Rais wa TFF, Tenga |
WARAKA wa
marekebisho ya Katiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umepita baada ya
kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu waliopiga kura.
Jumla ya Wajumbe
waliopiga kura kwa njia hiyo ya waraka ni 103 ambapo 70 wameunga mkono wakati
waliokataa ni 33. Idadi hiyo ni asilimia 68 ya kura zote zilizopigwa, hivyo
kupatikana theluthi mbili ya kura zilizopigwa ili kufanya marekebisho kikatiba.
Kura
zilizosema ndiyo kutoka kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa vyama vya mikoa ni 46,
wajumbe kutoka vyama shiriki ni 13 wakati klabu za Ligi Kuu zilizounga mkono ni
11.
Kamati ya
Utendaji ya TFF inawashukuru wajumbe wote wa Mkutano Mkuu- kwa waliounga mkono
na waliokataa kwa vile walikuwa wanatekeleza wajibu wao wa kikatiba.
Vipengele
vilivyoingizwa ni ‘club licencing’ kama ilivyoagizwa na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF), Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF kama ilivyoshauriwa na
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na kuondoa nafasi ya Makamu wa
Pili wa Rais.
Vilevile
Kamati ya Utendaji itakutana Desemba 23 mwaka huu kufanya marekebisho ya Kanuni
za Uchaguzi, kutokana na kupitishwa kwa marekebisho hayo ambayo yanaunda Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF. Pia itachagua wajumbe wa Kamati ya Rufani ya TFF.
Mkutano Mkuu
wa TFF ambapo pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi utafanyika Februari 23 na 24
mwakani. Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, wajumbe wanatakiwa kupewa taarifa ya
Mkutano Mkuu siku 60 kabla.
Wakati huo
huo: Mikoa sita ambayo ni wanachama wa Chama cha Soka ya Wanawake Tanzania
(TWFA) haitashiriki katika uchaguzi wa chama hicho utakaofanyika Desemba 19
mwaka huu mjini Morogoro.
Kwa mujibu
wa taarifa ya TWFA, wanachama hao hawatashiriki kwa vile hadi sasa haijapokea
taarifa za uchaguzi kwenye vyama hivyo. Vyama hivyo ni vya mikoa ya Arusha,
Kilimanjaro, Mbeya, Rukwa, Shinyanga na Tabora.
No comments:
Post a Comment