LONDON, England
KATIKA kile ambacho kinaonekana ni kutaka kunusuru
kibarua chake, Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ametangaza kuvunja kibubu na
kukwangua pauni milioni 65 ili aweze kurejea tena kwenye soko la usajili.
Wenger ambaye kwa sasa amekalia kuti
kavu, baada ya timu yake kuanza msimu huu vibaya kwa kuambulia kichapo cha
mabao 3-1 dhidi ya Aston Villa alitangaza uamuzi huo usiku wa kuamkia jana huku
akisema kuwa bado anatafuta ufumbuzi mwingine na kwamba atazitumia fedha hizo
kwa ajili ya kusaka nyota wengine kwenye michuano hiyo ya Ligi Kuu ya England.
Kwa sasa Gunners imeshatangaza dau
la pauni milioni 12 ikimsaka kiungo wa timu ya Taifa ya Ufaransa, Yohan Cabaye
dau ambalo limekataliwa na Newcastle
ambayo inataka dau hilo liongezeke zaidi.
Hata hivyo kwa mujibu wa Starsport klabu hiyo iliyokumbwa na mgogoro
inawawinda nyota wengine watatu ambao huenda wakaigharimu pauni hizo milioni
65.
Wanaotajwa kuwa mawindo ya timu hiyo
ni nyota wawili wa timu ya Swansea,
Michu na Ashley Williams pamoja na nyota
wa Manchester City, Micah Richards, ambaye mwenyewe binafsi anataka kujiunga
na Gunners.
Awali kabla ya kutangaza nyota hao,
Arsenal iliwahi kujaribu kurusha karata
yake kuwashawishi nyota wengine kama
Luis Suarez, Wayne Rooney na
Gonzalo Higuain,lakini ikashindwa na badala yake kocha Wenger akajikuta akikaliwa kooni na mashabiki
kwa kushindwa kutumia fedha msimu huu.
Mfaransa huyo tayari ameshaomba
radhi kwa mashabiki kufuatia kipigo hicho cha mabao 3-1 kutoka kwa
Aston Villa ikiwa nyumbani na
usiku wa kuamkia jana aliwatumia ujumbe wa barua pepe uliosomeka:
"Tunataka mashabiki wetu wawe na furaha. Unaposhindwa kufikia mafanikio
hayo ni lazima ujihisi mnyonge na mwenyekuchanganyikiwa. Watu wanadhani
hatutaki kutumia fedha ila tunataka kuzitumia."
No comments:
Post a Comment