Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, June 30, 2013

NEYMAR JINAMIZI JIPYA KWA RONALDO LA LIGA

PALE Mbrazil Neymar alipotangaza uamuzi wake wa kutua Nou Camp msimu ujao, hamasa iliongezeka La Liga, kutokana na hamu ya kuwaona mastaa hao wawili wakizitesa beki za timu kadhaa ndani ya ligi hiyo.
Neymar ataungana na jirani yake Muargentina, Lionel Messi kuwapa shida mabeki kwa chenga za maudhi na kuwanyima usingizi makipa wa timu kadhaa za La Liga kwa mabao ya dharau watakayokuwa wakitupia kila mwisho wa wiki.

Wakati makipa na mabeki wakiwa kwenye hali mbaya kutoka kwa watu hawa wawili, pia Neymar ni jinamizi jipya kwa Cristiano Ronaldo ambaye amekuwa akijaribu kuchukua ufalme wa Messi kwa misimu kadhaa sasa.

Kikosi cha Real Madrid pamoja na Ronaldo wako kwenye mchakato wa kuibuka upya, baada ya kuondokewa na kocha wake, Jose Mourinho na kurudi kwenye mchakato wa kuchukua mataji baada ya kupita patupu msimu uliopita, lakini ujio wa Neymar pale Barcelona ni bonge la changamoto kwa Real.
Ronaldo amekuwa akipigana kufa au kupona dhidi ya Messi, ikiwa katika harakati zake za kuhakikisha anatajwa kama kchezaji bora zaidi kwenye La Liga na cha muhimu zaidi kuibeba timu yake itawale mbele ya wapinzani wao wa jadi Barca.

Ujio wa Mourinho ulileta imani kubwa miongoni mwa mashabiki wa Real Madrid na kitendo cha kuchukua ubingwa La Liga baada ya Barca kufanya hivyo mara tatu mfululizo, ilikuwa kama mwanzo wa kipindi kizuri zaidi.
Lakini msimu mbaya uliopita ambao timu ilimaliza bila taji lolote na kushuhudia The Special One akirudi zake London, na kuiacha Madrid ikiwa vibaya, wakati Barca wakiendelea kuimarisha timu ni jinamizi kubwa sana kwa Ronaldo.

Madrid wanaweza kutumia fedha na kutengeneza timu ya kutisha zaidi, lakini Ronaldo kwa sasa yuko kwenye wakati mgumu zaidi wa kulazimika kuibeba Real katika kipindi hiki cha mpito.
Atakuwa na jukumu la kuiongoza Los Blancos msimu ujao, jukumu hilo ni kubwa sana hasa kutokana na ukweli kwamba kuteleza au makosa yoyote yale yatajibiwa na Messi na Neymar kwa kuihakikishia Barcelona inapata pointi zote tatu kiulaini.

Kwa ubora alionao, Ronaldo atakaa kimya na kuacha kipaji chake kiongee uwanjani. Hasa kipindi hiki wakati msimu mpya ukizidi kukaribia, watu wanasubiri kwa hamu kuona El Classico ya kwanza.
Msimu huu El Classico zitakuwa ni mechi kati ya Barca wanaotisha dhidi ya Ronaldo anayeutaka ufalme wa La Liga.
Lakini mechi hizo zitatimia iwapo tu Ronaldo atabaki Santiago Bernabeu, katika kipindi hiki cha usajili.
Kuna dalili za Ronaldo kuondoka Real Madrid wakati huu wa kiangazi, uvumi wa yeye kutua Old Trafford umekuwa ukiongezeka wiki hadi wiki hasa baada ya David Moyes kuanza kazi rasmi leo.
Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa na taarifa kwamba, Man United wanaamini kuwa wanaweza kumrudisha Ronaldo Old Trafford, baada ya kuondoka mwaka 2009 na kutua Madrid kwa ada ya pauni milioni 80.

Taarifa ya gazeti la Kihispaniola la El Pais, Jumatano iliyopita liliandika kwamba, Ronaldo atakutana na viongozi wa Manchester United ambao watamalizana naye kwenye ishu nzima ya usajili wake.
Man United hawajazungumza lolote kuhusu taarifa hiyo, japokuwa kuna kila dalili kwamba uhamisho wa Ronaldo kurudi Old Trafford utakutana na upinzani mkali wa Paris St Germain, ambao nao wanamlilia mchezaji huyo bora wa zamani wa dunia.

Kocha mpya wa Real Madrid, Carlo Ancelotti anaweza kuamua kumbakiza Ronaldo katika kipindi hiki atakachokuwa akitengeneza timu iliyoachwa na Mourinho, hata hivyo Ancelotti hana kauli ya mwisho, Ronaldo mwenyewe ndiye anaweza kuamua kuondoka au kubaki.
Lakini mambo bado hayaeleweki, Moyes anayeanza kazi rasmi leo pale Man United, jukumu lake la kwanza litakuwa kumaliza sakata la usajili la Wayne Rooney ambaye kama Ronaldo amekuwa akihusishwa na kuondoka kwenye timu hiyo.

PSG, Bayern Munich, Chelsea na Arsenal zote zinahusishwa na mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa England, pia kuna taarifa kwamba, Moyes anataka kumbakiza mchezaji huyo ambaye alimtambulisha kwenye soka la kulipwa alipokuwa Everton.

Man United wamekuwa wakiweka hadharani nia yao ya kumbakiza Rooney na pia kutaka kumsajili Ronaldo, hapa swali lanabaki je, Ronaldo ataachiwa na Florentino Perez aondoke Madrid?
Ronaldo anatakiwa kuamua iwapo anakimbia jinamizi jipya La Liga, au anabaki na kupambana na jinamizi hili jipya (Neymar) ambalo litakuwa limeungana na lile la zamani (Messi) na kuhakikisha kwamba anaibuka kidedea.

Wakati La Liga kuna jinamizi wawili, uvumi wa kurudi Old Trafford bado umemng’ang’ania Ronaldo ambaye anahitaji kufanya maamuzi magumu kwenye kipindi hiki cha soka lake.

Kiwango alichokionyesha Neymar kwenye michuano ya Kombe la Mabara ni uthibitisha tosha kuwa Ronaldo anakazi kubwa sana kujipambanua kama mchezaji bora wa La Liga iwapo atabaki Santiago Bernabeu.

No comments:

Post a Comment