Wawekezaji Watakiwa Kutumia Baraza la Masoko ya Mitaji Kutatua Migogoro Haraka




Msajili wa Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT), Mhe. Dkt. Martin Kolikoli, amewataka wadau na wawekezaji kulitumia baraza hilo kutatua migogoro ya kibiashara kwa haraka ili kuchochea ukuaji wa uwekezaji na uchumi wa Taifa.

Dkt Kolikoli alibainisha hayo wakati wa ziara yake katika Ofisi za Baraza la Ushindani (FCT) jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kiutendaji na mifumo ya kidijitali. 

Dkt. Kolikoli alieleza kuwa ziara hiyo inaisaidia CMT kujifunza kutoka FCT ambayo ina uzoefu wa miaka 20 na imetatua mashauri zaidi ya 500, ikilinganishwa na CMT iliyoanza kutekeleza majukumu yake takribani miaka mitatu iliyopita na kusajili migogoro sita, jambo litakalowezesha kuepuka changamoto na kuboresha utoaji wa huduma kwa wadau wa masoko ya mitaji na bidhaa. 

Alisisitiza kuwa mabaraza hayo yenye hadhi ya Mahakama Kuu yanalenga kurahisisha na kufupisha muda wa utatuzi wa migogoro ambayo ingeweza kuchukua muda mrefu mahakamani, ambapo kwa mujibu wa taratibu za CMT, mashauri yanapaswa kushughulikiwa ndani ya siku 90 ili kulinda imani ya wawekezaji, mabenki, mawakala, kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa, na washiriki wa soko la bidhaa wakiwemo wakulima na vyama vya ushirika. 

Aliongeza kuwa kasi ya utatuzi ni muhimu hasa katika masoko ya bidhaa na sekta ya fedha ili kuzuia bidhaa zilizohifadhiwa maghalani kupoteza ubora na kuepusha fedha kufungwa kwa muda mrefu, huku akiahidi kuwa CMT itaendelea kushirikiana na FCT ili kuimarisha uwezo wa watendaji na mifumo ya kidijitali. 

Kwa upande wake, Msajili wa Baraza la Ushindani (FCT), Mhe. Mbegu Kaskasi, alieleza kuwa baraza hilo lilianzishwa chini ya Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003 kushughulikia rufaa na migogoro ya kibiashara, akibainisha kuwa FCT imeshughulikia jumla ya mashauri 525 tangu kuanzishwa kwake na inapokea wastani wa mashauri 45 hadi 50 kila mwaka. 

Mhe. Kaskasi alikaribisha ushirikiano huo na kueleza kuwa baadhi ya mashauri yanahusisha uunganishaji na ununuzi wa kampuni zenye miamala ya matrilioni ya fedha, hivyo ushirikiano wa karibu kati ya FCT na CMT utaongeza ufanisi na kuhakikisha migogoro ya kibiashara inatatuliwa kwa wakati ili kutorudisha nyuma shughuli za wawekezaji na wafanyabiashara nchini.

No comments