Waganda waomboleza kifo cha Kapteni wa SC Villa David Owori
Soka la Uganda linaomboleza kifo cha kapteni wa klabu ya SC Villa, David Owori,(27) aliyekufa Jumatano baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana jijini Kampala .
Kiungo huyo aliripotiwa kuvamiwa jioni ya Jumanne alipokuwa anakaribia nyumbani kwake eneo la Makindye, na kukimbizwa katika Kliniki ya Case akiwa bado anajitambua kabla ya hali yake kuwa mbaya na kukata roho asubuhi ya Jumatano.
Uongozi wa SC Villa ulitoa taarifa ya kusikitisha ukieleza majonzi makubwa kwa kuondokewa na kiongozi wao bora huku ukitaka vyombo vya usalama kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusika na kitendo hicho cha kinyama.
Kifo cha mchezaji huyo kimeshtua jamii ya soka nchini Uganda, huku wachezaji, mashabiki, na viongozi wakitoa jumbe za rambirambi na kutaka uwepo wa usalama ulioboreshwa.
Owori alikuwa nguzo muhimu katika klabu hiyo inayoshikilia rekodi ya ubingwa nchini Uganda, ambapo hivi karibuni alikuwa amesaini mkataba mpya wa kusalia klabuni hapo hadi Januari 2027.
Mbali na kuichezea SC Villa, aliwahi pia kuitumikia timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, katika mchakato wa kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2021, huku mechi yake ya mwisho ikiwa ni Agosti 1 alipoiongoza timu yake kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Maroons FC katika michuano ya FUFA Super 8.

Post a Comment