Perez aliangalia mabao 203,
katika mechi 203, na kuamua kuvunja benki na kumfanya mtoto kutoka Madeira,
Cristiano Ronaldo dos Santos Aveiro, kuwa mchezaji anayelipwa zaidi sasa.
Ronaldo akiwa ameshasaini mkataba mpya mnono, ameendelea kuthibitisha thamani
yake kwa hat trick dhidi ya Galatasaray.
Katika taarifa iliyotolewa na
klabu ya Real Madrid, inasema mchezaji huyo amesaini mkataba wa miaka mitano
ambapo atakuwa anapokea kiasi cha pauni milioni 21 kwa mwaka, hivyo kumfanya
kuchukua kiasi cha pauni 403, 000 kwa wiki, kiasi ambacho kimezidi kwa pauni
milioni 1 kutoka kwa kile ambacho alikuwa anachukua mshambuliaji, Samuel Eto’o
katika klabu ya Anzhi Makhachkala.
Mchezo mzima ulichezwa na
wakala wake, Jorde Mendes, ambaye awali alikuwa anafanya mchezo wa kusema
mchezaji huyo anatarajia kurudi katika klabu yake ya zamani ya Manchester
United, tena akawa amepanga na mshahara kwamba klabu hiyo ipo tayari kulipa
kiasi cha pauni 300,000 kwa wiki.
Wachambuzi wengi wa soka hapo
awali waliamini ujio wa Gareth Bale katika klabu hiyo, ungeweza kumuondoa
mchezaji huyo na kurudi katika klabu ambayo kila siku amekuwa akisema kwamba
anatamani siku moja kurudi kucheza huko, kwani anaangalia kama
nyumbani kwake.
Lakini akili ya Perez ilikuwa
kwenye si tu uchezaji, aliangalia jinsi watu wa fedha wanavyomuangalia Ronaldo,
kwa ripoti za hivi karibuni, gharama za mchezaji huyo katika takwimu za
kifedha, zinaonyesha kwamba yamepanda na kufikia uero milioni 520.
Huku mchezaji huyo inaonyesha
ana mashabiki milioni 21.3 katika
mtandao wa Twitter, mashabiki milioni 60.4 katika mtandao wa facebook na
inasemekana amemzidi muajiri wake kwa asilimia 60, huku klabu hiyo ikiwa imeuza
zaidi ya jezi milioni 1 za mchezaji huyo katika mwaka wake wa kwanza.
Klabu ya Real Madrid baada ya
kuweka rekodi ya usajili wa kiungo wa zamani wa Tottenham, Gareth Bale kwa dau
la pauni milioni 86, ambalo liliweka rekodi ya manunuzi duniani, baada ya
kuvunja lile la Cristiano Ronaldo lililolipwa mwaka 2009 kwa klabu ya
Manchester United.
Bale alipowasili katika klabu
hiyo, alikuwa anakula kiasi cha paundi 160,000 sawa na Ronaldo, hiyo ilitosha kuwafanya
wachambuzi kuhisi kuwa huo ndiyo mwisho wa mchezaji huyo kuitumikia klabu hiyo
hasa baada ya mkataba wake kubakiwa na miaka miwili.
Kuonyesha kwamba ameridhika na
amefurahia kwa mchezaji huyo kuongeza mkataba, rais wa klabu hiyo ameliambia
gazeti la Marca kwamba, ubora, uzuri na umuhimu wa Ronaldo hauwezi kuonekana tu
kwa pasi 50 alizopiga, mabao 203 aliyofunga, mechi 203 alizocheza, bali wapi
aliitoa klabu hiyo na mpaka hapa alipoifikisha.
Wakati mshambuliaji wa
Barcelona, Mcameroon Samuel Eto’o anaondoka katika klabu ya Barcelona, watu
wengi walisema ilikuwa mbinu ya kumfukuza mchezaji huyo kwani Wahispania
hawakuwa tayari kuona rekodi za wachezaji wao wa zamani zinavunjwa na wageni,
lakini naona sasa imeshindikana kwa kuzuia kitendo hicho kufanyika kwa Lionel
Messi na Cristiano Ronaldo, kwani wachezaji hao kila mmoja kwa wakati wake
wamevunja rekodi kibao.
