MADRID, Hispania
HATIMAYE, Jumanne wiki hii Carlo Ancelotti alitangazwa rasmi
kuwa kocha wa Real Madrid na anatarajiwa kuanza kuijenga timu hiyo kwa ajili ya
msimu wa 2013-14.
Muitaliano huyo ambaye amewahi kuzifundisha klabu za Paris
Saint-Germain, Chelsea na AC Milan anasifika kwa kuwa na tabia ya kufanya
mapinduzi kwenye timu yoyote anayoifundisha na anatarajiwa kufanya hivyo pale Santiago
Bernabeu.
Ancelotti amekuwa akitumia mifumo mbali mbali kwenye maisha
yake ya ukocha, alipokuwa Paris Saint-Germain na Chelsea alitumia 4-4-2, AC
Milan 4-3-2-1.
Tofauti na makocha wengi Ancelotti amekuwa na tabia ya
kuendana na mazingira ya klabu aliyopo pamoja na wachezaji alionao na kuna kila
dalili kwamba Muitalioano huyo hatabadilisha mfumo wa sasa wa Madrid wa
4-2-3-1.
Siku zijazo anaweza kuja na mfumo mpya, lakini kwa sasa
anatarajiwa kutumia mfumo ambao ulikuwa ukitumiwa na Jose Mourinho.
Ancelotti atagundua kwamba hata kama akija na staili, mifumo
na ufundi mpya kwenye timu hiyo, anatakiwa kuendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1 katika
siku za mwanzo akiwa Bernabeu.
Kuondoka kwa Gonzalo Higuain kutamaanisha kwa Muitaliano huyo
amebakiza mshambuliaji mmoja tu mkali Karim Benzema, Japokuwa Alvaro Morata amepandishwa
kutoka timu ya vijana ya Real Madrid, Castilla, huku klabu hiyo ikiendelea
kumuwania Edinson Cavani na Luis Suarez.
Wote hawa rais Florentino Perez anawaona kama bei yao ni kubwa
sana na hilo linaweza kumaanisha kwamba hakuna mshambuliaji mpya atakayesajili
kipindi hiki cha kiangazi, huku klabu ikimtolea macho zaidi Gareth Bale.
Winga huyo wa Tottenham Hotspur atasajili wa bei kubwa, lakini
Perez yuko radhi kulipa dau lolote kwa ajili yake, kwa sababu staa huyo anaweza
kuongeza mapato kutokana na mauzo ya jezi na haki za picha.
Perez wiki hii alinukuliwa akisema; “Wachezaji wazuri
wanajilipia wenyewe. (Luis) Figo, (Zinedine) Zidane, Ronaldo na (David) Beckham
waliongeza mapato yetu. Kama ukiwekeza kwa mchezaji mzuri utaingiza fedha
nyingi zaidi.”
Bale, hata akiuzwa kwa euro milioni 90, yuko kwenye kundi
hilo. Cavani, kwa pauni milioni 63 hayako kwenye kundi hilo, hii inamaanisha Ancelotti
anaweza kumkosa mshambuliaji aliyewahi kutaka kumsajili alipokuwa Chelsea.
Isco tayari katua, staa huyo wa Malaga anakuja kujaza sehemu
ya kuingo mchezeshaji kutokana na Mesut Ozil na Kaka, ambaye alifanikiwa sana
chini ya Ancelotti, AC Milan, wakionekana kukosa nafasi.
Isco anaweza kuanza kama kiungo mshambuliaji au upande wa
kulia kwenye timu ambayo Bale atakuwa ndani pia. Na kama Bale asipotua Bernabeu
wakati wa kiangazi wote Isco na Ozil wataanza kwenye kikosi cha Ancelotti
Wakati huo huo Benzema atakuwa chaguo la kwanza kwenye timu
hiyo kama timu isiposajili mshambuliaji, japokuwa Isco, Bale na Cristiano
Ronaldo wanaweza kucheza kama washambuliaji wa kati.
Maeneo mengine Iker Casillas atarudishwa kwenye goli la timu
hiyo baada ya kusugua bechi chini ya Mourinho msimu wa 2012-13.
Ancelotti pia anapenda kutumia viungo wawili wa uchezeshaji
kwenye kiungo cha chini, Xabi Alonso atacheza sambamba na Luka Modric, huku Sami
Khedira akisugua benchi.
Madrid pia wanatafuta mtu wa kuziba nafasi ya Alonso, siku za
usoni, lakini wachezaji wanaowataka kina Ilkay Gundogan na Marco Verratti kwa
sasa hawapatikani kwenye soko la usajili.
Dani Carvajal atachuana na Alvaro Arbeloa kucheza nafasi ya
beki wa kulia baada ya kurudi Madrid akitokea Bundesliga.
Kikosi
kamili kitakuwa hivi; Mfumo 4-2-3-1; Iker Casillas; Alvaro Arbeloa, Sergio
Ramos, Raphael Varane, Marcelo; Luka Modric, Xabi Alonso; Gareth Bale, Isco, Cristiano
Ronaldo; Karim Benzema
No comments:
Post a Comment