KOCHA Mkuu wa zamani wa Simba, Trott Moloto,
ameililia Simba kwa kitendo chake cha kumtema Juma Kaseja katika msimu mpya wa
Ligi Kuu Tanzania Bara, unaotarajiwa kuanza baadaye mwezi huu.
Moloto, aliyeifundisha timu hiyo katika msimu
wa 2004/05 wa Ligi Kuu Bara, amepokea kwa masikitiko taarifa za Kaseja kutemwa
wakati akiwa ni kipa namba moja kwenye Kikosi cha Timu ya Taifa 'Taifa Stars'.
Kaseja alikuwa ni chaguo la kwanza katika
kikosi chake, wakati Moloto anaifundisha Simba, aliyeiacha baadaye kabla ya
kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu Bara, baada ya kutolewa na Enyimba ya Nigeria,
katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza jijini hapa, Moloto alishangaa
kusikia Kaseja kuachwa kwenye kikosi cha timu hiyo, huku akishindwa kufahamu
sababu zilizoufanya uongozi wa Simba kumtema.
Awali Moloto alitaka kujua maendeleo ya
Kaseja, baada ya kuachana naye kwa muda mrefu akiwa kocha wa timu hiyo, ambaye
baadaye mikoba yake aliichukua Mzambia,
Patrick Phiri.
"Kaseja hajambo?" Alimuuliza
mwandishi wa habari hizi, baada ya kubadilishana naye mawazo kwa muda walipokutana
katika Uwanja wa Klabu ya Mamelodi Sundowns anayoinoa kwa sasa.
Hata hivyo, alisema kuwa kama Simba walimtema
kwa sababu nyingine kama umri, huo ungekuwa ni uamuzi wa viongozi wake, kwa
kuwa ameweza kuichezea timu hiyo zaidi ya miaka 10, lakini kwa kiwango si
sahihi kwani bado ndiye namba moja katika Kikosi cha Stars.
Wakati huo huo, alisema ana mpango wa kuileta
nchini, timu ya Mamelodi ili iweze kucheza mechi tatu za kirafiki katika jiji
la Dar es Salaam na Mwanza.
Moloto alisema atawasiliana na uongozi wa
klabu hiyo ili waweze kupata ziara hiyo, ambayo inaweza kuwa na mafanikio kwao.
No comments:
Post a Comment