MANCHESTER, England
UHAMISHO wa Robin van Persie kutoka Arsenal kwenda
Manchester United, ndio uliotawala vichwa vya habari msimu uliopita.
Baada ya miaka nane akiwa London Kaskazini chini ya Arsene
Wenger, Mholanzi huyo aliamua kukataa kusaini mkataba mpya na hivyo kuuzwa Man
United kwa pauni milioni 24.5.
Alikuwa ameshinda tuzo ya ufungaji bora kwenye msimu
wake wa mwisho akiwa na The Gunners na kushinda tena kiatu cha dhahabu msimu
uliopita akiwa na Red Devils, baada ya kufunga mabao 26 kwenye mechi 38
alizocheza.
Lakini mwisho wa msimu uliopita, Sir Alex Ferguson alitangaza
kustaafu kufundisha soka baada ya miaka 26 akiwa na Manchester United. Fergie
alikuwa gundi iliyoiunganisha timu pamoja na bila shaka kocha bora wa muda wote
wa Uingereza.
Upande wa pili, msimu wa 2011-12 ulikuwa msimu
mwingine mbovu Emirates, huku Arsenal wakiishia kumaliza kwenye nafasi ya nne
na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya ambako wataanzia kwenye hatua ya mtoano,
walimaliza mbele ya Tottenham.
Van Persie alishinda taji lake la kwanza la Ligi
akiwa na miaka 29, hii ni baada ya miaka karibu 10 ndani ya Ligi Kuu England.
Siku ambayo timu hiyo ilikuwa ikipitisha ubingwa kwenye mitaa ya Jiji la
Manchester, hakuna ubishi kuwa Mholanzi huyo alikuwa hajutii maamuzi yake ya
kung’ang’ania kuondoka Arsenal.
Lakini miezi au miaka kadhaa anaweza kubadilika kwa
kile anachokifikiria kuhusu uamuzi wake wa kuondoka Emirates.
Arsenal imekuwa ikibanwa na mkataba wa ufadhili wa
Uwanja wa Emirates na Wenger (kwa hiyari yake) amekuwa akibana matumizi ya
klabu hiyo kila dirisha la usajili linapofunguliwa. Lakini hali sasa hivi
inabadilika.
Arsenal wanahusishwa na usajili wa mastaa kama
Gonzalo Higuain kutoka Real Madrid, Marouane Fellaini kutoka Everton na hata
staa mwenzake Van Persie pale Old Trafford, Wayne Rooney. Kumekuwa na
mabadiliko kwenye suala la matumizi na rasilimali, bata zote sasa hivi ziko Arsenal
na kama angebaki kwa msimu mmoja zaidi angeshiriki kwenye kula bata pande za
Emirates.
Huku Old Trafford alipo sasa hivi timu iko kwenye
kipindi cha mpito, kipindi cha kusahau utawala wa Ferguson na kuingia kwenye
zama za utawala wa David Moyes.
Kuna uwezekano mkubwa sasa kwa kiwango cha Manchester
City kupanda chini ya kocha mpya Manuel Pellegrini, ambaye tayari ametumia
kiasi cha pauni milioni 45 kwa kuwaleta Etihad, Fernandinho na Jesus Navas
halafu bado wanaweza kununua zaidi kwa sababu dirisha la usajili bado sana
kufungwa.
Jose Mourinho amerudi kuiongoza Chelsea, ni wazi
kuwa atatoa upinzani mkali kwa Man United msimu ujao. Yote kwa yote uwezekano
wa Man United kutetea ubingwa wao ni mdogo zaidi msimu ujao. Kumekuwa na
mabadiliko makubwa sana, siyo Old Trafford tu, bali kwenye timu zote
zilizomaliza ‘top 4’ msimu uliopita.
Arsene Wenger, mlezi wa Van Persie bado yuko Arsenal
amechukua cheo cha kocha aliyedumu kwa muda mrefu zaidi na timu kwa sasa, baada
ya Fergie kuondoka. Arsenal wanafedha ya kutumia na wanatarajiwa kutoa upinzani
wa kweli kwenye ubingwa msimu ujao.
Tukiwa wa kweli katika ishu hii, ni ngumu kuamini
iwapo Van Persie kuna siku atajutia kuondoka Arsenal, watu wanaamini kuwa
aliondoka kwa sababu alikuwa akiamini alikuwa ameshapata kila alichotaka akiwa
The Gunners na alikuwa akitafuta kubadilisha mazingira. Mwenyewe alisema
aliondoka Emirates kwa sababu alikuwa akitaka mataji na amepata moja tayari.
Hata hivyo, ni ngumu kuamini kama amepata kile
alichokitaka kutoka kwa Ferguson pale Old Trafford, watu wanahofu huenda akawa
anajuta kwa sababu Van Persie hakupata muda wa kutosha wa kujifunza kutoka kwa
kocha huyo aliyeachana na soka.
Kama mataji yakiendelea kutua Old Trafford chini ya
David Moyes hatojutia uamuzi wake, lakini iwapo Chelsea, Man City na hata Arsenal
wakifanikiwa kuitoa Man United kwenye ufalme wa England, RVP anaweza kujikuta
anajuta kutokana na kushindwa kupata mataji mengi zaidi kama alivyotarajia
wakati akitua Man United.
RVP anaweza kujiona kama mtu aliyepishana na gari la
mshahara, kwa kuja Man United kipindi ambacho Ferguson anakaribia kustaafu na
Arsenal wanaachana na ubahili, huku kukiwa na kila dalili za mafanikio kuhamia
Emirates.
No comments:
Post a Comment