Lakini ripoti hiyo inadai kwamba, Man United
watakuwa tayari kumuuza Rooney ikiwa tu, Mourinho atakubali kumjumuisha kiungo
wa Kihispaniola Juan Mata kwenye ofa yake.
Mourinho mwenyewe ameshaweza wazi kwamba,
atamfukuzia Rooney mpaka siku ya mwisho ya dirisha la usajili, lakini
akasisitiza kwamba akimkosa anaplan B na C, huku akigoma kuwataja wachezaji
ambao atawachukua kama akishindwa kumnasa Rooney.
Wachambuzi na mashabiki wa soka wamekuwa na mitazamo
tofauti kuhusu mchakato wa kumuhusisha Mata kwenye dili la kumnasa Rooney kuna
wanaoona Mourinho anachemsha.
Ili kujua nani analamba dume na nani anachemsha
kwenye dili hili, makala haya yanaangalia takwimu muhimu za kila mchezaji msimu
uliopita.
Mata alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Chelsea wa
mwaka, msimu uliopita, kutokana na kuwa na msimu mzuri sana, akifunga mabao
muhimu na kusaidia kupatikana kwa mengine mengi.
Mhispaniola huyo alifunga jumla ya mabao 12 kwenye
mechi 35 za Ligi Kuu England. Huku akifunga mengine nane kwenye michuano
mingine, hivyo alimaliza msimu na mabao 20 kwenye michuano yote.
Rooney naye alifunga mabao 12 ya ligi kwenye mechi
chache zaidi, lakini hakuweza kufikia idadi ya kutengeneza mabao kama ya Mata
msimu uliopita.
Mata aliwatengenezea wachezaji wenzake wa Chelsea
jumla ya nafasi 95, wakati Rooney alifanya hivyo mara 49 tu kwa msimu mzima.
Wachezaji wote wawili msimu uliopita, walicheza
kwenye nafasi moja kati ya tatu zilizonyuma ya mshambuliaji na walikuwa muhimu
sana kwenye mafanikio ya timu zote msimu huo wa 2012-13.
Japokuwa, Rooney hakutawala vyombo vya habari kama
alivyofanya Robin van Persie pale Man United, alikuwa na nafasi muhimu kwenye
kikosi cha Sir Alex Ferguson kilichorudisha taji la ligi kuu Old Trafford.
Mata pia alimfunika Rooney lilipokuja suala la
kugombea mipira, alishinda mipira hiyo kwa asilimia 55 wakati, Rooney kwa
asilimia 41 na hata kwenye kupiga pasi zilizofika Mata aliongoza pia, alipiga
pasi zilizofika kwa asilimia 85, huku Rooney akifanya hivyo kwa asilimia 83.
Kama ukipewa jukumu la kuchagua mchezaji na baada ya
kuona takwimu hizi ni wazi kabisa Mata atakuwa chaguo la kwanza. Amethibitisha
ubora wake kwamba ni mchezaji mzuri na mwenye tabia nzuri. Pia ana miaka miwili
chini ya Rooney.
Hakuna sababu ya msingi kwa Jose Mourinho kumtoa
kafara staa huyo, lakini hili linaweza kubadilika kutokana na nia ya dhati ya
Mreno huyo kumpata Rooney.
Takwimu zinaonyesha wazi kwamba, Mourinho atachemsha
kwa kumtoa Mata na fedha kwa ajili ya Rooney, huku Man United wakilamba dume
kutokana na ukweli kwamba, Rooney ameshaonyesha nia ya kutaka kuondoka Old
Trafford huku timu hiyo bado ikihitaji kiungo fundi kumchezesha RVP.
Lakini kwa upande wa pili wa shilingi, baada ya
kumuona Mata akicheza pambano la juzi dhidi ya Aston Villa na mfumo unaotumika
na Mourinho kwa sasa, hata kama akibaki kwenye timu hiyo hatafanya vizuri kama
msimu uliopita.
Inaonekana kama Mourinho ameamua kuimarisha zaidi
pembeni, hivyo ile nafasi ambayo Mata alikuwa nayo ya kucheza huru haitakuwepo
tena na Chelsea kwa sasa inahitaji straika wa kweli, kutokana na Fernando
Torres, Demba Ba na Romelu Lukaku kushindwa kuongoza mashambulizi ya timu hiyo.
Hivyo ujio wa Rooney kwenye timu hiyo hautatumika
kama kiungo bali atakuwa straika namba moja wa timu, kitu ambacho kitaongeza
nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo na kuifanya kuwa moto zaidi.
Man United wanaweza kufaidika zaidi kwa kumtoa
Rooney na kupata fedha na Mata, Mhispaniola huyo ataweza kuziba pengo la Rooney
kwenye idara ya utengenezaji, lakini kama siku RVP akiumia watapata tabu sana
mtu wa kucheza mbele na umuhimu wa Rooney utaonekana hapo.
Kwa kifupi uhamisho wa wawili hao ni sawa na
biashara kichaa kwa timu zote mbili kwa sababu kuna mawili wote wanaweza
kulamba dume au kuchemsha au mmoja kuchemsha na mmoja kulamba dume.
No comments:
Post a Comment