HADI sasa siku zinahesabika kabla ya kuanza michuano ya Ligi Kuu ya England, ambayo ni kati ya ligi zenye mashabiki wengi katika maeneo mbalimbali duniani.
Wakati siku zikiwa zinahesabika, tayari imeshuhudiwa baadhi ya timu zikifanya mabadiliko ya makocha kwa lengo la kuhakikisha msimu ujao zinafanya vizuri.
Katika msimu huu, timu tano zimeajiri makocha wapya ambao zinaamini watazisaidai katika kuwania ubingwa wa michuano mbalimbali England na pengine barani Ulaya.
Msimu huu imeshuhudiwa, David Moyes akiitema Everton na kujiunga na Manchester United baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Sir Alex Ferguson kutangaza kuachana na masuala ya ukocha na katika kuziba pengo la David Moyes, Everton wakaamua kumchukua, Roberto Martinez ambaye alikuwa akiinoa timu ya Wigan, na baada ya Stoke City kumtimua aliyekuwa kocha wake, Tony Pulis, wakaamua kumchukua kocha wa zamani wa QPR, Mark Hughes.
Mbali na timu hizo, Man City wao wamemchukua, Manuel Pellegrini baada ya kumfukuza, Roberto Mancini na baada ya Rafael Benitez kumaliza kibarua chake cha muda, Chelsea nafasi yake ikachukuliwa na 'Special One' Jose Mourinho, ambaye anadai amerejea nyumbani.
Makocha hao kila mmoja ana rekodi mbalimbali tangu waanze kufundisha soka na jambo hilo ndilo linawafanya wachambuzi wa masuala ya soka kuangalia rekodi hizo huku wakihoji kama wataweza kuendelea nazo.
Wakianza na Jose Mourinho (Chelsea)
Wanasema, Jose Mourinho amerejea mara ya pili kuinoa Chelsea.
Ujio wa kocha huyo umepokelewa kwa mikono miwili na mashabiki na wachezaji wa klabu hiyo ya jijini London.
Tangu aondoke kwenye klabu hiyo Septemba 20, 2007, Mourinho ameshafundisha klabu mbili kubwa ambazo ni Inter Milan ambako alitua Juni, 2008 na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia, Seria A na Kombe la Ligi ya nchi hiyo na msimu uliofuata akaiwezesha kutwaa ubingwa wa ndani wa Ligi Kuu na Kombe la Coppa Italia.
Baada ya kutwaa mataji hayo, Mourinho baadaye aliihama Inter Milan na Mei, 2010 akaenda kuifundisha Real Madrid ambako ukiwa msimu wake wa kwanza akiwa kocha aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Kombe la Copa Del Rey mbele ya wapinzani wao Barcelona kabla ya msimu uliofuata kutwaa ubingwa wa La Liga.
Hata hivyo msimu uliopita, Mourinho hakuweza kufanya vizuri, kwani hakuweza kutwaa ubingwa wowote na kisha akaambulia kuingia kwenye uhasama na wachezaji, Iker Casillas na Sergio Ramos.
Kutokana na matatizo hayo kwa kinywa chake akauita msimu uliopita kuwa ulikuwa msimu wa balaa kwake, akiwa na timu hiyo ya Real Madrid.
Tangu arejee tena Chelsea, Mourinho ameshanunua wachezaji wanne, Andre Schurrle, Mark Schwarzer na makinda wawili, Marco Van Ginkel na Cristian Cuevas.
Mbali na wachezaji hao wanne, Mourinho ameshatangaza mchezaji ambaye anamwinda kwa udi na uvumba ni Wayne Rooney licha ya kuwekewa ngumu.
Rekodi yake tangu arejee tena Chelsea:
Julai 17 vs Singha All-Stars alishinda 1-0
Jumapili ya Julai 21, vs Malaysia XI akashinda 4-1.
Alhamisi Julai 25, vs BNI Indonesia All-Stars akashinda 8-1.
Alhamisi Agosti 2 vs Inter Milan akashinda 2-0.
Matokeo haya yanatajwa na wachambuzi wa masuala ya soka kuwa huenda yakawa mwanzo mzuri kwa kocha huyo.
Roberto Martinez (Everton)
Roberto Martinez hatimaye ameitema klabu yake kipenzi Wigan, baada ya kuangaika nayo katika shida na raha na huku akiwa ameshakataa ofa nyingi kutoka klabu mbalimbali.
Kwa sasa kocha huyo ameamua kutimkia kwenye klabu hiyo ya Merseyside, baada ya David Moyes kuondoka Everton.
