Mshambuliaji hatari wa timu ya Coastal Union, Nsa Job, amesema anasikitishwa na kitendo cha kipa wa timu ya JKT Ruvu, Patrick, kutompigia simu wala kumuona hadi sasa.
Nsa alipata maumivu makubwa ya goti lake wakati alipogongana na kipa wa timu hiyo katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu katika uwanja wa Chamazi, Complex, Oktoba mwaka jana na kupelekea goti lake kuzunguka. Lakini baada ya kufanyiwa upasuaji uliokwenda vizuri nchini, India, mshambuliaji huyo wa zamani wa timu za Simba na Yanga, ameanza mazoezi na sasa ana matumaini ya kucheza soka kwa mara nyingine.
“Yule kipa wa JKT Ruvu, hajawahi kunipa pole wala kunijulia hali hadi sasa. Unajua nilikata tamaa ya kucheza tena soka nilipoona hali ya mguu wangu mara baada ya kuumia. Nilijua ndiyo mwisho wa kipaji changu, lakini sasa nafarijika na kujiona mwenye nguvu mpya baada ya kuanza mazoezi” anasema, mshambuliaji huyo mwenye mabao matatu hadi sasa.
” Narudi kivingine, waambie mashabiki kuwa narejea kwa nguvu na watarajie mambo mazuri kutoka kwangu”, Nsa anasemaje kuhusiana na mwenendo wa ligi kuu. ” Ligi imeingia katika kipindi ambacho kinachangamoto nyingi. Mimi nafikiri timu iliyofanya maandalizi mazuri ndiyo itapata matunda” anamaliza.
Ikumbukwe TFF waliomuomba radhi Nsa kwa kukosekana gari la wagonjwa wakati wa mchezo huo.
Coastal imeanza mzunguko wa pili kwa ushindi wa bao 3-1 dhidi ya Mgambo FC kutoka Tanga.
No comments:
Post a Comment