Kocha Ernust Brands wa Yanga akiwa na wachezaji baada ya kumaliza mazoezi |
Wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini leo huku kocha wao mpya Ernust Brands akifuatilia kwa makini |
ZIKIWA zimebakia siku moja kabla ya mchezo wa watani wa
jadi, Simba na Yanga ambao ni wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baadhi ya mbinu za
kutafuta ushindi zimekuwa zikiendelea kwa Wanajangwani.
Katika mazoezi ambayo, HABARI ZA MICHEZO iliweza kuyashuhudia kwenye
Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Yanga ilikuwa inanolewa na kocha mpya, Ernstus
Brands ilikuwa ikitengeneza kikosi maalum cha ushindi ambacho kitashuka kesho
kwenye uwanja huo huku kikiwa na damu mchanganyiko.
Baadhi ya wachezaji ambao waliweza kuonekana kupewa majukumu
ni pamoja na Haruna Niyonzima, Ally
Mustafa ‘Barthez’, Oscar Joshua, Hamisi Kiiza, Athuman Idd Chuji, Saimon Msuva,
Mbuyi Twite, Frank Domayo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Didier Kavumbagu na Kelvin Yondani, ambao walifanya mazoezi mepesi.
Yanga ambayo tofauti na siku nyingine ilikuwa imeimarisha
ulinzi kwa kile kilichobainika kwamba ni kuhofia watani wao wa jadi kujua mbinu
zao, ambazo zilikuwa zinatolewa na mholanzi huyo aliyejiunga na kikosi hicho
akitokea APR ya Rwanda.
Aidha baadhi ya wachezaji walionekana kupewa majukumu ya
ziada ya kupachika mabao ikiwa ni mikakati wa Ernstus Brands ya kuhakikisha
anapata ushindi huku mfumo ambao aliokuwa anautumia ni pamoja na ule wa 4-4-2
na 3-3-4.
Mazoezi hayo yalifanyika kwa muda wa dakika 120 ambazo
zilikuwa ni za nguvu hali ya juu inayoonyesha kwamba Mholanzi huyo anahitaji
matokeo bora katika mchezo wa kesho.
Katika hatua nyingine, ulinzi ulikuwa ni wa hali ya juu
kwenye mazoezi hayo ambapo hata mashabiki waliokuwa wanatarajia kuchungulia
kupitia nondo zilizopo kwenye ukuta huo hivyo mashabiki hao kujikuta
wakiambulia patupu.
Awali katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika
kwenye uwanja wa Taifa juzi Jumapili, Yanga iliweza kushinda African Lyon kwa
mabao 3-1 huku Kocha msaidizi, Fred Minziro akisema kuwa kazi iliyopo mbele yao
ni kubwa.
“Tunajua kwamba tuna deni la kulipa mabao 5-0 ya msimu uliopita
hivyo lazima tujitahidi na kuhakikisha kwamba tunapata ushindi ili tupate
pointi 10 wakati wenzetu nao wanahitaji kushinda ili kusonga mbele zaidi.
“Kwa hali ilivyo ni lazima tujitume kadri inavyowezekana ili
kuhakikisha tunawapa mashabiki wetu raha lakini najua nini cha kufanya ingawaje
siwezi kuahidi mambo makubwa kutokana na mpira kuwa na matokeo matatu,
kushinda, sare na kufungwa kwa hiyo lolote linaweza kutokea,” alisema Minziro.
Yanga kwa sasa ipo kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa
Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kushuka dimbani mara nne huku ikishinda michezo
miwili lakini imefanikiwa kupata sare moja na kufungwa mechi moja. Hadi sasa imefunga
mabao saba na kufungwa matano ikiwa na pointi saba.
No comments:
Post a Comment