipira iliyokuwa ikiingia kwenye eneo lao na alifanya kosa la kumpoteza, Toure kwenye kona na kusababisha wafungwe bao la pili.
Pia analazimika kubeba lawama kwa kushindwa kuwasiliana na wenzake na kumruhusu, Sergio Aguero kumtoka na kufunga bao la tatu.
Uchezaji wa Rooney siku hiyo ulionekana kumkuna kocha wake, David Moyes ambaye alimsifia lakini, kwa kipindi hiki ambacho, Van Persie amekosa mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya England tangu atue Old Trafford mwaka 2011, tunaweza kuona ni jinsi gani Mholanzi huyo ana umuhimu kwenye kikosi cha Mashetani hao Wekundu.
Ni sawa na alivyo Kompany kwa upande wa Man City; haiwezi kuwa nzuri bila ya yeye kuwepo katika safu ya ulinzi.
Lakini swali ambalo mashabiki wanaweza kuendelea kujiuliza kuhusu Man United baada ya mechi chache za mwanzo msimu huu ni kwamba je, baadhi ya wachezaji wake wana uzuri kama unaofikiriwa? Kama mwedo wao utaendelea hivyo, hatutegemei iwapo timu hiyo itatwaa ubingwa.
Mabadiliko ambayo Moyes aliyafanya wakati timu yake ikiwa nyuma kwa mabao 4-0 kumuingiza Tom Cleverley badala ya Ashley Young, ilidhihirisha ni jinsi gani ina uhaba wa viungo wa ukweli kuweza kukabiliana na timu ngumu.
@ Ingekuwa vipi Ligi Kuu England bila ya Wenger?
LEO Jumatatu kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, anafikisha miaka 17 ndani ya klabu hiyo ya Emirates.
Lakini mwishoni mwa wiki alisheherekea kufikisha miaka hiyo 17, tangu atue kwenye klabu hiyo mwaka 1996 kwa kuichapa Swanasea City mabao 2-1.
Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, ambaye ni mchambuzi wa mtandao wa Daily Mail, aliandika kuhusiana na Wenger akisema: “Wote tunapaswa kuwa mashabiki wa Arsenal.”
Mawazo hayo hayawezi kukubaliwa na mashabiki wa White Hart Lane wala wale wa Stamford Bridge, Manchester hata wa Merseyside. Lakini msimu huu wote tunapaswa tuwe mashabiki wa Arsenal, aliandika Carragher.
Aliendelea kusema kuwa kama Arsenal watafanikiwa, basi hiyo ina maanisha Wenger atabaki Ligi Kuu England na ukweli ni kwamba anahitajika kubaki.
Filosofia ya Wenger imeleta mambo makubwa katika soka la England na soka lingekuwa bofu kama sio yeye.
Ligi ya England isingekuwaje kama kama sio Wenger? Klabu zisingefikiria kutafuta makocha wakigeni kwa haraka kama asingefanya lolote.
Mafanikio yake yamefungua milango kwa makocha wengine kutua England, tangu kuwasili kwake Arsenal mwaka 1996,  makocha 47 kutoka sehemu wameajiriwa kwenye klabu kubwa, ukilinganisha na makocha 120 wa England. Hiyo ni idadi ya ajabu.
Hakuna ubishi kwamba bila ya Wenger, kusingekuwepo na Jose Mourinho, Rafa Benitez, Roberto Mancini au Carlo Ancelotti.
Bila ya Wenger, isingewezekana kumuona Thierry Henry, Cesc Fabregas na Robert Pires na wachezaji wengine wengi kutoka nje, ambao wameweza kubadilisha soka la England.
Beki huyo wa Reds, alisema kuwa Wenger, ndiye aliyemtia hofu na kumfanya aongeze kiwango chake cha soka, wakati huyo akicheza mpira kabla ya kustaafu.
Arsenal alifanikiwa kutwaa mataji mbalimbali  kutoka mwaka 2002-2004, ambapo kikosi chake kilifanikiwa kuitwa kikosi kilisichofungika, baada ya kumaliza msimu bila ya kufungwa hata mechi moja.
Wachezaji wenye kiwango kizuri na wenye uwezo wa kukimbia — walikuwa na kila kitu. Hata wachezaji wa upinzi waliposimama nao kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, walianza kuogopa kabla ya mechi.
Walikuwa wachezaji wazuri na kuwa na timu ambayo ilikuwa ya kiufundi na nguvu kidogo. Ilikuwa ni timu ambayo imeungana pamoja kuanzia mlinda mlango hadi washambuliaji.
Wachezaji walikuwa wamejengeka kimwili na kama utajaribu kuwasukuma unaweza kuanguka mwenyewe.
Ikiwa unacheza beki wa kulia kwa timu pinzani, halafu ukakutana na Arsenal ya wakati huo, utakuwa na kazi ngumu, kutokana na kuwepo na wachezaji kama Henry, Ashley Cole na Pires.
Wachezaji hao walikuwa na uwezo wa kukufanya kitu kibaya kutokana na uwezo wao wa kukokota mpira kwa kazi  na kumfanya beki akose muda wa kufikiria cha kufanya.
