MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wamezidi kuwa tishio
baada ya jana kuifunga Timu ya 3pillars ya Nigeria bao 1-0.
Mchezo huo wa kirafiki wa kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara,
ulifanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Yanga, inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts, ilianza kuonesha
cheche zake tangu dakika ya kwanza ya mchezo huo kwa kuweza kucheza kandanda
safi na kuwapoteza wapinzani wao.
Hussein Javu, aliyesajiliwa kutoka Mtibwa msimu huu, ndiye
aliyezamisha jahazi la 3Pillars, kufuatia kufunga kwa shuti kali akimalizia
pasi ya Haruna Niyonzima, dakika ya 40.
Katika kipindi cha pili, 3Pillars ilionesha uhai wake kwa
kulishambulia lango la Yanga mara kwa mara, ila uhodari wa Ally Mustapha
ulionekana baada ya kuokoa michomo kadhaa ya hatari.
Yanga walionesha kandanda safi, lakini waliingia dosari kwenye dakika ya
85, baada ya mwamuzi Charles Mbaga kumtoa katika benchi Kocha wao, Ernie Brandts,
kufuatia kupinga maamuzi yake wakati mchezo huo ukiendelea, hata hivyo hadi
mechi hiyo inamalizika Yanga ilifanikiwa kushinda kwa bao 1-0.
Yanga iliwakilishwa na Ally Mustapha, Juma Abdul/Salum Telela, David Luhende, Rajab
Zahir, Nadir Haroub/Kelvin Yondani, Athuman Idd/Issa Ngao, Said Bahanunzi,
Haruna Niyonzima/Bakari Masoud, Jerson Tegete/Didie Kavumbagu, Husein
Javu/Abdallah Mguhi/Shabani Kondo na Mrisho Ngassa.
3Pillars: Tunde Adegbite, Daniel Agu/Azan Ibrahim, Olabode Adeoti, Adeshelo
Adeniran, Sulaiman Teslim/Kabir Rahma, Gabi Ekelojuote, Lanrewaju
Saluka/Riliwan Raheem, Daniel Ivang,
Chukwuma Chukwu/Felix Ikechukwu, Tijani Adewale na Paul Umen.
No comments:
Post a Comment