LUIS SUAREZ (Liverpool)
Huyu
ndiye Luis Suarez a.k.a ‘Mla watu wa Ajax’
*Tyson amkubali kwa kumpiga jino Ivanovic
* Alishawahi kumng’ata mtu akiwa Uholanzi
HILI ni tukio lililoushangaza ulimwengu wa soka juzi – baada
ya Luis Suarez (26) akiwa na hasira kumng’ata beki wa Chelsea, Branislav
Ivanovic, katika pambano kati ya Liverpool na Chelsea lililomalizika kwa sare
ya 2-2.
Tukio hilo la kushangaza lilitokea katika dakika ya 65 ya
mchezo, kati ya timu hizo na kuwashtua mamilioni ya mashabiki waliokuwa wakitazama
mechi hiyo na kuzua hasira huku wengi wakitaka afungiwe muda mrefu.
Hii ni mara ya pili kwa mshambuliaji huyo mtata kumng’ata
mpinzani wake, aliwahi kufanya hivyo wakati akichezea klabu ya Ajax, mwaka
2010.
Kitendo ambacho kilimpa jina la utani la The Cannibal of Ajax
(Mla Nyama za Watu wa Ajax) kutokana na kumng’ata begani kiungo wa PSV
Eindhoven, Otman Bakkal — alifungiwa mechi saba kutokana na tukio hilo.
Usiku wa juzi mshambuliaji huyo wa Uruguay – ambaye amekuwa
akitawaliwa na matukio ya utata – alikiri kumng’ata Ivanovic na kuomba radhi.
Suarez aliomba msamaha wake wa kwanza kupitia akaunti yake ya
Twitter “Ni tabia isiyo vumiliika, nimesikitishwa na kilichotokea.”
Dakika chache baadaye aliomba radhi kupitia taarifa
iliyotolewa na Liverpool, akisema amejaribu kumtafuta Ivanovic azungumze naye.
Suarez aliongeza: “Ninamuomba radhi pia kocha wangu, wachezaji
na kila mtu kwenye klabu ya Liverpool nimewaangusha.”
Tukio hilo lilitokea kwenye uwanja wa Anfield wakati Ivanovic
alipomzuia Suarez kwenye eneo la hatari la Chelsea.
Ivanovic alijaribu kumuonyesha mwamuzi Kevin Friend, sehemu
aliyong’atwa na Suarez lakini mwamuzi hakuchukua hatua yoyote.
Bado haijajulikana hatua ambazo atachukuliwa, lakini mabosi wa
FA wanalipitia tukio hilo.
Mashabiki wanalilia kuona Suarez anakutana na adhabu kali
ikiwa ni pamoja na kufungiwa mechi nyingi, huku wengine wakitoa ushauri wa njia
za kumzuia asirudie tena kufanya kitendo kama hicho.
Maoni ya
Liverpool
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers alisema: “Baada ya kuangalia
video ya tukio hilo, tabia yake haikubaliki na nimemwambia.”
Mkurugenzi Mkuu wa klabu, Ian Ayre alionya: “Tabia yake
haiendani na mtu yoyote anayevaa jezi la Liverpool, tutalishughulikia swala
hili ndani kwa ndani na tunasubiri maamuzi ya FA.”
Utata wa Suarez
Kabla ya Tukio hilo Suarez aliwahi kufungiwa mechi nane kwa
kuonyesha matendo ya ubaguzi wa rangi dhidi ya beki wa kushoto wa Manchester
United, Patrice Evra.
Kudaka mpira kwenye mstari wa goli kwenye mechi ya robo
fainali dhidi ya Ghana, tabia ya kujiangusha na kutafuta penalti kwenye mechi
za ligi kuu.
Desemba 2011, alifungiwa kutokana na kuwaonyesha ishara ya
matusi mashabiki wa Fulham.
Oktoba 2013, alisherekea bao dhidi ya Everton kwa kujiangusha
mbele ya David Moyes — ambaye aliwahi kusema kwamba wachezaji wanaojiangusha
kama Suarez wanawakera mashabiki.
Maoni ya
Wadau
Gwiji wa Liverpool, Graeme Souness alisema: “Sijawahi kuona
kitu kama hiki kwenye mechi ya soka, hivi hutokea kwenye michezo ya kitoto,
kila akiingia uwanjani lazima afanye kitu cha kijinga.”
Kiungo wa zamani wa Liverpool, Jamie Redknapp alisema:
“Tofauti na matarajio ya wengi ameiangusha klabu.”
Tyson
amkubali Suarez
Kitendo cha Luis Suarez kumng’ata Ivanovic amepata shabiki
mmoja tu ambaye ni Mike Tyson.
Bingwa wa zamani wa uzito wa juu duniani, ambaye aliwahi
kumng’ata sikio Evander Holyfield mwaka 1997, - alimfuata Suarez kwenye mtandao wa Twitter dakika chache baada
ya tukio hilo.
Tyson (46), alifungiwa kupigana baada ya tukio hilo na kutozwa
faini ya pauni milioni 2.
No comments:
Post a Comment