Heshima ya Wenger ilikuwa juu, akiwa ameshinda taji la Ligi Kuu England, mataji mawili ya Kombe la FA na mengine mawili ya Ngao ya Jamii katika muda wa misimu mitatu.
Lakini kwa sasa anaweza kuonekana kituko kwa watu kwa kushindwa kunyakua hata taji moja katika miaka tisa.
Arsenal wameshindwa kushindana na Manchester City na Chelsea, kutokana na matumizi mabaya ya fedha, huku wengine wakiiga mfumo wa Wenger kununua chipukizi kutokana nje.
Ijumaa iliyopita kulikuwa na kauli ya kumuunga mkono kocha huyo, kutoka kwa tajiri mwenye hisa nyingi kwenye klabu hiyo, Stan Kroenke.
Lakini, huu si wakati wa kuanza kumsifia Wenger, bali mashabiki na wadau wanapaswa kusubiri hadi majira ya Krismasi. Kwa sasa ni mapema sana kusema kitu kwa Arsenal, ingawa wanaongoza Ligi Kuu England.
Bila ya shaka wana mambo mengi ya kuwathibitishia na wana kikosi cha ukweli kuweza kuvaana na Manchester City, Manchester United na Chelsea.
Ushindi mmoja walioupata dhidi ya mahasimu wao Tottenham, kikosi pekee chenye  upinzani ambacho Arsenal wamekutanana nacho, hautoshi kuwapima Gunners.
Wakiwa chini ya Wenger, wamefanikiwa kufuzu kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa muda wote wa miaka 16, lakini wameshindwa kunyakua Kombe la FA ama la ligi, pamoja na kuwepo ‘top four’, kutokana na kutokuwa wazuri.
Wengi wa mashabiki wanaweza kuwa wamechoshwa na Wenger kwa kuwa wanaijua klabu yao, lakini mara nyingi wale ambao wamekuwa wakimkasirikia pale timu inapovurunda ila ikifanya vizuri wamekuwa wakigeuka na kucheka baada ya kuona mazuri.
Mwanzoni mwa msimu, baada ya Arsenal kuchaowa mabao 3-1 dhidi ya Aston Villa, mashabiki wengi walianza kumzodoa kocha huyo. Wengi wakisema hakuna jipya, wanaonekana kuwa wadhaifu.
Lakini, kuwasili kwa Mesut Ozil, kumewasaidia kufanya vizuri na kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho.
Ozil ni mchezaji pekee mwenye kiwango kizuri, ambaye amewasili Arsenal siku kabla ya dirisha la usajili kufungwa na kuifanya timu hiyo kuwa ya kuvutia katika wiki za mwanzoni, lakini mambo yanaweza yakawa magumu wiki hii kwa kukutana na Napoli hapo kesho.
Lakini kuna maeneo muhimu ambayo yanatakiwa yawekwe vizuri kwenye kikosi hicho. Watakuwa kwenye matatizo kama mshambuliaji wao Olivier Giroud atapata majeruhi, lakini pia wanapaswa watoe ofa kwa ajili ya mlinda mlango wa Real Madrid, Iker Casillas au Victor Valdes wa Barcelona kwa ajili ya kuwasajili Januari mwakani, ili wawe na mlinda mlango mwenye kiwango wanaemhitaji.
Wanaweza wakamaliza wakiwa ‘top four’ tena. Lakini tumtarajie kumuona Wenger kuingia sokoni dirisha la usajili la January na kusajili wachezaji wengine wenye kiwango, ili waweze kupambana na kuweza kuwania taji.
Carrangha, alimaliza kwa kusema kuwa tunamtaka abaki, ili tupata kuona soka zuri zaidi la Arsenal na wachezaji atakaowazalisha.
Tunapaswa kuwaunga mkono Arsenal msimu huu. Wenger anahitaji kipindi kingine cha kunyakua mataji na wote tunapaswa kumtakia mafanikio mema, ili soka la England lipate kufanikiwa kutoka kwake.
Miaka ya Wenger, Arsenal
1996-97:  Nafasi ya tatu Ligi Kuu England
1997-98: Mabingwa wa li, Kombe la FA
1998-99: Mshindi wa pili wa ligi
1999-00: Mshindi wa pili wa Kombe Uefa na mshindi wa pili Ligi Kuu England
2000-01: Mshindi wa pili wa ligi na Kombe la FA
2001-02: Mabingwa wa li na Kombe la FA
2002-03: Kombe la FA na washindi wa pili wa ligi
2003-04: Mabingwa wa ligi
2004-05: Washindi wa pili wa ligi na Kombe la FA
2005-06: Washindi wa pili wa ligi
2006-07: Nafasi ya nne ya ligi na nafasi ya pili wa Kombe la Ligi
2007-08: Nafasi ya tatu  Ligi Kuu England
2008-09: Nafasi ya nne Ligi Kuu England
2009-10: Nafasi ya tatu  Ligi Kuu England
2010-11: Nafasi ya nne Ligi Kuu England, washindi wa pili wa Kombe la Ligi
2011-12: Nafasi ya tatu  Ligi Kuu England
2012-13: Nafasi ya nne Ligi Kuu England

No comments:

Post a Comment