Hadi sasa, Martinez ameshajijengea jina katika kipindi chote ambacho ameinoa Wigan Athletic kati ya mwaka 2009 na 2013, ikiwa ni baada ya kuondoka kwenye klabu yake ya kwanza Swansea City.
Katika msimu wake wa kwanza Martinez wa 09/10, Wigan ilimaliza msimu ikiwa nafasi ya 16, nafasi ambayo ilikuwa ni pointi sita juu ya ukanda wa kushuka daraja, lakini mashabiki wa Wigan walifurahi kwa timu yao kubaki Ligi Kuu.
Msimu uliofuata wa 10/11, Wigan iliumaliza ikiwa nafasi ya 16 tena lakini safari hii ilikuwa juu kwa pointi tatu juu ya ukanda wa kushuka daraja.
Msimu uliofuata wa 11/12, Wigan iliumaliza ikiwa nafasi ya 15 na safari hii ikiwa juu ya ukanda huo kwa pointi 6 na katika msimu wake wa mwisho, Martinez alipata matokeo mchanganyiko ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Wigan kutwaa ubingwa wa Kombe la FA.
Tangu awasili Everton Mei 11 mwaka huu, Martinez ameshasajili wachezaji watatu akiwamo mmoja aliyemsajili kwa mkopo.
Wachezaji waliosajiliwa na kocha huyo hadi sasa ni pamoja na wawili aliowanunua akiwa Wigan ambao ni Antolin Alcaraz na Arouna Kone.
Katika usajili huo, Kone ameigharimu Everton pauni takribani milioni 6 wakati Alcaraz amesajiliwa kama mchezaji huru, baada ya kutosaini mkataba mpya na Wigan.
Wengine waliosajiliwa na kocha huyo ni mlinda mlango kinda wa Athletico Madrid, Joel Robles ambaye amesajiliwa na Everton kwa ada ya pauni milioni tatu na nusu.
Mbali na wachezaji hao, Martinez vilevile amemsajili kwa mkopo kinda mwenye umri wa miaka 19, Gerard Deulofeu kutoka kwa mabingwa wa Hispania, Barcelona.
Kinda huyo, Deulofeu ana uwezo wa kucheza nafasi yoyote mbele ikiwa ni pamoja na mshambuliaji wa pembeni.
Rekodi yake tangu awasili Everton:
Jumapili ya Julai 14 vs Austria Vienna alichapwa 2-1.
Jumatano 17 vs Accrington Stanley akashinda 4-1.
Jumamosi Julai 27 vs Blackburn Rovers akashinda 3-1.
Matokeo hayo nayo yanadaiwa kuwa siyo mabaya kwa kocha huyo na huenda akaisaidia zaidi.
David Moyes (Manchester United)
Ulimwengu wa soka ulishtuka mwishoni mwa msimu uliopita, wakati kocha, Sir Alex Ferguson alipotangaza kuwa anastaafu kufundisha soka.
Tamko hilo liliambatana na wiki kadhaa za tetesi kuhusu nani atakayemrithi kocha huyo kabla ya Mei 9 mwaka huu kutangazwa kuwa David Moyes ndiye atakayeinoa Manchester United na kwamba, angeanza kazi rasmi Julai mwaka huu.
Inaelezwa kuwa kabla ya taarifa hizo, mara zote ilikuwa ikionekana Moyes ndiye mtu anayefaa kukabidhiwa mikoba hiyo ya kuinoa Manchester United, wakati Ferguson atakapoamua kustaafu.
Hata hivyo inaelezwa kuna mtazamo tofauti kuhusu uwezo wake kwenye mikikimikiki ya michuano ya Ulaya, kutokana na kwamba hajawahi kushinda taji kubwa.
Moyes anasemekana amejijengea jina katika medani ya soka kwa kazi aliyoifanya na bajeti ndogo ya Everton kwa jinsi alivyoitumia.
Katika michuano ya Ligi Kuu, Moyes amejitahidi mno kwa kuiwezesha timu hiyo kumaliza ligi ikiwa nafasi kati ya sita hadi nane.
Moyes aliajiriwa na Everton Machi 2002 akitokea timu ya Preston North End, ikiwa ni baada ya kushindwa kuipaisha Preston katika Ligi Kuu.
Inaelezwa kuwa moja ya kitu kilichoivutia Toffees, ni jinsi alivyokuwa akiiendesha klabu hiyo kwa fedha kidogo na kitu hicho ndicho alichokifanya akiwa Everton.
