Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, August 11, 2013

YANGA YAKAMILIKA 100%


KUREJEA dimbani kwa wachezaji muhimu katika kikosi cha kwanza cha Yanga, kumekifanya kikosi cha timu hiyo, kukamilika kwa asilimia 100, huku wachezaji na benchi la ufundi wakitamba kufanya vizuri katika mechi zao zote zitakazowakabili mbele yao.

Kikosi cha Yanga kimekamilika wiki hii, baada ya kurejea kwa wachezaji wake, Mbuyu Twite ambaye ni beki, kiungo Frank Domayo na winga Simoni Msuva na kuifanya safu ya timu hiyo kutimia zaidi.
Kikosi cha Yanga kwa muda sasa kilikuwa kinawakosa nyota hao kutokana na kusumbuliwa na majeraha, hivyo kucheza mechi kadhaa bila nyota hao ambao ni tegemeo.

Twite, ambaye alikuwa na uvimbe kwenye mguu wa kulia, ameanza mazoezi mepesi tangu jana na kwamba hivi sasa anaendelea vizuri katika maandalizi yake, akijiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, hapo Agosti 17, mwaka huu.
Daktari wa timu hiyo, Nassor Matuzya, amesema kuwa Mbuyu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la uvimbe kwenye mguu wake ambao uliwekewa chuma, lakini sasa amepata nafuu na anaendelea vizuri na mazoezi.

Kwa mujibu wa Matuzya, mbali na Twite, wachezaji wengine wawili wa timu hiyo, Domayo na Msuva ambao walikuwa wagonjwa, wanaendelea vizuri baada ya kuanza mazoezi mepesi, huku hali zao zikionekana kuimarika zaidi tofauti na awali, ambapo sasa wataweza kucheza mechi za mwanzo za Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara msimu huu.
Nyota hao vijana kwa nyakati tofauti walikuwa wakisumbuliwa na malaria, hivyo kuifanya Yanga kuwakosa kwa wiki kadhaa, ingawa ujio wao ni mwelekeo mzuri wa kuimarika kwa kikosi hicho.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Ernie Brandts, anafanya kila linalowezekana kuhakikisha anapata matokeo mazuri katika siku zijazo, baada ya kuimarisha safu ya ushambuliaji.
Kuwepo kwa nyota hao sasa kunaifanya Yanga kuwa imara kwa asilimia 100, kutokana na nyota wote wa kikosi cha kwanza kuwepo kikosini, huku Hussein Javu na Mrisho Ngassa wakiongeza nguvu kwa wababe hao wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

Yanga imeonekana kuwa fiti katika idara zote, hasa baada ya ujio wa wachezaji wake nane waliokuwa kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Mashabiki wa Yanga sasa wamepata imani kwamba kikosi chao kimekamilika na kwamba kitatengeneza 'First Eleven' ambayo ni tishio.

Wachezaji wa Yanga waliokuwa kwenye kikosi cha Stars ni pamoja na kipa Ali Mustafa Barthez, mabeki David Luhende, Nadir Haroub Cannavaro, Kelvin Yondani, viungo Athumani Iddi 'Chuji', Domayo na Msuva pamoja na mshambuliaji Mrisho Khalfani Ngassa.
Yanga inaendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola, iliyoko Mabibo, jijini Dar es Salaam, chini ya kocha Brandts.

Yanga leo inakipiga na SC Villa ya Uganda, ambayo ilicheza na Simba jana katika maadhimisho ya tamasha la kila mwaka la 'Simba Day', ikiwa ni mechi yake ya mwisho ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Azam hapo Agosti 17, kabla ya kuanza kwa ligi Agosti 24.

Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema jana kuwa mechi hiyo ni fursa nzuri kwa kocha Brandts kuangalia uwezo wa vijana wake kabla ya kukutana na Azam.
"Tunatarajia itakuwa mechi nzuri na ya kuvutia na ni fursa nzuri kwa mashabiki wa timu yetu kuiona timu yao kwa kiingilio cha chini cha Sh 5,000/- kwenye mzunguko.

Jumapili iliyopita timu hiyo ilikipiga na Mtibwa Sugar na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, na kuwakuna mashabiki wake kwa kutandaza soka safi na ya kuvutia, ambapo mabao yake yalifungwa na mastraika Said Bahanunzi, Jerryson Tegete na Hussein Javu. Baadaye Alhamisi ikacheza na 3 Pillers ya Nigeria na kushinda 1-0.

Baada ya mechi hizo mbili, mashabiki wa timu hiyo walionekana kuvikubali vitu vya wachezaji wapya na wa zamani, ukiachilia mbali chachu itakayoongezwa na waliokuwa majeruhi, ambao wataifanya timu kuzidi kuwa kivutio.

No comments:

Post a Comment