TIRA Yazitaka Kampuni za Bima Kuja na Bidhaa Zenye Majibu Halisi kwa Wananchi
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imezitaka kampuni za bima nchini kuacha kupima ubora wa huduma zao kwa idadi ya watu waliojiunga pekee, badala yake zibuni bidhaa zinazotoa majibu ya vitendo na kukidhi changamoto halisi zinazowakabili wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bidhaa tatu mpya za bima ya maisha za Jubilee Life Insurance jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Bima, Dk Baghayo Saqware, ambaye hotuba yake ilisomwa na Mkurugenzi wa Uzingatiaji wa Sheria na Kanuni wa TIRA, Alex Meela, alisisitiza kuwa uelewa wa wananchi hujenga imani inayochochea matumizi endelevu ya bima.
Alisema kampuni zinazolenga kuongeza ujumuishi wa kifedha zinapaswa kwanza kuelewa mazingira halisi ya Watanzania na kuhakikisha mikataba inapatikana kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza ili kutoa uwazi wa faida, masharti na taratibu za madai.
“Wito wangu kwa Jubilee Life Insurance na kampuni nyingine za bima ni kuendelea kubuni bidhaa zinazotoa majibu kwa changamoto za wananchi na kuboresha maisha yao,” alisema Dk Saqware.
“Ubora wa bidhaa haupimwi kwa idadi ya watu waliojiunga pekee. Uelewa hujenga imani, na imani huongeza matumizi endelevu ya bima.”
Pia alisema uzinduzi wa bidhaa hizo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye uwezo wa kustahimili misukosuko.
Alisema hatua hiyo pia inaunga mkono Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020–2030, ambao unalenga kuongeza mchango wa bima ya maisha katika pato la taifa hadi kufikia asilimia 3 ifikapo mwaka 2030.
Alisema matumizi ya teknolojia yanapaswa kwenda sambamba na uwazi, usalama wa taarifa na urahisi wa matumizi akisisitiza umuhimu wa mikataba na nyaraka za bidhaa za bima kupatikana kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza ili wateja waweze kuelewa vizuri faida, masharti, gharama, muda wa bima, mambo yasiyolipwa na taratibu za kuwasilisha madai kabla ya kufanya maamuzi.
Alisema TIRA itaendelea kufuatilia utendaji wa bidhaa hizo mpya na kushirikiana na Jubilee Life Insurance kuhakikisha zinaendelea kutoa thamani iliyokusudiwa kwa wananchi.
“TIRA, kupitia idara yake ya utafiti, iko tayari kushirikiana na wadau katika kufanya tafiti zitakazochochea ubunifu na maendeleo ya soko la bima nchini,” alisema
Katika hafla hiyo alizindua bidhaa tatu za Jubilee Life Insurance ambazo ni Fanaka Plus, Smart Education Insurance Plan na Akiba Flex Plan, zilizobuniwa kusaidia wananchi katika uwekaji akiba, maandalizi ya elimu, ulinzi wa maisha na mahitaji mengine ya kifedha ya baadaye.
Alisema bima ya maisha ni nyenzo muhimu katika kujenga usalama wa kifedha na uwezo wa kustahimili changamoto kwa mtu binafsi, familia na taifa kwa ujumla.
Aidha alisema bima hiyo hulinda kipato na mipango ya maisha dhidi ya athari za kifo, ulemavu, maradhi, ajali na matukio mengine yasiyotarajiwa, huku pia ikiwasaidia wananchi kuweka akiba kwa ajili ya mahitaji muhimu ya baadaye, yakiwemo elimu ya watoto na ustawi wa familia.
“Bila ulinzi wa bima, tukio lisilotarajiwa linaweza kukatisha elimu ya watoto, kuathiri maisha ya familia na hata kuzima ndoto za wanufaika,” alisema.
“Kupitia bima ya maisha, ndoto na mipango hiyo inaweza kulindwa na kuendelea kuwa halisi.”
Hata hivyo, alisema matumizi ya bima ya maisha nchini bado hayajafikia kiwango kinachotarajiwa, huku baadhi ya sababu zikitajwa kuwa ni aina na muundo wa bidhaa zinazopatikana sokoni pamoja na uwezo wake wa kujibu mahitaji halisi ya wananchi.
Katika muktadha huo, aliipongeza Jubilee Life Insurance kwa kuwekeza katika utafiti na kuelewa mahitaji ya Watanzania kabla ya kuyatafsiri kuwa suluhisho la bima.
Alisema bidhaa hizo mpya zinatoa fursa kwa wananchi binafsi, wakiwemo wale ambao hawapo katika mipango ya bima za vikundi au waajiri, kupata huduma za bima kulingana na mahitaji, uwezo wa kifedha na mipango yao binafsi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jubilee Life Insurance Tanzania, Helena Mzena alisema kampuni hiyo imeendelea kuboresha bidhaa zake ili kuwapatia wateja thamani na uhakika zaidi.
Alisema Fanaka Life Plan imeboreshwa na kubadilishwa jina kuwa Fanaka Plus, ikiwapa wateja fursa ya kukuza fedha zao huku wakipata ulinzi wa maisha na amani ya moyo.
Andela alisema Akiba Flex inawapa wateja uhuru zaidi wa kuweka michango na kufanya miamala ya fedha kulingana na mahitaji yao.
Aidha, alisema Smart Education Insurance Plan imeundwa mahsusi kuwasaidia wazazi na walezi kujiandaa kwa ajili ya elimu ya watoto wao.
“Hapa, mteja anaweza kuweka akiba ili kuhakikisha ndoto za kielimu za watoto wake zinatimia, huku pia akiwa na ulinzi wa maisha,” alisema.
“Bidhaa hizi za bima ni ushahidi kwamba tunajali na kuthamini ndoto za wateja wetu na tunataka kuhakikisha ndoto hizo zinatimia bila msongo usio wa lazima.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Jubilee Insurance, Amyn Lalji alisema uzinduzi huo ni hatua nyingine muhimu katika safari ya Jubilee Life Insurance Tanzania na unaakisi dhamira ya kampuni hiyo ya kutoa suluhisho bunifu na la vitendo linalokidhi mahitaji yanayobadilika ya Watanzania.


Post a Comment