WATAALAMU OFISI YA WAZIRI MKUU WAREJESHA TABASAMU KWA WANANCHI MGOGORO WA ARDHI MTONI KIZINGA

Bw. Ivan Kihiyo
 

Timu ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotumwa na Waziri Mkuu kutatua mgogoro wa umiliki wa Kiwanja Na.2013 na 2014, Kitalu “U”, eneo la Mtoni Kizinga, Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam, uliodumu kwa miaka 17  imefanikisha maridhiano ya kumaliza mgogoro huo..

Mgogoro huo ulikuwa kati ya mfanyabiashara Hersi Warsame Mohamed na wananchi watano. 

Timu hiyo ya Waziri Mkuu chini ya uenyekiti wa Msaidizi wa Waziri Mkuu – Mahusiano, Asasi za Kiraia na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bw. Tryphone Mkolokoti na katibu wake Msaidizi wa Waziri Mkuu – Masuala ya Ardhi, Bw. Senso Magessa ,ilifanikiwa kufanikisha maridhiano hayo kwa kuzingatia taarifa ya uchunguzi wa mgogoro huo iliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), hukumu ya Mahakama katika kesi iliyofunguliwa na wananchi hao ambayo Bw. Hersi Warsame Mohamed alishinda, pamoja na maelezo ya Maafisa Ardhi kutoka Manispaa ya Temeke walioshiriki katika mchakato wa maridhiano.

Katika mgogoro huo, wananchi hao wakiongozwa na Bw. Ivan Kihiyo, walimwandikia barua Mheshimiwa Waziri Mkuu wakilalamika kuwa mfanyabiashara Hersi Warsame Mohamed amejimilikisha eneo lao kinyume cha sheria. Wananchi hao walimuomba Waziri Mkuu awasaidie kutatua mgogoro huo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu,utiaji saini wa makubaliano ya maridhiano hayo ulifanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu,Magogoni, jijini Dar es Salaam, na kushuhudiwa na Wataalamu wa Ardhi kutoka Manispaa ya Temeke, Bw. Salim Shedafa na Bw. Salim Urembo, pamoja na Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Pande zote mbili zilimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa utaratibu mzuri unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kutatua migogoro ya wananchi kwa njia ya mazungumzo na maridhiano.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, kiongozi wa wananchi hao, Bw. Ivan Kihiyo, alisema: “Tumefikia maridhiano haya kwa akili zetu wenyewe, bila kushurutishwa, na tumekubaliana kulimaliza suala hili kwa amani. Wenzetu hawakushurutishwa na sisi hatukushurutishwa.”

Naye Msemaji wa familia ya Bw. Hersi, Yassin Hersi Warsame, alimshukuru Mungu kwa mgogoro huo kumalizika kwa njia ya maridhiano. Alisema familia itaendelea na uwekezaji wake katika eneo hilo na kuchangia katika ujenzi wa Taifa la Tanzania bila bughudha.

Waziri Mkuu ameweka utaratibu wa kutatua baadhi ya migogoro mbalimbali ya wananchi inayomfikia kupitia mikutano ya hadhara na kwa njia ya barua, kwa kutumia Kamati yake ya Maridhiano, ambayo imeendelea kutatua migogoro mbalimbali kadiri inavyoagizwa na Waziri Mkuu.



No comments