TIMU ya Abajalo ya Dar es Salaam leo imetolewa kwenye
mashindano ya bingwa wa mikoa baada ya kufungwa bao 1-0 na Kariakoo Lindi.
Mchezo huo ambao ulikuwa na ushindani ulichezwa kwenye
Uwanja wa Ilulu mjini Lindi, na wenyeji kufanikiwa kutumia Uwanja wao vema na
kufanikiwa kusonga hatua ya tatu.
Akizungumza kwa njia ya simu toka Lindi, Mwenyekiti wa Chama
cha Soka mkoa wa Lindi (LIREFA), Francis Ndulane alisema kuwa bao hilo
lilifungwa na mshambuliaji Salum Abilah kipindi cha kwanza baada ya kuwazidi
mbio mabeki wa Abajalo.
“Mchezo umemalizika na Kariakoo Lindi wamefanikiwa kusonga
mbele baada ya kuifunga Abajalo bao 1-0 lililofungwa na Salum Abilah kwa shuti
kali lililomshinda golikipa wa Abajalo baada ya kuwazidi mbio mabeki”, alisema
Ndulane.
Kariakoo inayofundishwa na Nyamwase Rashid kwenye mchezo wa
ugenini Dar es Salaam walilazisha sare ya mabao 2-2 kwani walitoka nyuma wakiwa
wamefungwa mabao 2-0 na kufanikiwa kusawazisha zote na kuahamsha matumaini ya
kusonga mbele.
Abajalo inakuwa timu ya pili toka Dar es Salaam kuaga
mashindano haya baada ya Friends Rangers kutolewa kwenye hatua ya kwanza.
No comments:
Post a Comment