Serikali yafafanua kanuni mshahara kima cha chini
KIMA cha chini cha mshahara katika sekta binafsi nchini kinawekwa kwa kuzingatia sekta za kiuchumi, bunge limeelezwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mahonda, Abdullah Ali Mwinyi (CCM).
Mwinyi aliuliza: “Serikali haioni kama inatengeneza tabaka katika jamii kwa kanuni za mishahara ya kima cha chini kubagua kiwango cha mishahara kati ya kampuni za kigeni na za kizawa?”
Sangu alijibu kuwa kanuni ya kima cha chini cha mshahara inawekwa kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura ya 300. Sheria hiyo imeunda bodi za kima cha chini cha mshahara za kisekta kwa umma na binafsi.
Alisema, Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara katika Sekta Binafsi ina jukumu la kufanya utafiti na kumshauri waziri mwenye dhamana na masuala ya kazi kupanga na kutangaza kima cha chini cha mshahara kwa sekta husika.
“Kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi nchini kinawekwa kwa kuzingatia sekta za kiuchumi,” alisema. Aidha, upangaji wake unazingatia vigezo mbalimbali vilivyowekwa kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa na sheria za nchi, vinavyojumuisha uwezo wa waajiri kufanya biashara na kulipa ujira pamoja na gharama za maisha.

Post a Comment