Ronaldo kwa sasa anakaribia
kuvunja rekodi ya mabao ya kipenzi cha mashabiki wa Real Madrid, Raul
Gonzalenz, ambaye wakati wa uchezaji wake, aliweza kufunga mabao 323 na tayari
ana mabao 203, aliyoyafunga katika kipindi cha miaka minne huku matarajio yake
ni kufunga mabao 200 zaidi kama alivyosema katika taarifa yake wakati anasaini
mkataba mpya.
Sioni kama itakuwa tabu au
hasira kwa mashabiki wa Real Madrid, kwa mchezaji huyo kuvunja rekodi ya Raul,
kwani pamoja na kwamba kuna wakati walikuwa wakimzomea uwanjani, wanatambua
fika kwamba mchezaji huyo ndiye tegemeo lao kwa sasa, wanajua fika kwamba kwa
kuwa majirani na wapinzani wao Barcelona wana Lionel Messi, basi wao wana
Cristiano Ronaldo na sasa wanatarajia kuona Bale akifunika sifa za Neymar.
Ninachokiona kwa sasa, Perez
amefanya kama kulipa fadhila kwa faida ambazo Ronaldo amekuwa akiingizia klabu
hiyo, pia kuhakikisha kwamba anashinda tena katika uchaguzi wa urais kwa awamu
ijayo, kwani wachezaji wengine ambao aliwanadi katika kampeni zake kama Ricardo
Kaka na Karim Benzema wameshindwa kumfanya aonekane alikuwa sahihi sana kuwasajili.
Kuonyesha nini matarajio yake
kwa Ronaldo na kuwashawishi mashabiki wa Real Madrid, rais huyo ameweka bayana
kwamba, Ronaldo ni muhimu kuliko mchezaji yeyote katika klabu hiyo na kuongeza
kwake mkataba kunamaanisha kwamba, makombe yanakuja katika klabu hiyo.
Wakati naisikia taarifa hii,
nilisema ingekuwa hapa kwetu, basi baada ya mechi kadhaa tungesikia wachezaji
wana mgomo baridi, kisa tu, kuna mchezaji kaambiwa muhimu kuliko yeyote, lakini
wenzetu wana heshima na wanajua nani kamzidi na nini kinafanyika wakiwa
uwanjani, ndiyo maana haikuwa kazi kubwa kwa Bale kusema pamoja na kuja katika
klabu hiyo, akiweka rekodi ya manunuzi na watu wengi wakiwa na matarajio
makubwa kutoka kwake, lakini bado anamchukulia Cristiano Ronaldo kama bosi
kwake na kwa klabu hiyo.
Kitu kingine ambacho, Perez
amekiangalia ni idadi kubwa ya mashabiki ambao watakuwa wakizidi kufurika
uwanjani kumuangalia Ronaldo, kama alivyofanya miaka minne iliyopita pale
aliposema: “Uwanja umejaa na hakuna
mechi inayochezwa ni uwepo wa Cristiano Ronaldo,” na bado anamuangalia mchezaji
huyo kama mtu muhimu katika mapato zaidi kwa
klabu hiyo.
Najua kitendo cha mchezaji huyo
kusaini mkataba mpya, kumezima ndoto za mashabiki wa Manchester United, ambao
ndoto yao kubwa ilikuwa kuja kumuona mchezaji huyo akirejea katika klabu yao
siku moja, lakini utajiri ambao ataupata Ronaldo, utakuwa ukiisaidia familia
yake na kizazi chake kwa maisha, lakini pia rekodi yake ambayo anataka kuiweka
katika klabu ya Real Madrid ikifanikiwa, itadumu daima, kwani bila ubishi,
sioni kama kuna mtu atakuja na kuwa na uwezo wa kufunga mabao mengi kama
wanavyofanya Messi na Ronaldo.
No comments:
Post a Comment