Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, May 19, 2013

HAWA WALIPELEKA VILIO SIMBA NA YANGA


KATIKA safu hii ya mechi ninayoikumbuka, itakuwa tofauti kidogo na kawaida yetu, lakini sababu kubwa ni kutokana na mchezo wa jana wa watani ambao ni Simba na Yanga, zilikutana kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika makala ya leo tutaelezea baadhi ya wachezaji ambao walishapeleka vilio kwa pande zote mbili miaka ya nyuma na kwa nyakati tofauti.
 
Kibadeni
1. Abdallah ‘King’ Kibadeni

Huyu ni mmoja wa wachezaji wa Simba ambaye ameipatia mafanikio makubwa klabu hiyo katika miaka ya 1970. Kibadeni alikuwa ni mchezaji machachari, mwenye chenga za maudhi ambaye alikuwa tegemeo katika klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, maarufu kama ‘wekundu wa Msimbazi’.

Kibadeni anakumbuka mechi iliyokutanisha timu yake ya Simba dhidi ya Yanga ya mwaka 1977 ambapo yeye aliweza kufunga mabao matatu kati ya sita ambayo yalipatikana siku hiyo.

Katika mechi hiyo ambayo ilikuwa ni ya kuwania Ubingwa wa Tanzania Bara, Kibadeni alifunga bao la kwanza katika dakika ya 25. Bao la pili beki wa Yanga, Selemani Said Sanga alijifunga baada ya kiki kali iliyombabatiza iliyopigwa na Willy Mwaijibe.

Kibadeni alirudia tena kufunga bao la pili ambalo lilikuwa ni la tatu kwa timu yake dakika moja kabla ya mapumziko. Jumanne Masmenti alifunga bao la nne katika dakika ya 60, baada ya kumpiga chenga kipa wa Yanga,  Bernard Madale.

Jumanne Masmenti alifunga tena bao la tano katika dakika ya 74. Dakika chache kabla ya mchezo kumalizika Kibadeni alifunga tena bao la tatu ambalo lilikuwa ni la sita kwa timu yake ya Simba. Hivyo mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika Simba walitoka uwanjani wakiwa washindi kwa kuwafunga Yanga mabao 6-0.

Kikosi cha Simba siku hiyo kilikuwa ni Omari Mahadhi (marehemu), Daudi Salum ‘Bruce Lee’, Mohamed Kajole (marehemu), Aloo Mwitu, Mohamed Bakari ‘Tall’, Athumani Juma (marehemu), Willy Mwaijibe (marehemu), Aluu Ali, Jumanne Masmenti (marehemu), Abdallah ‘King’ Kibadeni na Abbas Dilunga.

Kikosi cha Yanga kilikuwa Benard Madale (marehemu), Boniface Makomoye, Selemani Said Sanga (marehemu), Charles Mwanga, Selemani Jongo, Sammy Kampambe, Shabani Katwila ‘Suzuki’, Ezekiel Greyson ‘Juju Man’ (marehemu), Mwinda Ramadhani, Yanga Fadhil Bwanga na Ayoub Shabani. 

2. Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’.
Hivi sasa ukiwauliza wapenzi na mashabiki wa Yanga kuwa ni wakati gani timu yao ilikuwa na washambuliaji ambao ni mara chache walitoka uwanjani bila ya kufunga bao, ni dhahiri kuwa watakuambia huo ulikuwa ni wakati walipokuwa na mshambuliaji hatari Makumbi Juma maarufu kama Homa ya Jiji,  kama wapenzi hao walivyozoea kumwita.

Makumbi alikuwa ni mshambuliaji hatari mno, kwani alikuwa na nguvu na mashuti makali na aliwafanya mabeki aliokuwa anakabiliana nao kupata wakati mgumu kumkabili. Kutokana na mikikimikiki yake na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kupachika mabao wapenzi wa klabu hiyo ya Yanga walimbatiza jina la ‘Homa ya Jiji’.

Makumbi anaikumbuka mechi iliyokutanisha timu yake hiyo ya Yanga dhidi ya Simba iliyochezwa siku ya Jumamosi tarehe 20, Oktoba, 1990, mchezo wa ligi daraja la kwanza Tanzania Bara, uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam (sasa uwanja wa Uhuru).

Matokeo ya mechi hiyo ambayo ilikuwa ni ya mzunguko wa pili ni kwamba Yanga waliwafunga watani wao hao wa jadi, Simba mabao 3-1. Bao la kwanza katika mechi hiyo lilifungwa na Makumbi Juma, la pili lilifungwa na Thomas Kipese na la tatu lilifungwa na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’. Bao pekee la Simba lilifungwa na Edward Chumila.

Kikosi cha Yanga siku hiyo kilikuwa Sahau Kambi (marehemu), Fred Felix ‘Majeshi’, Kenneth Mkapa, Said Zimbwe (marehemu), Godwin Aswile, Rajab Rashid, Justine Mtekere (marehemu), Athumani China, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’, Sanifu Lazaro na Thomas Kipese ‘Uncle Thom’.

Kikosi cha Simba kilikuwa Patrick Mwangata\Mackenzi Ramadhani (marehemu), Raphael Paul ‘RP’ (marehemu), Twaha Hamidu ‘Noriega’, Frank Kasanga ‘Bwalya’, Adolph Kondo, Iddi Selemani ‘Mayor’, Method Mogela ‘Fundi’ (marehemu), Hamisi Gaga ‘Gagarino’ (marehemu), Ally Machela (marehemu), Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’ na Edward Chumila (marehemu).

3. Mohamed Mwameja
Mwameja alikuwa golikipa aliyeipatia mafanikio makubwa klabu ya Simba. Mbali na uhodari wake wa kudaka awapo uwanjani, pia alikuwa ni mahiri sana katika udakaji wa mipira ya penalti.

Kipa huyu mahiri anakumbuka mechi iliyokutanisha timu yake ya Simba dhidi ya Yanga mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru), uliochezwa siku ya Jumamosi, Julai2 mwaka 1994.

Matokeo ya mchezo huo ambao ulikuwa ni wa ligi daraja la kwanza Tanzania Bara (sasa ligi kuu), Simba waliwafunga Yanga mabao 4-1. Simba walipata bao la kwanza katika dakika ya 16,  kwa mkwaju wa adhabu ndogo uliopigwa na George Masatu baada ya Nico Bambaga kumfanyia madhambi Edward Chumila.

Dakika ya 20, Yanga ilipata bao lililofungwa na beki wake raia wa Burundi, Costantino Kimanda lililotokana na mpira wa adhabu ndogo.

Simba walipata bao la pili lililofungwa na Athumani China kwa mpira wa kona iliyochongwa na George Masatu. Katika dakika ya 76 Simba walifanikiwa kupata bao la tatu lililofungwa na Madaraka Selemani. Katika dakika za mwisho mwisho Simba walifanikiwa kupata bao la nne baada ya kutokea purukushani langoni mwa timu ya Yanga.

Kikosi cha Simba siku hiyo kilikuwa ni Mohamed Mwameja, Godwin Aswile, Deo Mkuki, Mustapha Hoza, George Masatu, Iddi Selemani ‘Mayor’, Athumani China, Hussein Marsha/George Lucas ‘Gazza’, Madaraka Selemani, Edward Chumila (marehemu) na Dua Said.

Kikosi cha Yanga kilikuwa ni Stephen Nemes, Selemani Mkati, Kenneth Mkapa/ Willy Martin, Salum Kabunda ‘Ninja’ (marehemu), Costantino Kimanda, Nico Bambaga (marehemu), Mohamed Hussein ‘Mmachinga’/Ali Yusuph ‘Tigana’, Sekilojo Chambua, Said Mwamba ‘Kizota’ (marehemu), James Tungaraza ‘Bolizozo’ na Edibily Lunyamila.

4. Sekilojo Chambua
Wapenzi wa soka wa klabu ya Yanga sio rahisi kulisahau jina la mpachika mabao wao,  Sekilojo Chambua, kwa sababu ameichezea timu hiyo yenye maskani yake makuu Mtaa wa Jangwani na Twiga kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka 1994 hadi 2005.

Chambua anakumbuka mechi iliyokutanisha timu yake ya Yanga dhidi ya Simba, mchezo uliochezwa katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma siku ya Jumamosi ya Novemba 8, mwaka 1997.

Mechi hiyo ilikuwa ni moja ya mchuano wa mwisho wa ligi kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo matokeo ni kwamba Yanga waliifunga Simba bao 1-0.

Chambua

Chambua anakumbuka mechi hiyo kwa sababu yeye ndiye aliyefunga Yanga bao lile pekee la ushindi ambalo liliwawezesha kunyakuwa Kombe la Jamhuri ya Muungano kwa mara ya tatu mfululizo, na hivyo kulitwaa Kombe hilo moja kwa moja.

Kikosi cha Yanga kilichotwaa taji hilo kilikuwa ni Joseph Katuba (marehemu), Mzee Abdallah, Kenneth Mkapa, John Paul Masanja, Abdallah Msheli, Salvatory Edward, Sekilojo Chambua, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, Idelfonce Amlima, Thabit Bushako na Edibily Lunyamila.

Kikosi cha Simba kilikuwa ni Issa Manofu, Abubakar Kombo, Alfonce Modest, Mathias Mulumba, George Masatu, Nico Bambaga (marehemu), Madaraka Selemani, Rajab Msoma (marehemu), Ahmed Mwinyimkuu, Bitta John, William Fanbullah, Thomas Kipese na Abdallah Msamba.


No comments:

Post a Comment