Petroli, dizeli yashuka bei
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli zilizoanza kutumika jana, zikionesha petroli imeshuka kwa Sh 102 kwa lita, huku dizeli ikishuka kwa Sh 101.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Salum Mnuna juzi usiku ilisema kushuka kwa bei hiyo kunatokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali kuhakikisha bei himilivu za mafuta zinaendelea kuwepo nchini.
“Ewura imeendelea kufuatilia bei za mafuta ambazo zimekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara kutokana na vita inayoendelea eneo la Mashariki ya Kati. Kushuka kwa bei hizi pia ni matokeo ya hatua zinazochukuliwa na serikali,” alisema Mnuna.
Akichanganua kushuka kwa bei ya mafuta, Mnuna alisema bei kikomo za rejareja kwa mafuta ya petroli yaliyoingia kupitia Bandari ya Dar es Salaam ni Sh 3,796 kwa lita moja, huku dizeli ikiuzwa kwa Sh 3,877 na mafuta ya taa Sh 3,713 kwa lita moja.
Mwezi uliopita, bei kikomo za rejareja kwa petroli katika Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa Sh 3,898 kwa lita moja, huku dizeli ikiuzwa kwa Sh 3,978 na mafuta ya taa yaliuzwa kwa Sh 4,003 kwa lita moja.
Mnuna alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, Kifungu namba 166, bei za bidhaa za petroli zitaendelea kupangwa na soko huku mamlaka hiyo ikiendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei hizo kikomo.
Hata hivyo, alisema kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani, isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa kama zilivyokokotolewa.
Kadhalika, vituo vyote vya mafuta vinapaswa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.
“Pale inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani,” alisema Mnuna.

Post a Comment