TANZANIA KUNUFAIKA NA SH. BILIONI 10 ZA BIASHARA YA KABONI



Tanzania inatarajiwa kuingiza zaidi ya Sh bilioni 10 kutokana na mauzo ya biashara ya kaboni baada ya Serikali kuidhinisha miradi minne itakayouza tani milioni 4.2 za kaboni katika soko rasmi la kimataifa.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo tarehe Agosti 5, 2026.

Waziri Masauni amezitaja miradi iliyopata kibali kuwa ni nishati safi ya kupikia inayotekelezwa na Burn Manufacturing, programu ya athari za kijamii inayosimamiwa na AP Energy Group kwa kushirikiana na Sayari SA Limited, mradi wa maji safi wa Water Mission International Tanzania, na mradi wa majiko banifu unaotekelezwa na Bridge Carbon Tanzania Limited.

Amesema miradi hiyo itachangia kupunguza uzalishaji wa gesi joto kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama, kutengeneza ajira, na kusaidia utekelezaji wa lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 85 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Akifafanua zaidi, Waziri Masauni ameeleza kuwa mapato hayo yanatokana na asilimia nane ambayo Serikali hupata kutokana na mauzo ya kaboni kwa mujibu wa Kanuni za Usimamizi wa Biashara ya Kaboni, ambapo tani milioni 4.2 za kaboni zilizothibitishwa zina thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 52.1 (sawa na takribani Sh bilioni 135.5), huku Serikali ikitarajia kupata zaidi ya dola za Marekani milioni mbili, sawa na zaidi ya Sh bilioni 10.

“Fedha hizi zinatokana na juhudi za Serikali za kujenga mfumo imara wa biashara ya kaboni unaolinda maslahi ya taifa na kuongeza mchango wa sekta hii katika uchumi,” alisema Masauni na kusisitiza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Biashara ya Kaboni (NCMC) kilichoanzishwa chini ya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191.

Aliongeza kuwa hadi Julai mwaka huu, NCMC imesajili miradi 117 ya biashara ya kaboni, na Serikali itaendelea kutathmini miradi mingine katika sekta za maji, bioanuwai, usafiri na magari ya umeme ili kuongeza fursa zaidi.

Aidha, mradi wa maji utakaotekelezwa katika mikoa yote 26 nchini unatoa ajira kwa Watanzania 1,000 na kwa wasambazaji zaidi ya 100, huku miradi hiyo ikichangia upatikanaji wa maji safi na salama katika mikoa ya Kigoma na Dodoma na kunufaisha kaya zaidi ya milioni moja kwa maji safi na kutoa ajira zaidi ya 350 kwa Watanzania.

No comments