Kamati
ya Uchaguzi ya TFF katika kikao chake kilichofanyika Septemba 15, 2012
ilijadili michakato ya uchaguzi wa vyama wanachama wa TFF inayoendelea
hivi sasa kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa TFF mwishoni mwa mwaka
huu. Kamati iliamua yafuatayo;
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NJOREFA)
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF ilibaini kuwa uongozi wa muda wa NJOREFA haukutoa
ushirikiano wa kutosha kuiwezesha Kamati ya Uchaguzi ya NJOREFA kuanza
mchakato wa uchaguzi kwa tarehe kwa tarehe iliyokuwa imepangwa na hivyo
kusababisha kuchelewa kuanza kwa mchakato huo wa uchaguzi wa mkoa huo
mpya.
Kamati
imebaini pia kuwa kutokana na changamoto za kiuongozi zinazoukabili
mkoa huo mpya, mchakato wa uchaguzi ulioanza Septemba 2, 2012
haukuzingatia kikamilifu Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Kutokana
na kasoro hizo za msingi, mchakato wa uchaguzi wa NJOREFA utaanza upya
Septemba 18, 2012 ukizingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Uchaguzi wa NJOREFA utafanyika Oktoba 28, 2012.
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA)
Kamati
ilibaini kuwa kuna mkanganyiko katika mchakato wa uchaguzi wa TAREFA na
kwamba mkanganyiko uliotokea umesababishwa na Kamati ya Uchaguzi ya
TAREFA kutotimiza wajibu wake wa kusimamia uchaguzi wa TAREFA kwa mujibu
wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Kutokana
na kuvurugika kwa mchakato wa uchaguzi wa TAREFA uliosababishwa na
kiwango kikubwa cha ukiukwaji wa Kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Uchaguzi
ya TFF imejiridhisha kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA haina uwezo wa
kusimamia majukumu ya uchaguzi wa TAREFA na kuzingatia kikamilifu
matakwa ya Kanuni za Uchaguzi ya Wanachama wa TFF.
Kwa
kuwa Kamati ya Uchaguzi wa TAREFA imeshindwa kutimiza wajibu wake na
hivyo kusababisha mkanganyiko na uvurugaji wa uchaguzi wa TAREFA, Kamati
ya Uchaguzi ya TFF kwa mamlaka yake yaliyoainishwa katika Katiba ya TFF
Ibara ya 49(1) na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya
10(6), 26(2) na (3) imeamua yafuatayo;
(i) Imefuta
Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA. Uongozi wa TAREFA unatakiwa kuteua Kamati
mpya ya Uchaguzi itakayoandaa na kutekeleza majukumu yake ikizingatia
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na Katiba ya TAREFA. Uteuzi wa
Kamati mpya ya Uchaguzi ya TAREFA ufanyike kabla ya Septemba 24, 2012.
(ii) Imefuta
mchakato wa uchaguzi wa TAREFA. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya
Septemba 25, 2012 na uchaguzi utafanyika Novemba 4, 2012.
Vyama vya Mpira wa Miguu mikoa ya Manyara (MARFA) na Kilimanjaro (KRFA)
Uchaguzi wa MARFA na KRFA utafanyika Septemba 22, 2012 kama ilivyopangwa.
UTENDAJI WA KAMATI ZA UCHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF
Kamati
imebaini baadhi ya viongozi wa vyama vya wanachama wa TFF wanaomaliza
muda wao wanashiriki kudhoofisha michakato ya uchaguzi ya vyama vya
mpira wa miguu kwa kutotoa fursa kwa Kamati za Uchaguzi za vyama
wanachama kuanza michakato ya uchaguzi kwa tarehe zilizopangwa na Kamati
ya Uchaguzi ya TFF.
Kwa
kuwa ni wajibu wa viongozi waliopo madarakani kuhakikisha kuwa vyama
vyao vinafanya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba zao na Kanuni za Uchaguzi,
Kamati ya Uchaguzi ya TFF haitasita kupendekeza kwa Mamlaka husika za
TFF vyama hivyo kuchukuliwa hatua za Kikatiba kwa kushindwa kutimiza
matakwa ya Katiba ya TFF kwa kuwa na uongozi ambao muda wa ukomo wa
madaraka utakuwa umepita na hivyo kutokidhi matakwa ya Ibara ya 12(2)(a)
ya Katiba ya TFF.
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF inavishauri vyama wanachama wa TFF kuzingatia ratiba
ya uchaguzi na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF wakati wote wa
michakato ya uchaguzi wa viongozi wa vyama vyao. Viongozi walioko
madarakani wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa Kamati za Uchaguzi kama
ilivyoianishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi.
Hamidu Mbwezeleni
Makamu Mwenyekiti
Kamati ya Uchaguzi ya TFF
No comments:
Post a Comment