MCHAKATO TIKETI ZA ELEKTRONIKI WAFIKIA ASILIMIA 80
Ujenzi wa vifaa
(turnstiles) vitakavyotumika kwa ajili ya tiketi za elektroniki kwenye viwanja
saba kati ya nane vitakavyotumia mfumo huo umekamilika kwa asilimia
80.
Viwanja hivyo ni Chamazi (Dar
es Salaam), Jamhuri (Morogoro), Kaitaba (Bukoba), Sokoine (Mbeya), Sheikh Kaluta
Amri Abeid (Arusha), na Mkwakwani (Tanga).
Wakati Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam tayari una turnstiles, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza bado
haujaruhusu ufungaji wa vifaa ukisubiri idhini kutoka kwa wamiliki wake (CCM
Makao Makuu).
Vifaa vitakavyotumika kusoma
tiketi za elektroniki katika viwanja hivyo vinatarajiwa kuwa vimefungwa kufikia
Februari 20 mwaka huu.
Hakutakuwa na matumizi ya
fedha taslimu mara baada ya mradi huo wa tiketi la elektroniki kuanza, kwani
tiketi zitakuwa zikinunuliwa kwa kadi maalumu (smart card) katika vituo
mbalimbali vitakavyotangazwa baadaye.
Benki ya CRDB ndiyo
iliyoingia mkataba na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutengeneza
tiketi za elektroniki baada ya kuibuka mshindi kwenye tenda.
WAKENYA KUCHEZESHA MECHI YA
AZAM
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) limewateua waamuzi kutoka Kenya kuchezesha mechi ya kwanza ya
raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam ya Tanzania na Al Nasir Juba
ya Sudan Kusini itakayofanyika jijini Dar es Salaam kati ya Februari 15 na 17
mwaka huu.
Mwamuzi wa kati atakuwa
Davies Omweno na atasaidiziwa na mwamuzi msaidizi namba moja Peter Keireini,
mwamuzi msaidizi namba mbili Gilbert Cheruiyot wakati mwamuzi wa mezani Anthony
Ogwayo.
Kamishna wa mechi hiyo
atakuwa Hassan Mohamed Mohamud kutoka Somalia. Waamuzi wa mechi ya marudiano
itakayochezwa jijini Juba watatoka Rwanda wakiongozwa na Gervais
Munyanziza.
CAF YATEUA WATANZANIA
KUCHEZESHA CAMEROON
Waamuzi wa Tanzania
wakiongozwa na Israel Mujuni wameteuliwa kuchezesha pambano la awali la raundi
ya kwanza kuwania Kombe la Shirikisho kati ya UFC Haut Nkam ya Cameroon na US
Bougouni ya Mali.
Kwa uteuzi huo wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Mujuni na wenzake Ali Kinduli, Samuel Mpenzu na
Waziri Sheha watachezesha mechi hiyo itakayofanyika kati ya Februari 15 na 17
mwaka huu.
Pierre Alain Mouguengui
kutoka Gabon ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo. UFC Haut Nkam na US
Bougouni zitarudiana wiki mbili baadaye nchini Mali.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment