Mashabiki wa Kariakoo ya Lindi |
Mshambuliaji wa Kariakoo Lindi, Salum Abilah akijaribu kumtoka beki wa Abajalo, Jamal Machelanga kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa uliochezwa katika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana |
TIMU ya Abajalo ya Dar es Salaam jana ilishindwa kutumia
Uwanja wa nyumbani baada ya kukubali kutoka sare ya mabao 2-2 na Kariakoo ya
Lindi kwenye mchezo Ligi ya Mabingwa wa Mikoa, mchezo uliochezwa Uwanja wa
Karume jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo wa raundi ya pili ulishuhudia Abajalo wakijipatia
mabao yake kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji Abubakar Hiza dakika ya
20 na kiungo Wazir Abdallah dakika ya 39, wakati Kariakoo Lindi wakishangaa
nyasi bandia na maghorofa yaliyozunguka
Uwanja wa Karume.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko
na kuanza kucheza mchezo wa tahadhari kwani kila timu ilianza kucheza kwa kujihami.
Kariakoo Lindi ambayo ilikuwa na mashabiki wengi ilibadilika
na kucheza soka la kujiamini na kufanikiwa kurudisha mabao yote kupitia kwa
nahodha wao Hanafi Suleiman dakika ya 64 na mshambuliaji Salum Abilah dakika ya
69 kwa njia ya penalty baada ya beki wa Abajalo Rahim Abdallah kushika mpira
eneo la penalti.
Baaada ya kusawazisha mabao hayo Kariakoo iliyokuwa
imeambatana na uongozi wote wa chama cha soka (LIREFA) wakiongozwa na
Mwenyekiti wake Francis Ndulane walionyesha kandanda safi.
Baada ya mchezo kocha wa Kariakoo
Lindi, Nyamwase Rashid na kusema kuwa timu yake ilipoteza umakini kipindi cha
kwanza na kuruhusu mabao hayo lakini baadae wachezaji walibadilika na kuweza
kurudisha mabao yote jambo ambalo anaamini kwenye mchezo wa marudiano watafanya
vizuri.
“Timu ilipoteza umakini mwanzoni ila kwa matokeo haya naamini
tutasonga mbele kwani ugeni wa uwanja wa nyasi bandia ulitugharimu”, alisema
Rashid
Kwenye mchezo wa juzi Friends Rangers iliwafunga African Sports ya Tanga mabao 2-1 kwenye mchezo uliochezwa uwanja wa Chamazi.
Mabao Friends Rangers yalifungwa na Hatibu
Kuduku dakika ya 23 na Joseph
Mwakigara dakika ya 80 huku lile la African Sports likifungwa na Thabit
Digola dakika ya 67
Ligi hii inaendelea tena mwishoni mwa wiki
No comments:
Post a Comment