KATI ya Novemba 2008 hadi Machi 2009, mlinda mlango
wa Manchester United, Edwin Van der Sar, hakuruhusu bao hata moja liguse nyavu
zake.
Rekodi yake ya kutokufungwa ilikuja kuvunjwa na Samir
Nasri, wakati Man United walipopigwa mabao 2-1 na Arsenal ugenini. Kabla ya
mechi hiyo alikuwa amecheza jumla ya mechi 14 bila kufungwa, ambazo ni sawa na
dakika 1,311 (zaidi ya masaa 21), mara ya mwisho kufungwa ilikuwa na Peter
Lovenkrands wa Newcastle kwenye mechi iliyopigwa St. James’ Park.
Japokuwa rekodi hiyo alipewa Van der Sar, lakini
kiukweli siyo uwezo wake pakee ambao uliwaokoa kutokuruhusu bao kwenye kipindi
hiki. Timu nzima ilifanya vizuri na katika msimu huo walifungwa mabao 26 tu na
walishinda mechi zao nane kwa ushindi wa bao 1-0.
Mtu muhimu kwenye mafanikio haya alikuwa beki wa
kati wa timu hiyo, Nemanja Vidic.
Staa huyo wa Serbia alicheza mechi zote 14 ambazo
hawakuruhusu bao, mechi nane kati ya hizo alicheza sambamba na Rio Ferdinand,
licha ya kuzuia mabao pia alifunga mabao matatu na mawili kati ya hayo yalikuwa
ya ushindi.
Msimu huu alionyesha kiwango cha hali ya juu ambacho
hakuwahi kukionyesha hapo kabla na baada ya kipindi hicho, lakini kipindi
akionekana kuzidi kuthibitisha ubora wake na kutajwa kama beki bora Ligi Kuu
England akakutana na tatizo la majeruhi, kuanzia kigimbi, goti na mgongo na
kumfanya kucheza msimu mzima mara moja tu kwenye misimu minne iliyofuata.
Vidic alirudi kwenye kikosi cha Man United msimu
uliopita, baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeruhi.
Msimu wa 2011-12, alicheza mechi sita tu za ligi
kuu, hii ni baada ya kuumia goti katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi
ya Basel, alirudi kikosini Desemba mwaka jana na alilazimika kusubiri hadi Januari
kuwa fiti.
Baada ya kupona kabisa alirudi uwanjani kwenye mechi
dhidi ya Liverpool, Januari 13, (United walishinda 2-1 alifunga bao la
ushindi), alianza kwenye mechi 12 kati ya 16 za ligi kuu zilizokuwa zimesalia,
kati ya mechi hizo 10 United walishinda, moja wakafungwa na nusu ya hizo
walishinda bila kuruhusu bao langoni mwao.
Katika mechi 19 alizocheza msimu uliopita alikuwa na
wastani wa kuokoa hatari 10.5 kwa mechi, aliingilia pasi mbili kati kila mechi
na alifanikiwa kutengeneza mtego wa kuotea mara tisa.
Cha kufurahisha zaidi kuhusu uwezo wake ni kwamba
katika mechi zote hizo alipitwa mara mbili tu na adui, na pasi zake zilizofika
zilikuwa ni asilimia 87.4.
Kutokana na haya yote ndio maana kocha mpya wa Man
United, David Moyes, alimmwagia sifa Vidic, Jumanne hii wakati timu yake
ilipopata sare ya bao 1-1 na AIK katika pambano la kirafiki jijini Stockholm.
“(Vidic) alikuwa mtu muhimu zaidi kwetu – kufanikiwa
kucheza mechi nzima ni jambo zuri.” Alinukuliwa Moyes na mtandao wa klabu hiyo.
Na baada ya mechi hiyo Vidic mwenyewe alisema kwamba
sasa hivi yuko fiti kucheza msimu ujao wa 2013-14, baada ya kufanikiwa kupona
majeruhi yake yaliyomkosesha ziara ya ya timu yake Mashariki ya Mbali.
Sehemu kubwa ya mafanikio watakayoyapata Man United
msimu ujao yanatarajiwa kuchangiwa na kombinesheni ya Vidic na Ferdinand kwenye
ukuta wa timu hiyo.
Hii ni taarifa njema kwa United, hasa baada ya
kuchemka kufanya usajili mkubwa kwenye dirisha hili la usajili, wakiwakosa Thiago
Alcantara na Cesc Fabregas wakati huu wa kiangazi.
Man United wanahaha kuimarisha safu yao ya kiungo
ili kutengeneza ngao nzuri kwa mabeki wao, lakini kitendo cha kushindwa kufanya
usajili mkubwa mpaka sasa – huku mustakabali wa Wayne Rooney ukiwa bado
hauleweki – kuna uwezekano kabisa kurudi kwa Vidic uwanjani kukawa sawa na
usajili mpya kwenye kikosi cha Man United.
Ameshawahi kuonyesha hapo kabla jinsi gani beki wa
kati anavyoweza kuisaidia timu yake ishinde mechi, na lile tatizo la nani wa
kuokoa mipira ya juu pale United linakwisha kutokana na kurudi kwake.
No comments:
Post a Comment