BAADA
ya Juma Kaseja kutemwa katika usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara,
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo, Zakaria Hanspope, ameanika
sababu za kushindwa kumwongeza mkataba mpya, huku kiungo mshambuliaji wa zamani
wa timu hiyo aliyetua Coastal Union, Haruna Moshi ‘Boban’ akisema hayupo tayari
kucheza naye kikosi kimoja.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Hanspope alisema Kaseja alikuwa akiwapiga chenga
walipomhitaji kufanya naye mazungumzo baada ya mkataba wake kufikia ukingoni.
Hanspope
alisema walimwita ili kufikia mustakabali wake wa kuendelea kuichezea timu
hiyo, lakini hakuwa tayari na baadaye waliamua kuachana naye, wakiamini amepata
timu nyingine.
Hanspope
alisema Mei mwaka huu, walimwita kwa ajili ya mazungumzo lakini hakuitika wito
huo, kwa madai alikuwa katika majukumu ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, na
ilikuwa inakabiliwa na mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Taifa
Stars ilikuwa na mechi ngumu dhidi ya Morocco, ambapo ilifungwa mabao 2-1,
katika mchezo wa marudiano uliochezwa kwenye Uwanja wa Stade de Grand mjini
Marrakech na baadaye ilizamishwa na Ivory Coast mabao 4-2, kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Kaseja
ambaye mkataba wake ulimalizika rasmi jana, baada ya kuichezea timu hiyo tangu
mwaka 2002 akitokea Moro United, mara ya mwisho kukutana na mwenyekiti wa
usajili wa klabu hiyo, ilikuwa wakati Stars ikijiandaa kucheza na Morocco.
“Nilimwambia Kaseja sisi bado tuna nia ya
kuendelea na wewe msimamo wako ni upi? Alinijibu hawezi kusema lolote kwa kuwa
alikuwa katika majukumu ya timu ya taifa, akimaliza atanijibu,” alisema
Hanspope.
Alisema
aliendelea kuwa na msimamo wake usioeleweka baada ya kumaliza majukumu ya
kuitumikia timu ya taifa, ikiwa ni zaidi ya wiki mbili, hakuwahi kukaa katika
meza moja ya mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo licha ya kumtaka kufanya
hivyo.
Hanspope
alisema waliamini kwamba, amemaliza mkataba wake na wanamwita hataki labda
alikuwa na mipango yake mingine na waliamua kumwacha ili aendelee na utaratibu
wake.
Hata
hivyo, alisema uwezo wa Kaseja umeshuka mno tofauti na ilivyokuwa katika miaka
ya nyuma, hali inayompa wakati mgumu kwa mashabiki wa timu hiyo.
Msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara,
mashabiki walitaka kumpiga baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar mabao 2-0, katika
mchezo wa kwanza, uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Wakati
huo huo, Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’
aliyesajiliwa na Coastal Union katika majira haya ya joto kwa mkataba wa msimu
mmoja, ameeleza kuwa hataki kumwona Kaseja akijiunga na timu hiyo.
Habari
zilizopatikana jana kutoka kwa marafiki wake wa karibu LENZI YA MICHEZO kuzinasa,
zilidai kwamba Boban amechukizwa na mambo aliyofanyiwa na Kaseja wakati akiwa
nahodha wa Simba wa muda mrefu na ameweka wazi kuwa endapo atajiunga na
Coastal, yeye ataacha kuichezea miamba hiyo ya Tanga.
Boban
ni miongoni mwa wachezaji wa Simba waliotemwa na klabu hiyo, wengine wakiwa ni
Felix Sunzu na Amir Maftah, baada ya mikataba yao kumalizika huku Juma Nyosso,
Abdallah Juma na Paul Ngalema wakishindwa kuomba kuvunja mikataba yao miamba
hiyo ya Msimbazi.
No comments:
Post a Comment