JANA na leo, zimetolewa habari tofauti
kuhusiana na klabu ya Simba ambazo uongozi umeona ni vema uzitolee ufafanuzi kwa
lengo la kuweka rekodi sawa. Ufuatao ndiyo ufafanuzi wa taarifa
hizo.1. SIMBA
KUZUIWA HOTELINI
SAA mbili kabla ya mechi ya jana baina
ya Simba na Coastal Union ya Tanga, mmiliki wa Saphire Court Hotel alitoa
taarifa kwa uongozi wa Simba kwamba ataizuia timu isiondoke hotelini kwa vile
anaidai Sh milioni 25 na anataka alipwe zote jana. Ikumbukwe kwamba Simba imekuwa ikikaa
hotelini hapo kwa muda mrefu sasa wakati inapoweka kambi. Pia, wajumbe wa Kamati
ya Utendaji ya Simba walifanya mkutano na wachezaji wote wa Simba katika hoteli
hiyo usiku wa kuamkia jana. Wamiliki wa hoteli hiyo hawakutoa
taarifa yoyote kwa uongozi wakati huo juu ya dhamira yao hiyo.Wamiliki hao
hawakutoa taarifa asubuhi ya mechi na walisubiri mpaka wakati timu inataka
kuondoka ndiyo wakachukua hatua hiyo. Kwa uongozi wa Simba, hatua hiyo
ilikuwa ya ghafla mno. Ifahamike kwamba kabla ya hatua hiyo, uongozi wa Simba
ulikuwa umemlipa mmiliki huyo kiasi cha zaidi ya Sh milioni 30 katika kipindi
cha miezi 10 iliyopita. Mara baada ya mechi dhidi ya Libolo ya
Angola, Saphire walilipwa Sh milioni 15 na Simba. Hii maana yake ni kwamba klabu
yetu ina utaratibu wa kulipa madeni yake na si watu wasiolipa kama hatua hiyo ya
wamiliki wa Saphire inavyotaka kueleza. Uongozi wa Simba tayari ulitoa ahadi ya
kumaliza deni lote inalodaiwa baada ya kulipwa fedha zake inazodai zinazotakiwa
kulipwa wakati wowote mwezi huu au ujao. Simba inadai zaidi ya Sh milioni 500
kwa wadai wake wawili (Etoile du Sahel ya Tunisia na Push Mobile) na inataraji
kulipwa fedha hizo. Itakapolipwa fedha zake hizo, Simba
itakuwa na uwezo wa kulipa madeni yake yote inayodaiwa na watu binafsi na
makampuni bado ikabaki na fedha za kufanya mambo mengine ya
kimaendeleo. Wakati
ikisubiri ilipwe fedha zake inazodai, Simba itaendelea kulipa madeni yake
taratibu kwa kadri itakavyoweza. Ifahamike kwamba kwa sasa chanzo kikuu cha
mapato ya klabu ni fedha za mapato ya milangoni na za udhamini wa bia ya
KILIMANJARO ambazo hazikidhi mahitaji yote ya timu. Kwa kuzingatia nakisi hii ya mapato na
matumizi, Simba SC imeanza mchakato wa kutafuta wafadhili na wadhamini kokote
walipo duniani ili kuongeza mapato yake. Tayari mawasiliano yameanza na wenzetu
wa Sunderland ya England kupitia mradi wao wa Invest in Africa ili Simba nayo
ifaidike. Simba SC inaomba
pia umma ufahamishwe kwamba klabu ya soka kudaiwa si dhambi. Iwapo klabu kubwa
na tajiri duniani kama vile Manchenster United, Real Madrid na Liverpool zina
madeni, inakuaje madeni ya Wekundu wa Msimbazi (tena ambayo klabu ingeweza
kuyalipa yote iwapo wadeni wake nayo wangewalipa kwa wakati) yaonekane kama kitu
kigeni Uongozi unaahidi
kwamba utalipa madeni yake yote kwa kadri utakavyojaaliwa. Kwenye lugha ya
kibenki, credit worthiness ya mteja inamaanisha mteja ambaye anakopa na kulipa.
Simba inapenda kusisitiza kwamba ni taasisi ya kuaminika na yenye heshima kubwa
na bado inavutia watu na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Simba ni
CREDIT WORTHY INSTITUTION ! Hata hivyo, uongozi wa Simba unafikiria
kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wamiliki wa Saphire Court Hotel kwa kitendo
chake cha kuwazuia wachezaji na viongozi wa Simba hotelini kabla ya mechi ya
jana. Simba inachukulia
kitendo kile kama hujuma na kisheria kinaangukia katika kundi la FORCED
IMPRISONMENT kwa wamiliki kuwazuia watu kinguvu hotelini kwao. WAMILIKI
hawakutoa notisi kwa uongozi au taarifa yoyote ya mdomo au maandishi kabla ya
kuchukua hatua hiyo. Lengo
lilikuwa ni kuchafua heshima na hadhi ya Simba kwa hoteli ambayo imetoka kulipwa
Sh. milioni 15 wiki mbili tu zilizopita. Uongozi wa Simba SC unaapa kuilinda na
kuitetea hadhi ya klabu yetu kwa nguvu zetu zote, akili zetu zote na maarifa
yetu yote.
2. WACHEZAJI, BENCHI LA
UFUNDI KUFUKUZWA
KUNA
taarifa zimeenezwa pia kwamba kuna wachezaji wa Simba wamesimamishwa au
kufukuzwa kuchezea Simba. Habari hizi nazo hazina ukweli wowote. Ukweli ni kwamba, uongozi wa Simba
umetoa ruksa kwa benchi la ufundi kupanga timu ambayo litaona inafaa kwa mechi
husika. Uongozi hautaingilia, kwa namna,njia au aina yoyote ile utendaji wa
benchi la ufundi. Hakuna
mchezaji yeyote aliyesimamishwa hadi sasa. Pia uongozi unakanusha taarifa kuwa
Daktari Mkuu wa Klabu, Cosmas Alex Kapinga, kuwa naye ameachia ngazi. Habari
hizi hazina ukweli kwani daktari huyo ana ruhusa ya kikazi ya wiki mbili
inayojulikana.
HITIMISHO
KATIKA namna ya kipekee kabisa, uongozi
wa Simba unapenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwa washabiki wake
waliojitokeza Uwanja wa Taifa na kuisapoti timu kwa asilimia 100. Uongozi
unathamini sana mchango wa wanachama wake na unaahidi kufanya kila unachoweza
kuwarejeshea tena furaha mioyoni mwao. Uongozi pia unatumia nafasi hii
kuwapongeza wachezaji na benchi la ufundi ambao walicheza mechi ya jana katika
mazingira magumu. Walicheza bila ya kufanya warm up na wakitoka kuwa wamezuiwa
hotelini jambo ambalo lingeweza kuwaondoa mchezoni.
Imetolewa
naEzekiel
Kamwaga
Ofisa
Habari
Simba SC
No comments:
Post a Comment