Ni Kishindo cha TSN: Waandishi 12 Watinga Kinyang'anyiro Tuzo za Samia



Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) imetikisa uwanja wa uandishi wa habari baada ya waandishi wake 12 kufuzu na kuingia rasmi kwenye kinyang'anyiro cha kuwania Tuzo za Samia Kalamu Awards (SKA) 2026 zinazotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.

Waandishi hao waliowania tuzo hizo katika makundi mbalimbali ni miongoni mwa waombaji 985 waliowasilisha kazi zao. 

Kwa upande wa gazeti la HabariLEO, waandishi wanaopigiwa kura  na  makundi wanayowania kwenye mabano ni Zena Chande (Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo), Anna Mwikola (Maliasili na Utalii), John Nditi (Mazingira) na Eva Sindika (Siasa). 

Rahel Pallangyo anawania tuzo za Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Uchumi na Fedha, Kazi na Ajira, Uchumi wa Buluu, Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Watu Wenye Ulemavu, Tehama na Ubunifu, Mwandishi Mahiri wa habari za picha na Jinsia Wanawake na Maendeleo. 

Mchangiaji wa gazeti la HabariLeo, Albano Midelo naye anawania tuzo za Madini, Maliasili na Utalii, Ofisa Habari Mahiri wa Serikali na Watu Wenye Ulemavu. 

Wanaopigiwa kura kwa upande wa Daily News ni Susan Mmary (Maliasili na Utalii), Esther Kasanga (Afya), Elikana Kuhenga (Habari, Sanaa, Utamaduni, Sanaa na Michezo), Sophia Kumkana (Uchumi na Fedha), Ally Mayala (Uwekezaji, Utawala Bora na Diplomasia). Ahmada Yahaya anawania tuzo ya Vijana, Siasa, Utawala Bora, Uchukuzi, Viwanda na Biashara na Silvester Domasa anayewania tuzo ya upande wa online. 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati ya tuzo hizo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Peter Mwasalyanda alisema mawasilisho 294 yamefuzu kupigiwa kura kati ya mawasilisho 3003. 

“Tunawashukuru waandishi wote waliotuma kazi zao, mwitikio wa safari hii ulikuwa mkubwa… Sasa tunakwenda kwenye hatua ya kupiga kura kuanzia leo (jana) mpaka Septemba 30 ndiyo itakuwa mwisho wa kupiga kura,” alisema. 

Alisema njia za kupiga kura ni mbili; kwa njia ya tovuti rasmi ya samiakalamuawards na ujumbe wa maandishi kwa simu ya mkononi kwa mpigakura kwenda kwenye uwanda wa ujumbe na kuandika SKA, namba ya mshiriki kisha atatuma kwenda 15200. “Kura za wananchi ni sehemu muhimu katika mchakato wa kupata mshindi kwa kuwa wao ni watumiaji wa maudhui ya habari, kamati inawaomba wananchi kushiriki kikamilifu kwenye kupiga kura,” alisema. 

Aliomba wadau wa habari kuendelea kujitokeza kudhamini tuzo hizo kama njia ya kuhamasisha ushiriki wa waandishi wa habari. 

Naye Mwenyekiti Mwenza wa Mashindano hayo na Mkurugenzi wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema mashindano hayo yamewaleta pamoja waandishi wa habari kutoka maeneo ya vijijini na mijini, akisisitiza kuwa washiriki watashindana kwa kuzingatia ubora wa kazi zao na si umaarufu wao.

Kwa mujibu wa mmoja wa majaji wa mashindano hayo, Bi. Beatrice Bandawe, amesema kuwa miongoni mwa maeneo yaliyopatiwa kipaumbele katika kazi zilizowasilishwa ni pamoja na afya, jinsia na makundi maalum, mazingira pamoja na elimu.

Huu ni msimu wa pili wa tuzo hizo baada ya kufanyika kwa mara ya kwanza mwaka jana. 

SKA ni tuzo za kitaifa nchini zenye lengo la kutambua, kuthamini na kuhamasisha uzalishaji wa maudhui ya ndani yenye ubora na weledi katika waandishi wa habari za maendeleo. 

Tuzo hizo zinaratibiwa kwa ushirikiano wa TCRA, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Tanzania (JAB). Kwa mujibu wa waratibu, kura za wananchi hutoa asilimia 60 huku za majaji zikiwa ni asilimia 40.


No comments