Baada ya kutua Everton, Moyes aliinusuru kushuka daraja akiwa amecheza mechi chache za msimu wa 2001/02 kabla ya msimu wa 02/03 kutangazwa kuwa kocha wa mwaka kutokana na kiwango cha timu yake ilichokionesha baada ya kushuhudiwa ikicheza michuano ya Ulaya msimu wa 03/04.
Hata hivyo, hali mbaya aliiona wakati alipompoteza mshambuliaji wake, Wayne Rooney kwa Manchester United.
Tangu awasili Manchester United, Moyes ameshanunua mchezaji mmoja pekee kinda mwenye umri wa miaka 20, ambaye anacheza nafasi ya beki wa kushoto, Guillermo Varela.
Moyes amenunua kinda huyo kutoka timu ya CA Penarol Montevideo kwa ada ya pauni milioni 1.5.
Hata hivyo hadi sasa Moyes amekuwa akitangaza hadharani kumtamani nyota wa zamani wa Arsenal, Cesc Fabregas, ambaye Barcelona imeshatangaza wazi kuwa haitamuuza.
Mbali na mchezaji huyo, Moyes vilevile amekuwa akihusishwa na nyota anayesakwa na timu vigogo Ulaya, Gareth Bale.
Rekodi yake tangu awasili Man Utd:
Jumamosi Julai 13 vs Singha All Stars XI alichapwa 1-0.
Jumamosi ya Julai 20, vs A-League All Stars akashinda 5-1.
Jumanne Julai 23 vs Yokohama F Marinos alichapwa 3-2.
Ijumaa Julai 26 vs Cerezo Osaka, akatoka sare ya 2-2.
Jumatatu ya Julai 29 vs Kitchee akashinda 5-2.
Matokeo hayo nayo pia yanatabiriwa na wengi kuwa huenda timu hiyo msimu huu ikaenda na mwendo wa kusuasua.
Mark Hughes (Stoke City)
Mark Hughes msimu huu ndiye amechukua mikoba ya kocha wa muda mrefu wa timu hiyo, Tony Pulis.
Kibarua cha mwisho cha Hughes kilikuwa katika timu ya Queens Park Rangers ambako alisota bila kuambulia chochote.
Kabla ya kuondoka, Pulis amefanya kazi nzuri Stoke City kwa kuipandisha Ligi Kuu na kuhakikisha inakaa kwenye ligi hiyo, lakini baadaye mashabiki na viongozi wa timu wanaonekana kuchoka na mwenendo wa timu hiyo na hivyo wakaamua kuelekea njia nyingine kwa kumchukua Hughes.
Septemba 2004, Mark Hughes alitangazwa kuwa kocha mpya wa Blackburn Rovers na katika msimu wake wa kwanza wa 04/05 akaiwezesha kutinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la FA kabla ya kuiwezesha kutinga nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu uliofuata wa 05/06.
Baada ya kupata mafanikio hayo, kibarua cha Hughes kilianza kushika kasi na mwaka 2008 akapata changamoto kubwa ambayo hajawahi kuipata katika ukocha wake, ambapo ilishuhudiwa akikabidhiwa mikoba ya aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa ya England, Sven-Goran Erikson.
Akiwa na timu hiyo, mshambuliaji huyo wa zamani wa Man Utd aliwanunua wachezaji kama Vincent Kompany na Pablo Zabaleta ambao bado wapo kikosi cha kwanza cha Manchester City, ingawa usajili huo ulifanyika miezi miwili kabla ya timu hiyo kuingia mikononi mwa wawekezaji kutoka Falme za Kiarabu.
Kiongozi wa mageuzi hayo ni Sheikh Mansour ambaye hakuchukua muda kumruhusu Hughes kumsajili nyota wa Brazil, Robinho kwa kitita cha pauni milioni 32.5.
Desemba 2009, Hughes alitimuliwa baada ya kushinda mechi mbili za Ligi Kuu kati ya mechi 11 na nafasi yake ikachukuliwa na Roberto Mancini.
Tangu aondoke Manchester City hadi sasa, Hughes ameshazifundisha timu za Fulham ambapo aliiwezesha kumaliza msimu ikiwa nafasi ya nane ikiwa ni baada ya kuinoa kwa muda wa miezi 11 kabla ya kudai kuwa anataka kuongeza ujuzi zaidi.
Ndoto zake alizitimiza Januari 2012, alipoahamia kwenye timu ya Queens Park Rangers, akikabidhiwa mikoba ya Neil Warnock ambapo akiwa na timu hiyo, alipata mafanikio.
