UTAPELI WALAZIMISHA TCRA KUPIGA KAMBI KILOMBERO
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeweka kambi rasmi katika Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kwa lengo la kukabili wimbi la ulaghai na utapeli kwa njia ya simu uliokithiri katika eneo hilo, ambalo linashikilia asilimia kubwa ya matukio mkoani humo.
Akizungumza katika semina maalum iliyowashirikisha viongozi wa serikali mjini Ifakara, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Peter Mwasalyanda, amesisitiza kuwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika sekta ya mawasiliano nchini hayapaswi kuachwa yakihatarishwa na wahalifu wa mtandaoni.
Takwimu zilizowasilishwa na mamlaka hiyo zinaonyesha kuwa matukio ya ulaghai na utapeli kupitia simu za mkononi yamepungua kwa asilimia 25.29 kitaifa, yakiteremka kutoka majaribio 9,816 hadi 7,334 katika kipindi cha robo mwaka kuanzia Machi hadi Juni 2026.
Hata hivyo, takwimu hizo zilibainisha kuwa kati ya matukio yote yaliyoripotiwa katika kipindi hicho, Mkoa wa Morogoro pekee ulichangia matukio 2,079 sawa na asilimia 28.4, huku Wilaya ya Kilombero ikiongoza kwa kuwa na matukio 1,778 ambayo ni sawa na asilimia 86 ya mkoa mzima, wakati Mkoa wa Rukwa ukiripoti matukio 2,495 au asilimia 34. Pamoja na ukubwa wa tatizo hilo wilayani humo, uchambuzi wa jumla unaonyesha kuwa matukio ya utapeli wa mtandaoni yamepungua kwa asilimia 69 kulinganisha na kipindi cha kuanzia Septemba 2023 hadi Juni mwaka huu.
Mwasalyanda alifafanua kuwa uhalifu huo wa mtandao umekuwa ukijitokeza katika mbinu mbalimbali ikiwemo udanganyifu, udukuzi wa mifumo, wizi au matumizi yasiyoidhinishwa ya taarifa binafsi, utapeli wa kielektroniki, usambazaji wa programu hatarishi na matumizi mabaya ya akaunti za kidijiti.
Kutokana na changamoto hizo, mkuu huyo wa TCRA alisisitiza kuwa serikali inalipa kipaumbele suala la usalama wa mtandao na kwamba haitoshi kuwa na mifumo salama pekee, bali jamii inahitaji kuwa na watu wenye uelewa mpana wa namna ya kujilinda wanapokuwa mitandaoni ili kuepuka kuangukia kwenye mikono ya matapeli.
Kiongozi huyo alibainisha kuwa ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini umekuwa mkubwa na unahitaji ulinzi thabiti, akitolea mfano wa kuongezeka kwa usajili wa laini za simu za mkononi kutoka 52,813,930 zilizokuwepo mwezi Machi 2021 hadi kufikia laini 116,952,295 mwezi Juni mwaka huu.
Sambamba na ongezeko hilo, akaunti za fedha kupitia simu za mkononi zimeongezeka kwa asilimia 166, kutoka takriban milioni 32.7 hadi kufikia akaunti 87,046,089, hali inayozidi kuchochea umuhimu wa wananchi na watumiaji wote kujenga utamaduni wa usalama wa mtandao katika shughuli zao za kila siku.

Post a Comment