SERIKALI YA MKOA WA RUVUMA YASIMAMISHA SHUGHULI MBESA KUPISHA UCHUNGUZI WA MAUAJI




Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ameagiza kusimamishwa kwa shughuli za kawaida katika Kata ya Mbesa, wilayani Tunduru, kuanzia sasa hadi Jumapili, Septemba 27, 2026, ili kutoa fursa kwa Jeshi la Polisi kukamilisha uchunguzi wa mfululizo wa matukio ya mauaji, vurugu, na uharibifu wa mali uliosababishwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji. 

Akitoa agizo hilo baada ya kufika katika eneo hilo akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ili kujionea hali halisi na kusikiliza kero za wananchi, Brigedia Jenerali Ahmed alieleza kuwa katika kipindi hicho cha siku tatu, duka moja pekee linalotoa huduma muhimu litaruhusiwa kufanya kazi chini ya uangalizi maalum wa vyombo vya usalama, huku shughuli nyingine zote zikisubiri hadi uchunguzi utakapokamilika na hali ya amani kutarajiwa kurejea.

Aliongeza kuwa uamuzi huo wa kusimamisha shughuli umezingatia uzoefu wa matukio ya huko nyuma ambapo hatua kama hiyo ilisaidia kwa kiasi kikubwa vyombo vya usalama kuwabaini na kuwakamata baadhi ya watuhumiwa waliokuwa wamejificha baada ya kuchochea au kushiriki katika vurugu hizo, huku pia akiagiza kuwekwa kwa kikosi kidogo cha askari katika eneo la msitu wa akiba ili kudhibiti mienendo ya watu wanaoingia na kutumia eneo hilo kinyume cha sheria. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Dennis Masanja, alibainisha kuwa Serikali inafanya uchunguzi wa matukio mazito ikiwemo kifo cha mfugaji aliyetoweka baada ya ng'ombe 180 kuchukuliwa, pamoja na mauaji ya mtu mwingine aliyeshambuliwa kwa kuchomwa kitu chenye ncha kali, matukio yaliyofuatiwa na vitendo vya uharibifu ikiwemo kuchomwa kwa baadhi ya majengo ya serikali na nyaraka muhimu.

Masanja aliwakumbusha wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kulipiza kisasi kwa njia haramu kama vile kukata mifugo, kushambulia watu, au kuharibu mali za umma, akisisitiza kuwa vitendo hivyo haviwezi kuwa suluhu ya migogoro na kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa wote watakaobainika kuhusika. 

Hoja hiyo iliungwa mkono na mmoja wa wananchi walioumia katika vurugu hizo, Fidea Oswadi Chale, anayefahamika zaidi kama Bibi Chale, aliyelalamikia kuharibiwa kwa nyumba na mali zake ikiwemo milango, geti, televisheni, na matangi ya maji, huku akisisitiza kuwa wananchi wanahitaji ulinzi wa kudumu na hatua kali zichukuliwe dhidi ya wote wanaovunja amani na kuongeza mateso kwa wananchi wasio na hatia. 

Akihitimisha maelekezo hayo, Brigedia Jenerali Ahmed alisisitiza kuwa serikali haitatumia suluhu ya kuwafukuza wafugaji kwa misingi ya kikabila, bali viongozi wamejipanga kuhakikisha makundi yote mawili yanatafutiwa njia ya kuishi kwa amani na kufuata sheria za matumizi sahihi ya ardhi, ikiwa ni pamoja na kuwataka wamiliki wa ardhi wanaowakodisha wafugaji kuangalia uwezekano wa kuwauzia maeneo hayo ili kuwa na makazi ya kudumu na kuepusha migogoro ya mara kwa mara.

No comments