Watanzania 174 waliokuwa wakiishi Afrika Kusini wameishukuru serikali kwa kuwarudisha nyumbani.
Watanzania hao kutoka Mji wa Durban katika Jimbo la Kwa Zulu Natal waliwasili nchini juzi saa nne usiku katika Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere kwa ndege ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).
Awali, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana alisema kundi la kwanza lingekuwa na Watanzania 241 kutoka Durban lakini waliofanikiwa kurejea ni 174.
Balozi Bwana alisema Watanzania 679 wanatarajiwa kurejea nchini kupitia mpango huo na akabainisha kuwa kundi la pili linatarajiwa kuwasili Septemba mwaka huu.
Kabla ya kuondoka huko Watanzania hao walifanyiwa uhakiki wa kumbukumbu zao na mamlaka za Afrika Kusini, ikiwemo uhamiaji na polisi na wenye kesi au uchunguzi walitakiwa kukamilisha taratibu za kisheria.
Baada ya kuwasili juzi baadhi ya Watanzania hao walisema hawana mpango wa kurudi Afrika Kusini. Pascal Ndagama alisema siku za mwisho Afrika Kusini zilikuwa za hofu kubwa na kuongeza kuwa anataka kujikita katika kilimo cha kisasa na uvuvi mkoani Kigoma.
Naye Rashid Ramadhani alisema aliishi Afrika Kusini kwa zaidi ya miaka 30 tangu akiwa na miaka 22.
“Leo ndiyo nimerudi nyumbani. Namshukuru sana Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea usafiri wa kurudi. Kule nimeacha mtoto na mali nilizochuma si nyingi, ila siwezi nikalilia mali kuliko uhai. Ilikuwa bora afya yangu na usalama wangu,” alisema Ramadhani.
Kwa upande wake, Mkutala Sivaye alisema kila siku za Alhamisi walikuwa wanaulizwa wangeondoka lini nchini humo.
“Sitorudi tena Afrika Kusini. Nitafanya biashara ndogondogo ili mradi tumerudi nyumbani. Kikubwa tunaishukuru serikali kwa kuturejesha salama,” alisema Sivaye.

Post a Comment