TIMU kongwe za soka nchini ambao ni mahasimu wa jadi, Simba
na Yanga zilizoweka kambi ya kujiandaa na pambano lao la kufunga msimu Ligi Kuu
Bara visiwani Zanzibar, zimefanya bei ya vifaa ya madawa ya asili kuwa dili
ghafla ikiwemo mayai viza kutokana na kudaiwa kuongezeka kwa matumizi yake.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Lenzi ya Michezo na baadaye kufumania
nyendo kutoka kwa baadhi ya wadau waliokuwa wakishughulikia mchakato huo,
ulinasa orodha ya vifaa, timu moja ilivyotakiwa kununua na kisha kuvipeleka kwa
'mtaalamu' wao ambapo ubani, tende, sukari guru, kuku na mayai viza vikisakwa kwa udi na uvumba.
Kwenye kambi mojawapo ya timu hiyo ambayo
inatarajiwa kukutana na mpinzani wake kesho katika Uwanja wa Taifa, baada ya
raundi ya kwanza kutoka sare, imani kubwa imetanda kuwa vifaa hivyo
vikipatikana na kisha kufanyiwa mambo kwa 'mtaalamu' wao anaweza kubadili
matokeo.
Lenzi ya Michezo lilifanikiwa kunasa mawasiliano yaliyokuwa yakifanywa
baina ya viongozi wa timu moja yenye rekodi nzuri ya kumfunga mtani wake,
akifanya mawasiliano na kiongozi mmoja aliyekuwa akiwasiliana na waganga kutoka
Dar es Salaam na Pangani, Tanga.
Kwa mujibu wa mawasiliano hayo, tayari wamebaini kuwa timu
yao ilishazidiwa ujanja mapema na itakuwa ni vigumu kunusurika na kipigo, hivyo
jitihada za ziada zilihitajika ili 'mtaalamu' aweze kubadili matokeo.
Moja ya ujumbe mfupi (sms) ulionaswa kutoka kwa mganga
kwenda kwa kiongozi, ulisema ili kubadili matokeo lazima zitengenezwe kadi
nyekundu mbili kwa wapinzani wao na pia penalti moja na kwamba endapo akibadili
matokeo hayo, kuna uwezekano wa kuzuka vurugu kubwa.
“Kutakuwa na vurugu kubwa, kama nikifanya hivi, lakini mimi
nashauri mtimize yale niliyoyaagiza ili tupindue kwa njia nyingine na kazi
yangu ni uhakika kama mko tayari nianze
kazi mapema,” ulisema ujumbe huo mfupi.
Ujumbe mwingine kutoka kwa mganga kwenda kwa kiongozi wa
timu moja, ulikuwa ukiainisha vitu vinavyohitajika ili kuhakikisha kuwa timu
inapata matokeo mazuri katika mchezo huo.
“Nataka nipate vitu hivi ili nivipeleke kwa Bimtuka. Vitu vyenyewe
ni Halua kilo 3, tende kilo 3, Chungu 1, sahani nyeupe 1, visu 7, kibatari
kimoja, mafuta ya taa lita 5, sindano za kushonea kwa mkono 11, nyembe 11
pamoja na vitambaa na majina yote ya wachezaji wa wapinzani wenu,” ulisomeka
ujumbe huo.
Baada ya hapo kiongozi huyo alijibu kuwa kila kitu kiko sawa
na atakamilishiwa kila anachohitaji mganga huyo na kumtaka afanye kazi ya
uhakika kama ile ambayo aliwahi kuifanya na kuleta matokeo mazuri.
Ujumbe mwingine ulionaswa ukiwa ni kutoka kwa viongozi na
mmoja wa wanachama wa klabu mkoani Tanga, ulisema, “mkuu hadi sasa tumeona kuwa
tuna ushindi wa 3-0, hii ni kwa mujibu wa duru kutoka Pangani, lakini kwa kuwa
siku bado, chochote kinaweza kutokea, maana wenzetu pia wanahangaika sana, cha
msingi tuwe makini na nyie mlio na timu muwe makini zaidi na watu."
Kutokana na hali ya ushirikina kutawala katika kambi za timu
hizo kongwe, kwa sasa inadaiwa wachezaji wamepigwa marufuku kupeana mikono na
watu hovyo na wageni wamekatazwa kabisa kufika kwenye kambi zao.
Si jambo la ajabu kwa timu za Simba na Yanga kuonekana
zikiendekeza vitendo vya kishirikina kabla na siku ya mechi, lakini hata hivyo, Lenzi ya Michezo tunaamini maandalizi mema na kujituma ndiyo njia pekee ya kuweza kuibuka
na ushindi na ushirikina hauna nafasi katika soka.
No comments:
Post a Comment