Hughes aliuanza msimu uliopita kwa aina yake, baada ya kutumia mamilioni katika usajili lakini akashindwa kupata ushindi kwenye mechi 12 alizoiongoza timu hiyo na hatimaye akafukuzwa.
Tangu ajiunge na Stoke City, Mark Hughes ameshasajili wachezaji wawili akiwa ametumia pauni milioni 3.2.
Katika usajili huo, mchezaji, Eric Pieters amesajiliwa bila malipo yoyote akitokea timu ya PSV Eindhoven na ana uwezo wa kusimama beki ya kushoto.
Mwingine aliyesajiliwa ni Marc Muniesa, ambaye ni mchezaji huru.
Rekodi yake tangu ajiunge Stoke City:
Jumatano Julai 24 vs Houston Dynamo alifungwa 2-0.
Jumamosi Julai 27 vs FC Dallas akashinda 2-0.
Manuel Pellegrini (Manchester City)
Manuel Pellegrini huyu ni kocha ambaye amekabidhiwa mikoba ya kocha wa zamani Manchester City, Roberto Mancini.
Hadi anajiunga na timu hiyo, kocha huyo alimaliza mkataba wake mwaka jana wa kuinoa timu ya Malaga FC na akaamua kutafuta timu nyingine badala ya kukaa Hispania.
Man City ni timu ya 13 kwa Pellegrini kuinoa na mafanikio yake makubwa aliyapata akiwa anaifundisha timu ya Villarreal.
Katika msimu wake wa kwanza akiwa na timu hiyo ya Villarreal mwaka 04/05, aliweza kumaliza ligi ya La Liga akiwa nafasi ya tatu na hivyo kufuzu michuano ya Klabu Bingwa Ulaya na katika msimu huo, Villarreal ikafanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la UEFA.
Msimu uliofuata wa 05/06, kikosi hicho cha Pellegrini kilifanikiwa kutinga nusu fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya na huku akiiwezesha timu hiyo kumaliza michuano ya Ligi Kuu ya La Liga, ikiwa nafasi ya saba.
Mbali na mafanikio hayo, ilishuhudiwa Villarreal ikiimaliza misimu miwili iliyofuata ikiwa nafasi ya tano, huku ikishika nafasi ya pili msimu wa 07/08.
Msimu uliofuata wa 08/09, ilishuhudiwa Villarreal ikitinga robo fainali za michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, ambapo ilipangwa kukutana na Arsenal.
Mwanzoni mwa Juni 2009, Pellegrini aliondoka Villarreal na kujiunga na vinara wa soka nchini Hispania, Real Madrid.
Hata hivyo katika kipindi alichoinoa Real Madrid, kilikuwa kifupi na hakuweza kupata mafanikio makubwa zaidi ya kuweka rekodi ya kufikisha pointi 98 na huku akiiwezesha kushika nafasi ya pili nyuma ya Barcelona.
Pellegrini alitimuliwa Real Madrid, Juni 2010 na Novemba mwaka huo, akajiunga na timu ya Malaga.
Katika msimu wa 11/12, Pellegrini aliiongoza FC Malaga kushika nafasi ya nne kwenye michuano ya La Liga akivunja rekodi kwa timu hiyo kwa kufikisha pointi 58.
Msimu uliofuata, Malaga ilitinga robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya kabla ya kuondolewa na timu ya Borussia Dortmund kwa mabao mawili yaliyopatikana muda wa nyongeza.
Kwa upande wake, tangu atue Manchester City, Pellegrini amesajili wachezaji wanne kwa thamani ya pauni milioni 87.
Wachezaji hao ni Jesus Navas aliyemtoa Sevilla kwa kitita cha pauni milioni 17, Fernandinho aliyemng’oa Shakhtar Donetsk kwa pauni milioni 35, Alvaro Negredo kutoka naye Sevilla kwa pauni milioni 22 na Stevan Jovetic aliyemnunua kutoka timu ya AC Fiorentina naye kwa kitita cha pauni milioni 22.
Pamoja na fedha hizo, Pellegrini ameshasema kuwa atatumia fedha nyingine zaidi na kwa sasa ndiye anayeongoza kwa kutumia fedha nyingi kuliko timu yoyote nchini England.
Rekodi yake tangu atue Man City:
Jumapili Julai 14 vs Supersport Utd alifungwa 2-0.
Alhamisi Julai 18 vs AmaZulu FC akafungwa 2-1.
Jumatano Julai 24 vs South China akashinda 1-0
Jumamosi Julai 27 vs Sunderland akashinda 1-0.
Alhamisi Agosti 2 vs Bayern Munich akafungwa 2-1.
No comments:
Post a Comment