KWA wafuatiliaji wazuri wa hekaheka za usajili
barani Ulaya, haipiti siku ambayo wamesoma au kusikiliza habari za usajili bila
kusikia sakata la Gareth Bale au Luis Suarez.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers, alinukuliwa na
mtandao wa Goal.com akisema: “Unahitaji kuangalia soko na kulinganisha dau la
pauni 40,000,001 (ofa ya Arsenal kwa Suarez), kisha kuangalia ofa ya zaidi ya
pauni milioni 100 ya Gareth Bale.”
Licha ya Liverpool kupinga kumuuza Suarez wakati huu
wa kiangazi, Arsenal bado hawajakata tamaa ya kumsajili Mruguay huyo. Wakati
huohuo, staa wa Tottenham Hotspur, Bale amewekewa mezani ofa ya pauni milioni 100
na Real Madrid, jambo ambalo lilisababisha Rodgers kulinganisha wawili hao.
Rodgers alidai kwamba Bale na Suarez walikuwa
wachezaji bora zaidi kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, hivyo haiwezekani
Bale akamzidi thamani Suarez kwa zaidi ya asilimia 100.
Sawa hayo ni mawazo ya Rodgers, lakini je, yana
mashiko? Kutokana na sakata la usajili la wawili hawa na ofa ya mamilioni ya
fedha iliyoko mezani kwa ajili yao, imezua maswali nani bora kati ya Luis
Suarez na Gareth Bale?
Nani ana thamani kubwa na nani atarudisha fedha yote
kama akihamia timu nyingine wakati huu wa kiangazi?
Kujibu maswali haya, vinaangaliwa vipengele vinne
muhimu na kujua yupi anamfunika mwenzake kwa ubora.
Mabao
Suarez amefunga mabao 30 kwenye mechi 44 akiwa na
Liverpool msimu uliopita, hivyo ana wastani wa bao 0.68 kwa mechi. Bale alifunga
mabao 26 katika mechi 45 na kuwa na wastani wa bao 0.57 kwa mechi.
Idadi ya mabao ya Suarez, inathibitisha kwamba ni
bora zaidi ya Bale, na hili lilitegemewa kwa sababu Mruguay huyo ni straika.
Alifunga asilimia 32 ya mabao ya timu yake, kulinganisha na asilimia 31 ya
Bale.
Matokeo:
Akiwa kama mshambuliaji, Suarez anaongoza kipengele hiki cha kucheka na nyavu
na amethibitisha ubora wake kwa kufunga kila kukicha.
Miaka
Suarez atatimiza umri wa miaka 27 Januari mwakani na
hapo atakuwa ndiyo anaingia kwenye kilele cha soka lake kama mchezaji. Kama Arsenal
wakimsajili wakati huu wa kiangazi watakuwa wamemnasa mchezaji aliye kwenye
kilele cha soka lake, na atakuwa na miaka mitatu mbele yake kabla ya kiwango
chake kuanza kuporomoka.
Bale amezidiwa na Suarez miaka miwili na nusu na bado
ana misimu kadhaa kabla ya kufikia kilele cha mafanikio yake. Kuwekeza kwa Bale
sasa hivi kutalipa kwa miaka sita.
Ukiangalia hilo dau la pauni milioni 100 ambalo Real
Madrid wako radhi kutoa kwa ajili yake itakuwa ni sawa na pauni milioni 16,6
kwa msimu mpaka atakapofika miaka 30, wakati Arsenal wakitoa ofa yao itakuwa ni
sawa na pauni 13.3 kwa msimu mpaka Suarez akifikisha miaka 30 pia.
Matokeo:
Licha ya ofa yake kuwa kubwa, lakini umri mdogo wa Bale unamfanya kuwa
uwekezaji mzuri zaidi. Uwekezaji wa Bale ni wa muda mrefu kuliko Suarez ambaye
bado kidogo sana kumaliza kwenye soka. Pia umri wake mdogo kulinganisha na wa
Suarez unaipa Madrid nafasi ya kumuuza siku za usoni na kurudisha sehemu ya
gharama walizomnunulia kama wakimchoka.
Mchango
Mabao ndio kitu muhimu kwenye timu yoyote. Uwezo wa
wote kufunga unajulikana, lakini vipi kuhusu mchango wa Bale na Suarez katika
kuwalisha wachezaji wenzao.
Suarez anacheza sehemu ambayo anatengenezewa zaidi
kuliko kutengeneza, msimu uliopita alitoa pasi za mwisho tano na zote hizo
kwenye ligi kuu. Bale yeye alipiga pasi za mwisho 10.
Matokeo: Kutokana na kucheza nyuma zaidi kuliko Suarez
eneo la kiungo, inategemewa kuona Bale akiwa ametengeneza mabao mengi zaidi
kuliko Mruguay huyo. Msimu uliopita alipika mabao 10 na hii inamaanisha Bale
alichangia jumla ya mabao 36 ukijumlisha na aliyofunga, wakati Suarez yeye
alichangia mabao 35, Bale ni bora zaidi kwenye kipengele hiki.
Muonekano
kwenye jamii
Siku zote mchezaji husajili kutokana na uwezo wake
uwanjani. Lakini ukiangalia ofa za fedha zinazotolewa ni lazima timu itaangalia
muonekano wa mchezaji kwenye jamii na tabia zake kwa sababu kwenye soka la
kisasa timu hutaka kurudisha fedha yao waliyoweka kwa mchezaji kupitia mauzo ya
haki za picha na jezi.
Inapoangaliwa tabia ya Suarez siku zote amekuwa
hajatulia na amekuwa akiandamwa na matukio ya kitata, sasa hivi ana adhabu ya
kufungiwa mechi 10 kwa kumng’ata beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic msimu uliopita.
Suarez pia amewahi kufungiwa mechi saba msimu
uliopita kwa kumng’ata mtu alipokuwa akichezea Ajax mwaka 2012. Pia amewahi
kukutwa na hatia ya kumbagua Patrice Evra mwaka 2011, na kufungiwa mechi nane.
Mwaka 2010 wakati wa michuano ya Kombe la Dunia
alidaka mpira kwenye mstari wa goli katika mechi dhidi ya Ghana, na alishangilia
sana baada ya Asamoah Gyan kukosa penalti hiyo na alipondwa na watu kutokana na
kushangilia kitendo chake hicho. Pia Suarez anatajwa kama mfalme wa kujiangusha
kusaka penalti.
Upande wa pili, Bale amekuwa mkimya sana, ni mara
chache sana amekutana na skendo za ajabu ajabu, amewahi kulaumiwa kwa kupenda
kujirusha na kusaka penalti, lakini linapokuja suala la wadhamini Bale anavutia
zaidi udhamini kuliko Suarez.
Matokea:
Bale
ni mshindi kwenye kipengele hiki kutokana na tabia za Suarez mara nyingi
hufunika uwezo wake uwanjani, wakati Bale yeye ameacha miguu yake ifanye kazi
na ndio maana alishinda tuzo zote binafsi katika Ligi Kuu England msimu
uliopita.
No comments:
Post a Comment