BEKI wa Simba, Joseph Owino ametamba kuwa safu ya ulinzi ya
timu hiyo itakuwa tishio, kufuatia ujio wa Kaze Gilbert kutoka nchini Burundi.
Ukuta wa Simba umekuwa na shida tangu kuondoka kwa beki wao
kisiki, Kelvin Yondani ambaye alihamia kwa mahasimu wao wa jadi Yanga msimu
uliopita.
Kwa sasa safu ya ulinzi ya Simba itajengwa na Nassor Masoud
`Chollo`, Shomari Kapombe, Kaze Gilbert na Joseph Owino kwenye kikosi cha
kwanza hali ambayo inaelezwa kuwa ni ukuta mgumu zaidi kupata kutokea hapa
nchini.
Owino aliiambia LENZI YA MICHEZO jana kuwa anaifahamu Simba kwa miaka
mingi na kwamba mwaka huu safu yake ya ukuta itakuwa tishio, hasa kutokana na
wachezaji wanaocheza nafasi hiyo kuwa wazuri.
“Nikiangalia wachezaji waliopo katika safu ya ulinzi,
ninaimani msimu huu Simba ni tishio, nalifahamu soka la Tanzania na
nakuhakikishia kwamba ukuta wetu utakuwa ni zaidi ya ule wa Berlin,” alisema.
Owino alisema hana hofu juu ya uwezo wa mabeki wenzake,
kwani anawafahamu na kwamba tatizo la mipira ya juu limekwisha kwa kuwa yeye na
Kaze wapo kwa ajili hiyo.
“Jambo la muhimu ni ushirikiano na hili tunalifanyia kazi
vizuri sana,” alisema.
Beki huyo alisema alivyoiona Simba katika mechi ya kirafiki
dhidi ya URA, walicheza vizuri na asilimia kubwa wachezaji waliocheza katika
mechi hiyo wapo kikosini.
Owino aliyesajiliwa na klabu hiyo kwa mkataba wa miaka
miwili kwa dau la dola elfu 20, ni mara ya pili kuchezea klabu hiyo ya Simba.
No comments:
Post a Comment