ALIPOJIUNGA na Manchester City ni wazi kwamba
alionekana lulu, na kilichomchosha zaidi kukaa kwa washika Bunduki wa jiji la
London ni kukaa misimu mingi bila kutwaa taji lolote. Samir Nasir alitaka
kufanya kazi ambao licha ya kumpa mshahara mzuri lakini pia imlipe kwa maana ya
mafanikio kwa timu anayoichezea.
Kocha wa Manchester City, Roberto Mancini
alijiona amefanya uamuzi sahihi kwa kumanasa kiungo mshambuliaji mwenye uwezo
mkubwa wa kumiliki mpira na kufunga mabao. Alisaidia kuipa ubingwa timu hiyo
msimu uliopita na kujivuna kuwa katika kikosi cha mabingwa wa Uingereza.
Kwa msimu huu, hakuonekana kuwa ni mwenye
makali, hasa baada ya City kumnyakua Yaya Toure ambaye amekuwa chaguo la kwanza
kwa Mancini huku Nasri akipewa nafasi chache za kucheza na mara nyingi alikuwa
hatoi mchango uliotarajiwa na Mancini.
Alionyesha kuwa si mwenye furaha ndani ya
kikosi cha City msimu huu, hasa kutokana na kusugua benchi kwa muda mrefu na
wakati mwingine kusumbuliwa na majeraha ambayo kwa ujumla yalimfanya ashindwe
kabisa kuwika.
Katika moja ya mechi kocha Mancini alilumbana
na Nasri hasa kwa kumtuhumu kushindwa kufuata maelekezo yake hii ilitafsiriwa
kwamba siku za kijana huyo Mfaransa kwenye kikosi cha City zimekwisha kwani
kulifutiwa uvumi mkali juu ya nyota huyo kutaka kuondoka katika msimu wa dirisha dogo.
Sababu ya kutaka kuondoka aliiweka wazi kwa
kusema kwamba kiwango chake kimeonekana kutokumfurahisha kocha wake hivyo
yawezekana kuna klabu ikaona anafaa kuitumikia . “Mancini aliniambia kwamba
haridhiki na kiwango changu, katika mazingira haya ni lazima ujitume sana
mazoezini, lakini kama hafurahi basi jambo la muhimu ni kuondoka,” alisema.
Kocha Mancini alisema anataka
kumtimua na alimtoa kwenye kikosi mara baada ya kupishana kauli na hakumpanga katika mechi tano mfululizo
bila sababu wala kumueleza chochote. “Ni kweli sijawa na msimu mzuri, lakini si
kweli kwamba nimeshuka kiwango changu kwa asilimia 50, unapokuwa hupewi nafasi
na kuaminiwa mara kadhaa kila unachofanya hata kama ni kizuri hakionekani,”
alisema.
Lakini nini alichotakiwa
kufanya Nasri? Anachofanya sasa kwa timu yake pengine ndiyo jambo ambalo
alitakiwa kufanya tangu mwanzo wa msimu hasa kutokana na ukweli kwamba kwa sasa
amekuwa mtu anayetoa mchango muhimu sana kwa timu yake akicheza katika nafasi
ya kiungo mshambuliaji.
Kosa moja alilokuwa
akilifanya Mancini ingawa hakutaka kukubali ni kumpanga Nasri katika nafasi ya
kiungo mchezeshaji huku akimpa jukumu la kuwalisha mipira washambuliaji na
kusaidia safu ya ulinzi, na wakati huo akitaka kuona matunda yake katika
kufunga mabao.
Wanaomtazama sasa Nasri
watamuona kwamba amerejea katika kiwango chake, hii inatokana na ukweli kwamba
amekuwa akipangwa katika nafasi sahihi ambayo inamfanya awe na uwezo wa kufanya
mambo yake kwa uhuru zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzo.
“Inatakiwa kufahamu aina ya
mchezaji na aina ya uchezaji wake, Mancini hakuwa akimtumia vizuri Nasri, na
iliniuma alipomsuhutumu kwamba ameshuka kiwango, kiuhalisia Nasri ni kiungo
mshambuliaji kumbadilisha namba ni sawa lakini unapombadili usitegemee kupata
matunda kama yaleyale ya mwanzo,” anasema kocha wake wa zamani Arsene Wenger.
Wenger anaongeza kwa kusema
kuwa, alipomsajili, alimsaidia katika kubadili uchezaji wake kutoka ule wa
taratibu na kuwa wa kasi, na alimjengea mazingira mazuri ya kuwa na maamuzi
pale anapokuwa na nafasi, lakini kwa Mancini alimhitaji Nasri kuchezesha
wenzake na hata akifunga bao basi itokee kama dharura.
Kwa sasa Nasri ameoenekana
kuwa lulu kwa City, mchango wake umeiwezesha timu hiyo kuingia fainali ya kombe
la FA baada ya kuitoa Chelsea lakini pia amekuwa akimianiwa kuwa katika kikosi
cha kwanza cha vijana wa Etihad.
No comments:
Post a Comment