PAMBANO la watani wa jadi Simba na Yanga, limeonekana
kuwabakisha Kipa, Juma Kaseja na beki wa kulia wa timu hiyo, Nassoro Masoud
'Chollo' katika usajili ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kaseja na Chollo ni kati ya wachezaji wanaotarajiwa
kuongezewa mikataba mipya kabla ya mechi yao, itakayochezwa Mei 18, mwaka huu,
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana, zilielezwa
kwamba uongozi wa klabu hiyo, umeanza kuandaa mikataba ya wachezaji wote ambao
wataendelea kuitumikia timu hiyo.
Chanzo hicho
kilieleza kwamba, mikataba ya wachezaji hao itakamilika kabla ya mechi hiyo,
ili waweze kucheza wakiwa na matumaini mapya ya kuendelea kuichezea timu hiyo,
lakini kikubwa ni kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo.
Kilieleza matarajio ya uongozi huo ni kutaka
kumalizana na wachezaji wote ambao mikataba yao imemalizika ili wabakie na wale
wapya watakaosajiliwa kuanzia msimu ujao.
Wakati huo huo, Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ezekiel
Kamwaga alikiri kuwepo kwa mazungumzo ya
mwisho ya wachezaji ambao wataendelea nao msimu ujao.
Kamwaga alisema wachezaji hao wanatarajia kupewa
mikataba mipya kabla ya mechi yao dhidi ya Yanga, kutokana na wapo katika hatua
ya mwisho ya kukamilisha makubaliano yao.
"Tumeanza kuzungumza na baadhi ya wachezaji
ambao tuna imani tutaendelea nao msimu ujao na wenyewe wanajijua," alisema
Kamwaga.
Baadhi ya wachezaji wanaotarajia kumaliza mikataba
yao ni Amir Maftah, Felix Sunzu, Amri Kiemba, Shamte Ally, Chollo na Kaseja.
Kutokana na hali hiyo tayari Kaseja alikuwa ameanza
kufanya mazungumzo na baadhi ya klabu nchini ikiwemo klabu ya Ashanti United ya
jijini Dar es Salaam, ambayo ilionyesha nia ya kumsajili.
No comments:
Post a Comment