Manchester,
England
KITENDO cha Carlos Tevez kuthibitishwa
kutua Juventus kwa pauni milioni 10, kimefungua njia kwa Gonzalo Higuain
kukaribia kumalizana na Arsenal.
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid
amekubali kulipwa pauni 125,000 na 'the Gunners', na hivyo kuwa mchezaji
atakayelipwa zaidi Arsenal, hivyo kuwapiku Jack Wilshere, Theo Walcott na Lukas
Podolski.
Kwa sasa uhamisho wake unatarajiwa
kuthibitishwa rasmi na Kocha mpya wa Real, Carlo Ancelotti.
Higuain, 25, kwa muda mrefu amekuwa
akiwindwa na Juventus. Hata hivyo, kaka wa mchezaji huyo, Nicolas amethibitisha
kuwa baada ya Tevez kutua Juventus sasa Higuain yupo karibu kujiunga na wakali
hao wa Emirates.
Alisema: “Kama Tevez atajiunga na Juve,
Higuain anakaribia Arsenal? Nadhani hivyo.
“Juventus ni klabu kubwa, lakini
Gonzalo atakuwa ni ghali zaidi kwao. Siwezi kukana kwamba Gonzalo kwa sasa
anakaribia Arsenal.”
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger pia
anamtolea macho Kiungo wa Everton, Marouane Fellaini.
@@@@@@@
Paulinho aipeleka Brazil fainali
Mabara
Rio
de Janeiro, Brazil
BAO la usiku la kichwa lililozamishwa
kimyani na Paulinho, limeipeleka Brazil
kwenye mechi ya fainali ya kuwania Kombe la Mabara baada ya kuitungua Uruguay 2-1.
Fred ndiye aliyeifungulia Brazil milango baada ya kuifungia bao la kwanza
ikiwa ni dakika tatu baada ya Diego Forlan kukosa penalti kwa Uruguay.
Mwamuzi kutoka Chile, Enrique Osses alitoa penalti kwa Uruguay baada ya Beki wa Kati wa Brazil, David
Luiz kumchezea madhambi Diego Lugano katika eneo la hatari.
Mapema katika kipindi cha pili, Edinson
Cavani alifanikiwa kuisawazishia Uruguay
ikiwa ni baada ya kuihadaa ngome ya ulinzi ya Brazil, lakini katika dakika ya 86,
Paulinho alifunga bao la ushindi kwa wenyeji hao.
Uruguay
itabidi kujilaumu yenyewe baada ya Brazil kuonyesha kiwango duni
katika kipindi cha kwanza lakini ikashindwa kutumia nafasi hiyo.
Kwa matokeo hayo, Brazil sasa
katika mchezo wa fainali Jumapili, itakutana na Hispania ama Italia,
kutegemeana na matoke ya mechi ya nusu fainali ya pili iliyozikutanisha timu
hizo jana usiku.
Brazil
iliwachezesha: Julio Cesar, Dani Alves, Thiago Silva, Luiz, Marcelo, Oscar
(Hernanes 72), Gustavo, Paulinho, Fred, Hulk (Bernard 64) na Neymar (Dante 90).
Uruguay: Muslera,
Lugano, Godin, Caceres,
Maxi Pereira, Rodriguez, Arevalo Rios, Gonzalez (Gargano 83), Forlan, Suarez na
Cavani.
@@@@@@@
Real yamtoa Di Maria 'kafara' kwa Bale
Madrid,
Hispania
KLABU ya Real Madrid imetoa ofa ya
fedha na mchezaji mmoja kwa Spurs ili tu kuhakikisha Kocha wao mpya, Carlo
Ancelotti msimu uajao anafanya kazi sambamba na Gareth Bale.
Winga wa Argentina,
Angel Di Maria ni miongoni mwa wachezaji ambao miamba hiyo ya Hispania
inatarajia kuwatoa 'kafara' kwa klabu hiyo ya White Hart Lane ili kumnasa mchezaji huyo
bora wa mwaka wa Ligi Kuu England.
Hata hivyo, bado Tottenham imeendelea
kuikataa ofa ya kumtoa Bale, 23.
Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa
mrithi wa Jose Mourinho aliyetua Chelsea,
Ancelotti alisema: “Timu hii ni nzuri, lakini itahitaji mabadiliko kidogo, na
si makubwa.”
Rais wa Real, Florentino Perez
anawawinda Bale, Mshambuliaji wa Liverpool, Luis Suarez na nyota wa Napoli, Edinson Cavani.
Wakati huu ambao Bale hajaonyesha nia
ya kutua Bernabeu, Tottenham imemwekea mezani dili la mkataba mpya ambapo
atakuwa akilipwa pauni 170,000 kwa wiki.
@@@@@@@
Ronaldo huyooo United
Madrid,
Hispania
Cristiano
Ronaldo atakuwa njiani kutua Manchester
United baada ya taarifa kueleza kuwa anatarajiwa kukutana na uongozi wa wakali
hao wa Old Trafford siku tatu zijazo.
Nyota huyo wa Real Madrid
amekuwa akihusishwa na kurudi England
baada kumaliza msimu akiwa si mwenye furaha hapo Santiago Bernabeu, lakini ujio
wa Kocha mpya, Carlo Ancelotti unaweza kuhitimisha zoezi hilo kwa kufanikiwa kumbakisha Hispania.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa United,
amepewa ofa ya pauni milioni 12 kwa mwaka ili akubali kubaki Bernabeu, lakini
Ronaldo anahitaji pauni milioni tano zaidi, na amekuwa si mwenye furaha baada
ya kauli ya Rais wa Real, Florentino Perez aliyoitoa akidai kwamba ‘kila kitu
kina kikomo’.
Gazeti la Hispania "El Pais",
limeripoti kuwa nahodha huyo wa Ureno atakutana na uongozi wa United kabla ya
kwenda kujiandaa na msimu mpya na Madrid.
Lakini hata hivyo, Jumatano wakati
Ancelotti akitambulishwa kwa waandishi wa habari kama
kocha mpya wa Real, alisema: 'Cristiano ni mchezaji mkubwa na ninafura kufanya
naye kazi.
"Niliwanoa Zidane, Ronaldo na
Ronaldinho, na ninafurafa kufanya naye kazi."
Alipoulizwa kuhusu Radamel Falcao,
ambaye alikuwa akiwinda na Madrid kabla ya
kutua Monaco,
Ancelotti aliongeza: "Ni mchezaji mzuri, lakini kuna Ronaldo, Higuain na
Benzema."
No comments:
Post a Comment