BALE HORIZONTE, Brazil
BRAZIL waliipiga Uruguay 2-1 kwenye nusu fainali ya kwanza ya
michuano ya Kombe la Mabara mwaka 2013 na kujihakikishia kuingia fainali
mashindano hayo itakayopigwa kwenye dimba la Maracana.
Fred na Paulinho walifunga mabao ya Brazil wakati lile la
Uruguay liliwekwa kimiani na Edinson Cavani.
Makala haya yanaiangalia mechi hiyo kiufundi zaidi na kipi
kiliwapa vijana wa Luiz Felipe Scolari ushindi.
Mfumo
Uruguay walitumia mfumo wa 4-3-1-2, huku Diego Forlan akipewa
majukumu ya kucheza kama namba 10, wakati Brazil walitumia mfumo wa 4-2-3-1
ambao umewapa ushindi kwenye mechi zao zote za msimu huu.
Hakukuwa na mabadiliko yoyote yaliyofanyika kwenye kikosi cha Scolari,
lakini Oscar Tabarez alifanya mabadiliko tena.
Kukabia
juu kwa Uruguay
Uruguay (La Celeste) walianza kwa kukabia juu kwenye nusu ya
Brazil na kuwalazimisha Brazil kupiga pasi kurudi nyuma na mabeki wake kufanya
makosa.
Paulinho na Luiz Gustavo walihaha kutengeneza nafasi, huku
wakikabwa kwa nguvu na kina Edinson Cavani na Luis Suarez, hiki kilizima
mashambulizi ya Selecao.
Viungo watatu wa Uruguay, Alvario Gonzalez, Arevalo Rios na
Cristian Rodriguez – walikabia juu na kuwapa Brazil nafasi ndogo ya kucheza.
Kikosi cha Brazil kimekuwa na matatizo kwenye kutengeneza
nafasi, lakini kutokana na mfumo wa Tabarez mambo yalizidi kuwa magumu kwa
Wabrazil.
Brazil
kukosa mbinu mbadala
Kitendo cha Brazil kukabiwa juu kilimaanisha timu kushindwa
kucheza kupitia katikati ya uwanja, hivyo mara kadhaa walijikuta wakipiga mpira
pembeni na kuchezea huko.
Hii iliwasababisha wachezaji wa pembeni kuchangamka kwa sababu
viungo watatu wa Uruguay walifanya kazi nzuri sana kumtuliza Oscar ambaye
alikuwa akicheza kama Namba 10 na kumnyima nafasi ya kukimbia na mipira
katikati ya uwanja.
Marcelo alionyesha kiwango cha hali ya juu, lakini Neymar mara
zote alikuwa amekabwa na mtu zaidi ya mmoja. Hulk, kama kawaida yake hakuwa na
jipya, hakuna alichokifanya upande wa kuliwa wa Selecao na kumpa kazi kubwa
sana Neymar upande wa kushoto.
Neymar mara kadhaa alishuka chini sana kuchukua mipira, lakini
alipopata mipira alikuwa na wakati mgumu sana kumtafuta mtu wa kumpa mipira
zaidi ya beki wake wa kushoto.
Mipira mirefu
Kitendo cha Uruguay kukabia juu, kiliwalazimisha David Luiz na
wenzake kuanza kupiga mipira mirefu kutokea nyuma, hivyo beki ya Celeste
ililazimika kuwa vizuri kwenye mipira ya juu.
Bahati nzuri wote Diego Godin na Diego Lugano walikuwa vizuri
sana kwenye beki wa kati hivyo kumzima kabisa Fred ambaye alijikuta akishindwa
kucheza kabisa.
Ilihitajia kipaji binafsi kutoka kwa Neymar Brazil kupata bao
la kwanza; kwanza alinza kwa kujitengenezea nafasi na kukimbia huku
akihakikisha haotei na kupokea pasi ndefu ya Paulinho kwa kifua kisha kupiga
mpira ambao uligonga kipa wa Uruguay, Fernando Muslera usoni, lakini haikwenda
mbali na kumkuta Fred ambaye hakufanya ajizi alifunga kirahisi.
Bao hilo lilithibitisha kwamba mfumo wa Uruguay,
uliwalazimisha Brazil kucheza mipira mirefu ambayo pia ilisaidiwa na kipaji
binafsi cha mtu mmoja bao hilo kupatikana.
Kipindi
cha pili
Kipindi cha pili Brazil walianza kuchanganya licha ya Uruguay
kusawazisha bao hilo kupitia kwa Edinson Cavani, Brazil walionekana bora na
walistahili ushindi.
Kutoka kwa Hulk kuliifanya Selecao kubadilika na kuwa bora
zaidi, hii inatokana na Bernard aliyeingia kucheza upande wa kulia kuwa na kasi
na vitu vya ziada.
Kuingia kwa Bernard kuliisaidia Brazil kumiliki mpira zaidi
kwa sababu Hulk alikuwa akipoteza sana mipira, pia kinda huyo alikuwa muhimu
sana kwenye mashabulizi ya kushtukiza.
Hitimisho
Brazil bado hawajatulia na wanapoteza sana mipira. Kiungo cha
kati kwenye timu hiyo bado utata, japokuwa kilifanya vizuri zaidi baada ya Paulinho
kusogezwa mbele kucheza kama namba 10 kwenye dakika za mwisho za mechi.
Hawana kiungo mwenye uwezo wa kuchezesha timu na kumiliki
mpira na hilo linaweza kuwaangusha kwenye mechi ya fainali.
Hivyo ndio ilivyo kwa Uruguay wanaviungo wazuri, lakini bado
hawajafikia kuwa timu bora. Mashambulizi yao ya kushtukiza ni makali sana
lakini hawawezi kufika mbali kama kiungo chao kinamtegemea Arevalo Rios.
Neymar ndiye aliyetengeneza mabao yote mawili ya Brazil, la
kwanza baada ya kuonyesha kipaji cha hali ya juu, la pili kwa njia ya kona,
hivyo kipaji cha Neymar ndicho kilichoibeba Brazil.
No comments:
Post a Comment