TRACY NABUKEERA AWEKA HISTORIA, ASHINDA TAJI LA MISS SUPRANATIONAL AFRICA 2026
Mtanzania Tracy Nabukeera ameweka historia ya kipekee katika tasnia ya urembo baada ya kuibuka mshindi wa taji la Miss Supranational Africa 2026 kwenye mashindano ya kimataifa ya Miss Supranational yaliyofanyika nchini Poland.
Ushindi huu unamfanya kuwa mwanadada wa kwanza kutoka Tanzania kutwaa taji hilo la barani Afrika, hatua inayozidi kuitangaza na kuing’arisha nchi katika majukwaa ya kimataifa.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Tracy ameeleza kuwa anajivunia sana kuwakilisha taifa na kuwashukuru Watanzania wote waliomwonyesha ushirikiano na kumuunga mkono tangu kuanza kwa safari yake hiyo ya ushindani.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo si yake peke yake bali ni ya Watanzania wote waliomuamini kubeba bendera ya taifa.
Aidha, mrembo huyo ameeleza kuwa anakusudia kutumia nafasi hiyo kama fursa ya kuitangaza Tanzania kimataifa pamoja na kutekeleza majukumu yake kama balozi mwema wa urembo na maendeleo.
Kwa mujibu wa waandaaji wa mashindano hayo, Tracy anatarajia kuwasili nchini usiku wa kuamkia Jumatatu, Agosti 3, majira ya saa 8:15 usiku kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Post a Comment