SIMBA
imepata pigo kubwa baada ya beki wa timu hiyo, Shomari Kapombe kuugua malaria
kabla ya mechi yao ya leo ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting,
utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kapombe
anatazamiwa kuikosa mechi hiyo, ambayo ni muhimu kwa Simba kushinda ili iweza
kuwa na matumaini ya kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo.
Akizungumza jijini, Daktari wa timu hiyo, Cosmas Kapinga, alisema Kapombe anasumbuliwa
na malaria hivyo hataweza kucheza katika mechi hiyo.
Kapinga
alisema Kapombe amepewa mapumziko hadi atakapopata nafuu ambapo jana aliondolewa katika kambi ya timu
hiyo iliyoko Bamba Beach, Kigamboni, Dar es Salaam.
Alisema
kutokana na hali yake, anatarajia kupumzika ili awe fiti zaidi katika mechi yao
dhidi ya Polisi Morogoro, itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Wakati
huo huo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Liewig amekua na imani na kikosi
chake kuibuka na ushindi katika mchezo huo, kutokana na kikosi chake
kimekamilika katika idara zote.
Liewig
alisema kukosekana kwa Kapombe si tatizo kubwa katika kikosi chake, kwani pengo
lake linatarajiwa kuzibwa na beki mwingine.
Alisema wachezaji ambao wamebaki wanaweza kufanya
kazi nzuri na kuibuka na ushindi katika mechi hiyo.
Simba
tayari wametema ubingwa wa ligi hiyo, kutokana na kuwa hata kama watashinda mechi zao nne zilizosalia
hawataweza kuifikia Yanga inayoongoza kwa pointi 56.
Timu
hiyo inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 36, huku Azam FC ikiwa ya pili
yenye pointi 47 na Kagera Sugar inashika nafasi ya tatu kutokana na pointi 40.
No comments:
Post a Comment