KLABU ya Al-Makhia ya nchini Qatar, imekubali kutoa kiasi
cha Dola la Kimarekani 40,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 62 za Tanzania ili
kukamilisha usajili wa kiungo Mwinyi Kazimoto, aliyetokea Simba ya Dar es
Salaam.
Akizungumza na LENZI YA MICHEZO, Balozi wa klabu hiyo kwa Tanzania,
Boniface Pawasa, alisema kuwa klabu yake imekubali kutoa kiasi hicho cha fedha
ili kukamilisha usajili wa Kazimoto ambapo katika mkataba wa makubaliano baina
ya Simba na klabu hiyo, Wekundu wa Msimbazi watakuwa wakipata asilmia 20 ya
mapato kila mchezaji huyo atakapokuwa anauzwa.
“Tumefanikiwa kukamilisha baadhi ya mambo ya msingi ambayo
yanamhusu mchezaji mwenyewe, lakini pia klabu ya Simba ambayo ndiyo
wanaommiliki.
“Tunaelewa kuwa aliondoka katika mazingira yasiyokuwa bora
kwa sababu kulikuwa na majukumu ya
kitaifa, lakini klabu yake haikuwa imeridhia lakini amewaomba radhi wadau wote
waliokwazwa na hali hiyo,” alisema
Pawasa, nyota wa zamani wa Simba ambaye pia alishaitumikia Al-Makhia inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza nchini
humo.
Mbali na kitita hicho, lakini kwa upande wa maslahi atakuwa
akipokea mshahara wa Sh milioni 15 kwa mwezi pamoja na marupurupu mengine ya
msingi ambayo yataendelea kuinua kipato chake.
Kwa upande wake, Kazimoto aliliambia Dimba kwamba kitendo
alichofanya si kizuri na anakiri kosa, hivyo anawaomba radhi Watanzania
wamsamehe na kwamba atakuwa balozi mzuri kwa nchi yake.
“Ni kweli nilifanya makosa, lakini naomba Watanzania
wanisamehe kwa kile kilichotokea, ila ilikuwa kwenye harakati za kutafuta
maisha tu,” alisema Kazimoto kupitia mtadao wa kijamii wa Facebook.
Mwinyi Kazimoto alisajiliwa na Simba katika usajili wa mwaka
2011 akitokea JKT Ruvu Stars ya mkoani Pwani, ambapo sasa kazi iliyobakia ni
Simba kutoa ruhusa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hufanya uhamisho wa
kimatifa ambao utaombwa na chama cha soka cha Qatar (QFA).
No comments:
Post a Comment