Liverpool,
England
MSHAMBULIAJI
wa Liverpool, Luis Suarez, amenyanyapaliwa na Kocha wa timu hiyo, Brendan
Rodgers, kwa kutoruhusiwa kufanya mazoezi na wenzake, kwa madai ya kutoiheshimu
klabu, jambo ambalo sasa limemfanya kujifua na mwanawe.
Juzi
ilidaiwa kuwa Suarez ndiye aliyekataa kujifua na wenzake, lakini jana siri hiyo
ilifichuka, huku Rodgers pia akipinga kauli ya nyota huyo wa Kimataifa wa
Uruguay kuwa aliahidiwa kuruhusiwa kuhama majira haya ya joto endapo Liverpool
haitafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Suarez,
26, pia amekerwa na kitendo hicho na sasa wiki hii amepanga kuwasilisha ombi
lake la kutaka kuondoka Anfield, endapo ataendelea kuzuiwa kuhama, na kama
haitoshi ataishitaki kwa Chama cha Soka England, FA.
"Hakuna
aina hiyo ya ahadi iliyofanywa, wala ahadi iliyovunjwa," alisisitiza
Rodgers, akimzungumzia Suarez, ambaye msimu uliopita alifunga mabao 30 katika
mechi 44 alizoichezea Liverpool.
Tangu
ajiunge na timu hiyo akitokea Ajax Januari 2011 kwa ada ya pauni milioni 22.7 (Sh.
bilioni 55 za Tanzania), ameifungia Liverpool mabao 51 katika mechi 96 alizoichezea.
Akiwa Ajax alifunga mabao 49 katika mechi 48, huku Uruguay akiifungia mabao 35
kwenye mechi 69.
"Liverpool
imekuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na wawakilishi wa Suarez na inajua wazi
mtazamo wake. Kwa ujumla kumekuwa na ukosefu wa nidhamu kwa klabu ambayo imempa
kila kitu."
Chanzo
kimoja kilichopo karibu na miamba hiyo ya Anfield, kilisisitiza kuwa uamuzi wa
Suarez kutakiwa kufanya mazoezi peke yake ulitolewa kabla hata hajaanza
'kubwatuka', ambapo alifanya hivyo Jumanne.
Rodgers
aliongeza: "Nitaendelea kuchukua maamuzi magumu. Nadhani Luis anatambua ni
kwa jinsi gani anapata sapoti kutoka klabuni, kitu ambacho amekuwa akikipata
kwa msimu mzima uliopita.
"Kazi
yangu ni kupigana katika kuilinda klabu. Mazungumzo ninayoyafanya kuhusu yeye
ninayo na yataendelea kubaki kuwa siri."
Arsenal
imeshatoa ofa mbili ambazo zimekataliwa na Liverpool, ya mwisho kati ya hiyo
ilikuwa ni pauni milioni 40 (Sh. bilioni 97.2 za Tanzania) na pauni moja zaidi
ambayo itaiwezesha kufikia kigezo cha kuweza kuvunja mkataba wa Suarez.
Hata
hivyo, Mkurugenzi wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa, Gordon Taylor alifafanua
kuwa hakuna kipengele katika mkataba wa mchezaji ambacho kinaeleza kuwa
Liverpool italazimika kumuuza endapo itapewa ofa zaidi ya pauni milioni 40.
"Kama
kutakuwa na ofa chini ya pauni milioni 40, pande mbili zitaketi na kuijadili,
lakini hauelezi kuwa klabu itamuuza," alisema Taylor.
No comments:
Post a Comment