RAIS SAMIA AAGANA RASMI NA BALOZI WA MISRI NCHINI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri nchini, Mheshimiwa Sherif Ismail, aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kumuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake wa utumishi.
Katika mazungumzo yao, Rais Dkt. Samia amemshukuru Balozi Ismail kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa muda mrefu na wa kirafiki kati ya Tanzania na Misri katika kipindi cha miaka minne ya utumishi wake nchini.
Rais Dkt. Samia amesema Tanzania na Misri zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, elimu, afya, kilimo, nishati, utalii, usafiri na uchukuzi, pamoja na sekta nyingine.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu, Rais samia pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kupanua biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo ili kutumia kikamilifu fursa zilizopo na kuwaletea manufaa wananchi wa pande zote mbili.
Mazungumzo hayo pia yamegusia haja ya kuboresha miundombinu na huduma za usafiri na uchukuzi ili kurahisisha biashara kati ya Tanzania na Misri, pamoja na masoko mengine barani Afrika.
Katika sekta ya elimu, Rais Dkt. Samia ameishukuru Misri kwa kuendelea kutoa ufadhili wa nafasi za masomo, mafunzo na programu mbalimbali za kuwajengea uwezo Watanzania.
Viongozi hao pia wamejadili kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya, ikiwemo kutoa mafunzo kwa wataalamu, kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba na kuendeleza uzalishaji wa dawa.
Kwa upande wake, Balozi Ismail amemshukuru Rais Dkt. Samia, Serikali na wananchi wa Tanzania kwa ushirikiano, msaada na ukarimu alioupata katika kipindi chote cha utumishi wake nchini.
Amesema miaka yake minne nchini Tanzania imekuwa sehemu muhimu na ya kukumbukwa katika utumishi wake, na kuthibitisha kuwa urafiki kati ya Tanzania na Misri utaendelea kudumu.
Rais Dkt. Samia amemtakia Balozi Ismail mafanikio katika majukumu yake yajayo na kueleza imani kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Misri utaendelea kuimarika kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.

Post a Comment